Ticker

7/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY: KILA MTANZANIA KUPATA BIMA YA AFYA

 

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Baada ya kubaini changamoto ambazo Wananchi wamekuwa wakikabiliana nazo kwenye gharama za matibabu, sasa serikali ipo tayari kuupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Januari 23, 2023 Jijini Dar es Salaam mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa lengo la kuwafahamisha juu ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.


Baadhi ya Wahariri wakimsikiliza Waziri Ummy

Amesema mara baada ya Muswada huo kupitishwa na Wabunge na kuwa sheria kamili, Serikali inafikiria kuifungamanisha sheria hiyo na baadhi ya upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile leseni ya biashara, udereva au kitambulisho cha taifa.

"Hatutamuacha nyuma Mtanzania yeyote katika huduma ya afya, nawaomba wananchi anzeni kudunduliza ili mkate bima ya afya, ninataka muamini bima ya afya si kwa wagonjwa pekee hata wazima wanatakiwa kuwa na bima ya afya." 

Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema ipo haja kwa Wahariri wa vyombo vya habari kuibeba ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote, huku akibainisha kuwa itakapopitishwa na Bunge kuwa Sheria kamili italeta faraja na kuwa msaada mkubwa kwa Wananchi ambao wamekuwa wakibeba mzigo wa kulipia gharama kubwa za Matibabu.

"Niwaombe ndugu zangu Wahariri wa vyombo vya habari mliopo hapa, tulibebe jambo hili ambalo kwa hakika litakuwa na tija kwa Taifa, ninafahamu nguvu ya kalamu zenu kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili."

Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodautus Balile ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa Wahariri na vyombo vya habari katika kuisukuma ajenda ya Bima ya Afya kwa wote, na kuahidi kuwa wahariri watashiriki kikamilifu kuuelimisha umma juu ya suala hilo.

 


Post a Comment

0 Comments