Miaka kadhaa tangu kuondoka kwake duniani, bado mchango wake unaonekana kupitia wasanii aliowalea, aliowaamini na aliowapa nafasi ya kung’ara kwenye tasnia ya maigizo ya Bongo Movie.
Siku za hivi karibuni, gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii limekuwa ni taarifa za Patrick Kanumba kubarikiwa mtoto, jambo lililowagusa mashabiki wengi waliokuwa wakifuatilia maisha yake kwa karibu.
Kupitia picha na video zinazosambaa mtandaoni, Patrick ameonekana akiwa amembeba mtoto huyo kwa furaha na upendo mkubwa, hali iliyotafsiriwa na wengi kuwa mwanzo mpya wa maisha yake ya kifamilia.
Kilichozidi kuwavutia mashabiki ni hatua ya Patrick kuambatana na Jenifa kwenda nyumbani kwa Mama Kanumba kwa ajili ya kumsalimia na kumtambulisha mtoto huyo. Ziara hiyo imeonekana kuwa ya kipekee kwa sababu imeibua hisia nzito za kumbukumbu za familia ya Kanumba pamoja na mshikamano ulioendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Steven Kanumba.
Katika picha na video zilizozagaa mitandaoni, Mama Kanumba ameonekana akiwa mwenye furaha kubwa kumbeba mtoto huyo anayeelezwa kuwa mjukuu wake. Watu wengi waliguswa na namna familia hiyo ilivyoonesha upendo na umoja, huku wengine wakisema tukio hilo limerudisha kumbukumbu za siku ambazo Steven Kanumba alikuwa hai na akisimamia kwa karibu maisha ya ndugu zake pamoja na wasanii aliowazunguka.
Hata hivyo, jambo lililoendelea kuwa mjadala mkubwa ni kutofahamika rasmi mama wa mtoto huyo ni nani. Mpaka sasa, haijawekwa wazi kama mtoto huyo ni wa Jenifa au Patrick amepata mtoto huyo na mwanamke mwingine.
Kutokuwepo kwa taarifa rasmi kumeongeza maswali mengi kutoka kwa mashabiki wa burudani nchini, huku wengi wakisubiri wahusika wenyewe kuweka wazi ukweli wa jambo hilo.
Mitandao ya kijamii imejaa pongezi kwa Patrick Kanumba, ambapo mashabiki wengi wameeleza kufurahishwa na kumuona akiingia kwenye hatua mpya ya ubaba. Wengine wameandika kuwa familia ya Kanumba inaendelea kukua na kwamba mtoto huyo ni baraka nyingine kwa familia hiyo iliyowahi kupitia kipindi kigumu baada ya kumpoteza Steven Kanumba mwaka 2012.
Mbali na taarifa za mtoto huyo, wengi wamejikuta wakikumbuka nafasi kubwa aliyokuwa nayo marehemu Steven Kanumba katika kuwaibua Patrick na Jenifa kwenye sanaa ya uigizaji.
Kabla ya kuwa majina yanayotambulika leo, Patrick akiwa mdogo kabisa hakuwa akijulikana hadi pale Kanumba alipompa nafasi ya kuigiza nae kwenye filamu ya Ucle JJ na This is it.
Filamu hizo zilimpa mwanga Patrick na Jenifa na kujifunza misingi ya sanaa, namna ya kusimama mbele ya kamera na mbinu za kuigiza zinazoweza kugusa hisia za watazamaji.
Inaelezwa kuwa Steven Kanumba alikuwa mtu aliyependa sana kuwainua vijana wenye vipaji. Alitumia umaarufu wake kuwapa nafasi wasanii wachanga kushiriki katika filamu zake ili waweze kujifunza na kujitangaza. Kupitia mazingira hayo, Patrick alipata nafasi ya kuonekana kwenye kazi mbalimbali za filamu na taratibu kujijengea jina lake mwenyewe ndani ya tasnia.
Kwa upande wa Jenifa, wadau wengi wa filamu wanakumbuka namna alivyoanza kuonekana kwenye kazi zilizokuwa zikihusishwa na kundi la wasanii waliokuwa karibu na Steven Kanumba. Kupitia ushauri, mafunzo na mazingira aliyoyaweka Kanumba, Jenifa naye aliweza kujiamini zaidi kwenye uigizaji na kuanza kujijengea nafasi yake kwenye tasnia ya filamu za Tanzania.
Wengi wa waliowahi kufanya kazi na Steven Kanumba wamekuwa wakisema kuwa alikuwa zaidi ya mwigizaji; alikuwa mlezi wa vipaji. Aliamini kuwa mafanikio ya sanaa hayawezi kujengwa na mtu mmoja pekee, bali kwa kusaidiana na kupeana nafasi. Ndiyo maana hadi leo, baadhi ya wasanii waliopata nafasi kupitia kwake bado wanamtaja kama mtu aliyebadilisha maisha yao kisanaa.
Ziara ya Patrick na Jenifa nyumbani kwa Mama Kanumba imeonekana pia kama ishara ya kuendelea kuthamini mchango wa Steven Kanumba katika maisha yao. Kwa mashabiki wengi, tukio hilo halikuwa tu la kumtambulisha mtoto, bali pia lilikuwa kumbukumbu hai ya urithi wa Kanumba kwenye sanaa ya Tanzania.
Tasnia ya filamu nchini imeendelea kubadilika kwa kasi kubwa tangu kuondoka kwa Steven Kanumba, lakini bado jina lake linaendelea kutajwa kila inapozungumziwa historia ya mafanikio ya Bongo Movie. Filamu zake bado zinatazamwa na vizazi vipya, huku baadhi ya wasanii aliowalea wakiendelea kufanya kazi zinazobeba alama ya mafunzo aliyowaachia.
Kwa sasa, macho ya mashabiki wengi yameelekezwa kwa Patrick Kanumba wakisubiri kujua ukweli zaidi kuhusu mtoto huyo pamoja na maisha yake ya familia. Licha ya sintofahamu iliyopo kuhusu mama wa mtoto huyo, jambo lililo wazi ni kwamba tukio hilo limeleta furaha kubwa ndani ya familia ya Kanumba na kwa mashabiki wao.
Katika ulimwengu wa burudani ambao mara nyingi hujaa migogoro na maneno mengi, picha za Patrick, Jenifa na Mama Kanumba zimeonekana kuwa na ujumbe wa upendo, mshikamano na kuendeleza familia. Wapo wanaoamini kuwa huenda huu ukawa mwanzo wa ukurasa mpya wenye matumaini makubwa kwa familia hiyo maarufu katika tasnia ya filamu Tanzania.
0 Comments