Ticker

7/recent/ticker-posts

MWANZIVA: NGO's ZINAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KULETA MAENDELEO KWA WANANCHI


NA HADIJA OMARY -AFRINEWSSWAHILI-LINDI

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bi. Victoria Mwanziva, amesema mashirika yasiyo ya Kiserikali yameendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,  katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii.

Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Usanifu wa Programu ya Maendeleo Kiwalala, Halmashauri ya Mtama, Mwanziva alibainisha kuwa Serikali inatambua mchango wa wadau wa maendeleo katika kujaza pengo linaloweza kutokea kutokana na ufinyu wa rasilimali.


“Serikali inafanya kazi kubwa katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na Ufugaji na nyinginezo Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa nchi yetu, tunahitaji kushirikiana na wadau kama World Vision ili huduma ziweze kufika katika maeneo yote. Hili ni kuunga mkono moja kwa moja mwelekeo wa Serikali,” alisema.


Mwanziva aliongeza kuwa uzoefu wa mradi wa Nyangamara unaotekelezwa na World Vision umeonyesha mafanikio makubwa katika kugusa jamii, hivyo kupelekea kuanzishwa kwa Programu nyingine ya Kiwalala ambayo itapanua wigo na kugusa kata nyingine tatu.


Programu ya Maendeleo Kiwalala inatarajiwa kuwanufaisha wananchi wapatao 24,000 wa Kata za Mtua, Longa na Kiwalala katika Halmashauri ya Mtama. Ni programu ya pili baada ya Nyangamara ambayo ipo mwaka wake wa kwanza wa utekelezaji.


Mkurugenzi wa Ubora wa Programu na Mkakati wa World Vision Tanzania, Bw. Simon Moikan, alieleza kuwa hatua iliyofikiwa ni kukamilisha uchambuzi wa maoni ya wananchi. Maoni hayo yataandaliwa kuwa andiko rasmi la programu ambalo litawasilishwa katika Ofisi Kuu ya World Vision Marekani kwa ajili ya uidhinishaji wa mwisho.


Alisema kuwa baada ya kukamilika kwa andiko, shirika litaanza zoezi la uandikishaji wa watoto walengwa sambamba na kuandaa mpango kazi na bajeti. Anatarajia utekelezaji wa programu kuanza mwezi Oktoba, 2026 kwa muda wa miaka 10.


Katibu Tawala wa Wilaya ya Lindi, Bw. Udhaifu Rashid, aliwaomba wananchi wa maeneo husika kutoa ushirikiano kamili kwa World Vision ili kuhakikisha programu inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta tija iliyokusudiwa.


Wananchi wa Kiwalala na Mtua wameipongeza Serikali kwa kuwezesha mazingira wezeshi kwa wadau.   wamesema wanatamani kuona programu ikijikita katika elimu, afya lishe , ulinzi wa watoto na uwezeshaji wa kaya ili kuboresha maisha yao.

Post a Comment

0 Comments