NA. FATMA JALALA
Katika kipindi cha hivi karibuni, baadhi ya maeneo nchini Tanzania, ikiwemo Kigamboni,Kimara na kwengineko jijini Dar es Salaam, imeshuhudiwa kuibuka kwa taharuki ya kijamii kufuatia madai ya “kuibiwa” kwa via vya uzazi vya wanaume al maarufu nyeti. Tukio mojawapo lililoshuhudiwa linahusisha kijana aliyeshambuliwa karibu kupoteza maisha baada ya kushukiwa kuhusika na kile kilichoelezwa kuwa wizi wa viungo vya siri vya kijana mwenzake.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kijana aliyedai kuibiwa alikuwa akilia kwa uchungu, akisisitiza kuwa via vyake vya uzazi vilikuwa vimepotea ghafla baada ya kushikwa bega na mtuhumiwa. Hali hiyo ilichochea hasira za wananchi waliomshambulia mtuhumiwa kabla ya askari polisi kufika eneo la tukio na kuwachukua wahusika kwa ajili ya usalama na uchunguzi zaidi.
Taharuki hii imeenea kwa kasi nchini kupitia mazungumzo ya mitaani na mitandao ya kijamii, na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa vijana wengi. Baadhi yao wameanza kuishi kwa hofu na hata kuchukua hatua za kujilinda zisizo na msingi wa kisayansi, ikiwemo kuvaa pini mikononi wakiamini kuwa ni kinga dhidi ya tukio hilo.
Kwa mtazamo wa kitaalamu wa saikolojia, hali hii haiwezi kuelezwa kama tukio la kimwili pekee, bali ni matokeo ya mwingiliano kati ya hofu ya kisaikolojia na ushawishi wa kijamii. Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa hali hii inafanana na ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama Koro syndrome, ambapo mhusika hupata hofu kali kwamba sehemu za siri zinajikunyata au kupotea, na kuamini hali hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa, hata kifo.
Dalili zake ni pamoja na hofu ya ghafla, wasiwasi mkali, na imani thabiti ya kuwepo kwa mabadiliko yasiyo ya kawaida mwilini. Mara nyingine, mhusika huchukua hatua za kujilinda kama kushika au kuvuta sehemu husika akiamini anazuia madhara zaidi. Hata hivyo, tafiti za kitabibu zinaonyesha kuwa mara nyingi hakuna mabadiliko halisi ya kimaumbile, bali ni tafsiri potofu ya mwili inayochochewa na hofu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hali kama hizi zinaweza kuelezeka kitaalamu kama mass hysteria (hofu ya pamoja), ambapo jamii huathiriwa na taarifa zisizo na uhakika lakini zenye kuchochea hofu. Hali hii husababisha watu wengi kuamini jambo moja kwa wakati mmoja bila ushahidi wa kisayansi, jambo linalojulikana pia kama social contagion yaani maambukizi ya hofu ndani ya jamii.
Aidha aliyekuwa Mwanafalsafa na mwanasaikolojia wa kijamii marehemu Gustave Le Bon kutoka nchini Ufaransa aliwahi kueleza kuwa katika mazingira ya umati, hisia za mtu mmoja zinaweza kusambaa kwa wengine kwa haraka na kusababisha kundi zima kuathirika bila kufanya uchambuzi wa kina. Hii inaeleza kwa nini taharuki ya aina hii huenea kwa kasi na kuathiri watu wengi kwa wakati mmoja.
Aidha, wataalamu wa afya ya akili nchini, hususan kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamekuwa wakisisitiza kuwa imani za kijamii na mitazamo ya kitamaduni kuhusu mwili na uzazi zina mchango mkubwa katika kuibua na kueneza hofu za aina hii. Msongo wa mawazo, ukosefu wa elimu sahihi, na mazingira ya kijamii yenye taarifa zisizo sahihi vinaweza kumfanya mtu kuamini jambo lisilo na msingi wa kitabibu.
Ni muhimu pia kuelewa kuwa hata mabadiliko ya kawaida ya mwili yanapotafsiriwa kwa hofu yanaweza kuonekana kama tatizo kubwa, jambo linaloongeza mzigo wa kisaikolojia kwa mhusika.
Katika kukabiliana na hali hii, jamii inapaswa kuongozwa na utulivu, elimu sahihi na uwajibikaji wa pamoja. Wananchi wanapaswa kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa na badala yake kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya pamoja na kufuata miongozo ya mamlaka husika.
Zaidi ya hayo, historia inaonyesha kuwa taharuki za aina hii zinaweza kusababisha madhara makubwa ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kuwashambulia au kuwasingizia watu wasio na hatia.
Kwa hiyo, katika kipindi hiki cha sintofahamu, silaha muhimu si hofu bali ni uelewa. Kupitia elimu sahihi ya kisaikolojia na mshikamano wa kijamii, jamii inaweza kukabiliana na hali hii kwa utulivu na kurejesha usalama.
0 Comments