NA. FATMA JALALA
Katika zama hizi za kidijitali, jamii imejikuta katika mabadiliko makubwa ya namna taarifa zinavyotengenezwa na kusambazwa. Leo hii, karibu kila mwenye simu janja ana uwezo wa kufikisha ujumbe kwa hadhira kubwa ndani ya muda mfupi. Hali hii imeibua kundi jipya la watengeneza maudhui mtandaoni, ambao kwa kasi kubwa wameanza kuonekana kama sauti mbadala ya kuielimisha na kuhamasisha jamii. Hata hivyo, mabadiliko haya yameibua swali nyeti na la msingi: je, mtengeneza maudhui ana nafasi sawa na mwandishi wa habari, au tofauti yao ni kama ile ya mganga wa jadi na daktari?
Ni muhimu kuelewa kuwa uandishi wa habari si kazi ya kubahatisha, bali ni taaluma inayosimamiwa na sheria, maadili na misingi ya uwajibikaji. Kupitia Media Services Act, 2016, mwandishi wa habari anatambuliwa kisheria na kulazimika kufuata taratibu maalum ikiwemo kupata ithibati, kuheshimu maadili ya taaluma na kuwajibika kwa taarifa anazozitoa. Sheria hiyo inamweka mwandishi katika nafasi ya kipekee ya kuwa mhimili wa ukweli na uwazi katika jamii, huku ikitoa adhabu kwa yeyote anayekiuka misingi hiyo.
Kwa upande mwingine, watengeneza maudhui mtandaoni wameibuka kama nguvu kubwa ya mawasiliano, wakivutia hadhira kwa kutumia ubunifu, lugha rahisi na mbinu zinazogusa hisia za watu. Wana uwezo mkubwa wa kufikia watu wengi kwa haraka na hata kubadilisha mitazamo ya jamii. Hata hivyo, tofauti na waandishi wa habari, hawana mfumo maalum wa kisheria unaowasimamia kama taaluma. Wanachoguswa nacho kwa sasa ni sheria za jumla kama Cybercrimes Act, 2015, ambayo inalenga zaidi kudhibiti makosa ya kimtandao kama usambazaji wa taarifa za uongo au udanganyifu, lakini haijajenga mfumo wa maadili, ithibati na uwajibikaji wa kitaaluma kwa watengeneza maudhui.
Hapa ndipo tunapopaswa kujiuliza kwa uzito zaidi: katika mazingira haya, nani ana uhalali wa kuielimisha jamii? Jibu lake linapatikana katika msingi mmoja muhimu kuwa katika masuala ya kuielimisha jamii, uwezo unaweza kuvutia, lakini ni wajibu unaojenga uhalali; na bila uhalali, elimu hubaki kuwa maoni. Watengeneza maudhui wana uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe, lakini uwezo huo haujaambatana na wajibu wa kuhakikisha ukweli na uwajibikaji wa kile kinachotolewa. Kwa upande mwingine, mwandishi wa habari anabeba wajibu huo kwa mujibu wa sheria na taaluma.
Ndiyo maana kulinganisha nafasi hizi mbili ni sawa na kulinganisha mganga wa jadi na daktari. Mganga wa jadi anaweza kusaidia, anaweza kuaminika na jamii, na anaweza kuwa na uzoefu wa muda mrefu. Lakini daktari ndiye mwenye mafunzo rasmi, uthibitisho na uwajibikaji wa kisheria. Vivyo hivyo, mtengeneza maudhui anaweza kuhamasisha na kuelimisha kwa namna yake, lakini mwandishi wa habari ndiye mwenye uhalali wa kitaaluma wa kufanya hivyo kwa misingi ya ukweli uliothibitishwa.
Kinachotia wasiwasi zaidi katika mwelekeo huu mpya ni namna wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za umma na binafsi, wanavyoanza kuwapa kipaumbele kikubwa watengeneza maudhui na watu wenye ushawishi mtandaoni, hata kufikia hatua ya kuwalipa fedha nyingi zaidi kuliko waandishi wa habari wenye taaluma. Hii ni hali inayohitaji kutazamwa kwa jicho la kina, kwani inaibua maswali mazito kuhusu mustakabali wa taaluma ya uandishi wa habari.
Je, mwelekeo huu unalenga kuua taaluma ya habari kwa kuipa uzito burudani na mvuto kuliko ukweli na uwajibikaji? Au ni jaribio la kuiboresha taaluma hiyo kwa kuilazimisha kwenda sambamba na ushindani wa kidijitali? Ukweli ni kwamba ushindani wowote usiozingatia misingi ya taaluma unaweza kuleta madhara makubwa badala ya maendeleo.
Kuwapa kipaumbele watengeneza maudhui kwa sababu ya umaarufu wao pekee, bila kuzingatia ubora na ukweli wa taarifa wanazotoa, kunaweza kusababisha kuporomoka kwa viwango vya mawasiliano ya umma. Jamii inaweza kuanza kupokea na kuamini taarifa zisizo sahihi, hali ambayo inaweza kuathiri maamuzi muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, uchumi na utawala.
Hata hivyo, si sahihi pia kupuuza mchango wa watengeneza maudhui. Wao ni sehemu ya uhalisia wa dunia ya leo, na wana nafasi muhimu katika kufikisha ujumbe kwa watu wengi kwa lugha rahisi na inayovutia. Changamoto iliyopo si uwepo wao, bali ni namna wanavyowekwa katika mizani sawa na wataalamu waliofunzwa na kuthibitishwa.
Ni wajibu wa serikali na wadau kuweka mizania sahihi itakayolinda taaluma ya uandishi wa habari bila kuzuia ubunifu wa kidijitali. Hii inaweza kufanyika kwa kuhuisha sera na sheria ili ziendane na mazingira ya sasa, pamoja na kuweka miongozo itakayowalinda wananchi dhidi ya upotoshaji wa taarifa kutoka katika majukwaa ya mtandaoni.
Mwisho wa yote, jamii inapaswa kufahamu kuwa si kila anayezungumza ana uhalali wa kuongoza fikra za umma. Tofauti kati ya mtengeneza maudhui na mwandishi wa habari ni kubwa na ya msingi, sawa na ile ya mganga wa jadi na daktari. Wote wanaweza kusaidia, lakini mmoja ana wajibu, uthibitisho na uhalali wa kitaaluma.
Ikiwa tunataka kulinda ukweli na mustakabali wa taarifa sahihi katika jamii, hatuna budi kuitambua, kuithamini na kuilinda taaluma ya uandishi wa habari. Vinginevyo, tutakuwa tunajenga jamii inayosukumwa na mvuto wa maneno badala ya uzito wa ukweli.
0 Comments