| Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni. |
Kongamano hilo lililopangwa kufanyika Mei 28, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), lina lengo la kuwapa nafasi wataalamu kutafuta njia rafiki za kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kongamano hilo litakwenda sambamba na uzinduzi wa Kongamano la Wadau wa Mazingira (COSE) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC.
Akilitangaza kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amesema Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2026 pia yataambatana na matukio mbalimbali ya kitaifa yenye lengo la kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwakutanisha wadau wa mazingira kujadili masuala muhimu ya mazingira nchini.
Waziri Masauni amebainisha kuwa mbali na kutoa elimu kwa umma kuhusu uhifadhi wa mazingira, lakini pia kutakuwa na shughuli ya upandaji miti itakayofanyika Mei 15 katika eneo la Bwawa la Kidete wilayani Kilosa mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.
Aidha, Mei 26, 2026 kutafanyika Kongamano la Vijana kuhusu uhifadhi ya Mazingira katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa lengo la kuwajengea vijana uelewa na ushiriki katika agenda ya mazingira nchini.
Mei 29, 2026 itakuwa ni kilele cha Maadhimisho ya Miaka 40 ya NEMC tangu kuanzishwa kwake ambayo yatakayofanyika katika Ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salaam.
Aidha Waziri Masauni alisema kuanzia Juni 1 hadi 5, 2026 kutakuwa na maonesho ya teknolojia na ubunifu wa shughuli za uhifadhi wa mazingira katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Maonesho hayo yatashirikisha wizara, taasisi za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau mbalimbali huku zaidi ya mabanda 100 yakitarajiwa kuwepo.
Pia kutakuwa na uzinduzi wa Kituo cha Afrika cha Vijana cha Kujenga Uwezo kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Ofisi ya Kikanda ya Afrika ya Mfuko wa Upotevu na Hasara zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani nchini kitakuwa ni Juni 5, 2026 na yatahitimishwa katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambapo kauli mbiu ya kitaifa ni “Dira 2050: Tuwajibike kukijanisha Tanzania.” huku kimataifa ni "Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Vitendo".
0 Comments