Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA YAAHIDI KUIMARISHA HATUA DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI NA UHAMIAJI

 

James Chuyi, Afisa Mazingira , Ofisi ya Makamu wa Rais 


NA SIDI MGUMIA, DAE ES SALAAM 

Serikali ya Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuimarisha mikakati ya kitaifa na kikanda ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uhamiaji wa watu unaochochewa na athari za hali ya hewa.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na James Chuyi, Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, katika Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Utekelezaji wa Azimio la Mawaziri wa Kampala kuhusu Uhamiaji, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.

Chuyi alisema Tanzania inakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko ya mara kwa mara, ukame wa muda mrefu, na kuongezeka kwa viwango vya maji ya bahari. Matukio haya yamesababisha uharibifu wa miundombinu, kupungua kwa uzalishaji wa kilimo na kuwalazimisha maelfu ya wananchi kuhama makazi yao.

“Athari hizi si masuala ya kimazingira pekee bali pia ni changamoto za kibinadamu na maendeleo zinazogusa kiini cha jamii yetu,” alisema Chuyi.

Alisema kwa mwaka 2004 pekee, watu zaidi ya 278,000 waliathirika na mafuriko, huku ukame ukiathiri mfumo wa chakula na uchumi. Chuyi alisisitiza kuwa mpango wa kitaifa wa utekelezaji wa Azimio la Kampala (KDMECC) utasaidia kuunganisha juhudi za kitaifa na za kikanda.

Kuhusu mikakati na ushirikiano wa kikanda, Azimio la Mawaziri wa Kampala, lililoidhinishwa Julai 2002 na kusainiwa na Tanzania mnamo 2022, linahimiza ushirikiano wa kikanda katika kushughulikia changamoto za tabianchi na uhamiaji. Tanzania kwa sasa ipo kwenye hatua ya kuandaa Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kukamilika 2026.

Maurizio Busatti, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) nchini

Naye Maurizio Busatti, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) nchini, alisema kuwa uhamiaji umekuwa njia ya binadamu kukabiliana na majanga kwa karne nyingi. Alisisitiza kuwa ni muhimu kulinganisha changamoto na fursa za kikanda na utekelezaji katika ngazi ya kitaifa na za mitaa.

Aliongeza kuwa changamoto zinazoikabili Tanzania ni pamoja na kuongezeka kwa Viwango vya Maji ya Bahari, Maziwa na Mito hivyo kutishia makazi ya watu na shughuli za kiuchumi.

Changamoto nyingine ni mafuriko mara kwa mara ambayo yanaharibu miundombinu na mashamba, uUkame wa muda mrefu ambao unapunguza uzalishaji wa kilimo na kuathiri usalama wa chakula pamoja na uhamiaji wa ndani unaowafanya wananchi kuhama kutoka maeneo yenye changamoto kubwa za tabianchi kwenda mijini au maeneo salama zaidi na hivyo kuongeza shinikizo katika miji.

Upendo Mwakyusa, mwakilishi wa Asasi za Kiraia (CSOs)

Akizungumzia mchango wa asasi za kiraia, Upendo Mwakyusa, mwakilishi wa Asasi za Kiraia (CSOs), alisema mashirika ya kiraia nchini yamekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Asasi za kiraia zinahamasisha jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kushughulikia migogoro ya ardhi, utetezi wa sera na uhamasishaji wa jamii, kutoa elimu ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kusaidia wahanga wa majanga,” alsimea Mwakyusa

Alisisitiza kuwa wakulima na wafugaji kutoka maeneo kame, hasa Kanda ya Kati na Kaskazini, wamekuwa wakihamia maeneo yenye mvua za kutosha kama Kigoma na Katavi kutokana na ukame na uharibifu wa ardhi.

Pamoja na hilo, Mwakyusa ameseMashirika kama ForumCC, Haki Ardhi, Pastoral Women’s Council, na Cove Environmental Conservation yamekuwa yakilinda maslahi ya makundi yaliyo hatarini, hasa wanawake na wasichana.

Sikhulile Dhlamini, Mratibu wa Programu wa IOM Tanzania akiongea wakati wa majadiliano

Kwa upande wake Sikhulile Dhlamini, Mratibu wa Programu wa IOM Tanzania, aliipongeza mapendekezo yaliyotolewa kupitia mashauriano na wadau yaliyofanyika Augosti 5-6, 2025 jijini Dar es Salaam na akaahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali. Pia alisisitiza umuhimu wa kushirikisha vijana katika utekelezaji wa miradi ya mazingira na tabianchi.

Kimsingi, Tanzania inaelekea kwenye hatua muhimu ya utekelezaji wa Azimio la Kampala na mikakati ya kitaifa ya tabianchi. Ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, na jamii ni msingi wa kuhakikisha kuwa changamoto hizi zinazohusisha mazingira na uhamiaji zinatatuliwa kwa njia endelevu, ili kulinda ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

 


Post a Comment

0 Comments