Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo.
NA JIMMY KIANGO
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania imekanusha uwepo wa dawa (Kapsuli) zenye misumari ndani yake na kueleza kuwa video iliyobeba maudhui hayo imetengenezwa kwa lengo la kupotosha umaa na kuzua taharuki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 6,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, video hiyo imeandaliwa kwa lengo la kupotosha na kuzua hofu. Kufungua kapsuli na kuweka vitu vya kigeni ni mbinu inayotumiwa na watu wasio waaminifu kutengeneza maudhui ya kushtusha.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa dawa zote zinazoingia nchini hukaguliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba
“Hivi karibuni kumekuwa na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mtu akifungua kapsuli na kutoa vitu vinavyofanana na misumali midogo. Tunapenda kufahamisha umma kuwa:-
Video hii imeandaliwa kwa lengo la kupotosha na kuzua hofu. Kufungua kapsuli na kuweka vitu vya kigeni ni mbinu inayotumiwa na watu wasio waaminifu kutengeneza maudhui ya kushtusha.
“Dawa zote zinazoingia nchini hukaguliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA). Aidha, viwanda vya dawa vina mifumo ya mashine inayozalisha maelfu ya vidonge kwa dakika, na haiwezekani kitaalamu kwa msumali mmoja mmoja kuingizwa ndani ya kapsuli moja.”
Taarifa imebainisha kuwa iwapo kungekuwa na kitu kigumu kama msumali ndani ya kapsuli, mashine za kufunga dawa (blister packing) zingeharibika au kushindwa kufunga kidonge hicho vizuri.
“TMDA inashauri jamii kuendelea kutumia dawa kama tunavyoelekezwa na wataalam wa afya na kuhakikisha kuwa tunanunua dawa kwenye sehemu za kutolea huduma ya dawa (Famasi au Duka la Dawa Muhimu) au sehemu za kutolea huduma ya tiba kama zahanati, kituo cha afya au hospitali iliyosajiliwa.
“Vilevile, TMDA inatoa wito kwa wananchi kuwa ukihisi au kuona kitu kisicho cha kawaida kwenye dawa yako, usikimbilie mitandaoni, badala yake unaombwa kutoa taarifa ofisi za TMDA Makao Makuu na ofisi za Kanda zilizopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Songea, Tabora na Geita au kupitia barua pepe ya info@tmda.go.tz, ofisi za afya za Halmashauri au kupiga simu bila malipo kupitia Na.0800110084.
“Aidha, tunaomba wananchi kuacha kusambaza video hizo kwani zinaingilia matibabu ya wagonjwa na kusababisha hofu isiyo na msingi.”
0 Comments