NA MWANDISHI WETU
Tanzania kupitia kwa Mwakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Barani Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutokomeza Jangwa na Ukamwe (UNCCD) ambae pia ni Mwenyekiti wa chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) Dkt. Ellen Okoedion,leo Juni 17,2026 inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame (UNCCD Day 2026).
Siku hii huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha hatua za kulinda ardhi, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya ukame na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Rangelands: Recognize. Respect. Restore”, ikimaanidha “Tambua Ardhi ya Malisho. Waheshimu Wafugaji. Rejesha Ardhi Iliyoharibika.”
Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha jamii kutambua thamani ya maeneo ya malisho, nyanda kavu, savanna na mifumo mingine ya ardhi inayotegemewa na mifugo, wanyamapori, vyanzo vya maji, bioanuai na maisha ya mamilioni ya watu duniani.
Dkt. Ellen anasema kuwa kwa Tanzania, ujumbe huu una uzito wa kipekee kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya mifugo katika uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi wa vijijini. Maeneo ya malisho si ardhi tupu kama ambavyo mara nyingi hufikiriwa ni mifumo hai inayozalisha chakula, kipato, ajira na kuhifadhi utamaduni wa jamii nyingi za wafugaji na wakulima-wafugaji.
“Takwimu za sekta ya mifugo zinaonesha kuwa Tanzania ina takribani ng’ombe milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8 na kondoo milioni 5.3. Mifugo hii ndiyo tegemeo la mamilioni ya wananchi kwa chakula, lishe, biashara na kipato.
“Hata hivyo, uwezo wa sekta hii kuendelea kuchangia maendeleo ya taifa unategemea afya ya maeneo ya malisho yanayoiwezesha kuishi.
“Kwa sasa, maeneo mengi ya malisho nchini yanakabiliwa na changamoto kubwa zinazotishia mustakabali wake. Mabadiliko ya tabianchi, ukame wa mara kwa mara, uharibifu wa ardhi, kupungua kwa maeneo ya malisho, uhaba wa maji, kuenea kwa mimea vamizi na matumizi yasiyo endelevu ya ardhi vinaendelea kuongeza shinikizo kwa jamii zinazotegemea rasilimali hizo.”Amesema.
Ameongeza kuwa wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa athari za uharibifu wa malisho haziishii kwenye mazingira pekee, zinagusa usalama wa chakula, upatikanaji wa maji, amani katika jamii, ajira za vijana, usawa wa kijinsia na maendeleo ya uchumi kwa ujumla.
Katika muktadha huo, maadhimisho ya mwaka huu yanakuja wakati ambapo Umoja wa Mataifa umetangaza mwaka 2026 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Malisho na Wafugaji, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa dunia kuhusu mchango wa maeneo ya malisho na watu wanaoyasimamia katika kuhifadhi mazingira na kuimarisha usalama wa chakula.
Aidha, dunia inaelekea kwenye Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD COP17), utakaofanyika jijini Ulaanbaatar,
Mongolia, kuanzia Agosti 17 hadi 28, 2026.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili kwa kina masuala ya urejeshaji wa ardhi, ustahimilivu dhidi ya ukame, usalama wa chakula na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Ellen anaweka wazi kuwa katika kuadhimisha siku hii, asasi za kiraia ndani na nje ya Tanzania zinatoa wito kwa serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, vyombo vya habari na wananchi
kwa ujumla kuongeza juhudi za kulinda na kurejesha maeneo ya malisho yaliyoharibiwa.
Wito huo unasisitiza mambo manne muhimu.
Kwanza, maeneo ya malisho yatambuliwe kama rasilimali muhimu za taifa. Maeneo haya yana mchango mkubwa katika uzalishaji wa mifugo, uhifadhi wa bioanuai, utalii wa wanyamapori, upatikanaji wa maji na ustahimilivu wa mazingira. Kupotea kwake kunahatarisha usalama wa chakula na uchumi wa taifa.
Pili, wafugaji watambuliwe kama sehemu ya suluhisho badala ya kuonekana kama chanzo cha matatizo. Maarifa yao ya jadi kuhusu usimamizi wa malisho, uhamaji wa mifugo na matumizi ya rasilimali katika nyanda kavu ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na ukame na mabadiliko ya tabianchi.
Tatu, urejeshaji wa malisho uzingatie mahitaji ya jamii. Hili linahusisha kulinda maeneo ya malisho, kutambua njia za mifugo, kusimamia vyanzo vya maji, kurejesha nyasi za asili, kudhibiti mimea vamizi na kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema dhidi ya ukame.
Nne, wanawake na vijana washirikishwe kikamilifu katika maamuzi yanayohusu usimamizi wa malisho. Wanawake wana mchango mkubwa katika usalama wa chakula wa kaya na uchumi wa familia, huku vijana wakibeba fursa za ubunifu, teknolojia za kidijitali, ajira za kijani na ujasiriamali wa mazingira.
Wadau wa mazingira wanaeleza kuwa ukame hauanzi wakati mifugo inapokufa au mazao yanapoharibika. Huanzia pale jamii zinaposhindwa kulinda ardhi, vyanzo vya maji na mifumo ya ikolojia inayowezesha maisha kuendelea.
Kwa sababu hiyo, Tanzania inapaswa kubadili mtazamo kutoka katika kushughulikia majanga baada ya kutokea kwenda katika kuwekeza kwenye maandalizi, usimamizi endelevu wa ardhi na ushirikiano kati ya wakulima, wafugaji, serikali za mitaa na wadau wa maendeleo.
Kadri taifa linavyojiandaa kushiriki mijadala ya kimataifa kuelekea COP17, kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika mipango ya matumizi ya ardhi, usimamizi wa rasilimali za maji, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa, ushiriki wa jamii, uongozi wa wanawake na uwezeshaji wa vijana katika sekta ya mazingira.
Siku ya UNCCD 2026 inatoa fursa muhimu ya kutafakari ukweli kwamba ardhi yenye afya ndiyo msingi wa maisha. Ardhi inapolindwa na kurejeshwa, mifugo hustawi, uzalishaji huongezeka, vyanzo vya maji huimarika, migogoro hupungua na jamii hupata uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kimazingira.
Ujumbe wa mwaka huu unaweka wazi hilo kwa kusema:Tutambue ardhi ya malisho, tuwaheshimu wafugaji na turejeshe ardhi iliyoharibika kabla ukame haujageuka kuwa janga.
0 Comments