| Picha ya pamoja ya viongozi na wawakilishi wa vikundi vitakavyounda Jukwaa la Kitaifa la Vikundi via Ujasiriamali kazi za Uchumi wa Buluu. |
Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN) limevikutanisha pamoja vikundi vya kitaifa zaidi ya 24 kutoka Zanzibar na Bara ambavyo vinajihusisha na ujasiriamali wa kazi za Uchumi wa Buluu kwa lengo la kuanzisha Jukwaa la Kitaifa la vikundi vya ujasiriamali kazi za Uchumi wa Buluu.
Kutano hilo la siku nne limeanza jana, Agosti 11,2025 jijini Dar es Salaam kwa kufunguliwa na mgeni rasmi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Christian Nzowa na linatarajiwa kufikia tamati Agosti 14,2025.
Wakati wa ufunguzi Nzowa alionesha kulitia shime jukwaa hilo na kutaka lianze akiamini litakuwa ni sauti ya vikundi kazi hivyo vilivyowekeza nguvu na akili zao kwenye uchumi wa buluu.
“Yapo mafanikio yaliyopatikana kutoka kwenye kufanikisha harakati za kuukuza uchumi wa buluu, lakini pia zipo changamoto, na changamoto kubwa ni ukosefu wa Jukwaa la uratibu kati ya wadau wa sekta za Uchumi wa Buluu nchini, juhudi za kuanzishwa kwa jukwaa hili kutatoa sauti ya vikundi vya jamii, litakalowaunganisha, kuwapa nafasi ya kushirikisha uzoefu, changamoto, mafanikio na kupata uongozi wa Pamoja kwa maendeleo yao,” alisema Nzowa.
Kwa upande wake Mwakilishi IUCN Tanzania, Charles Oluchina, aliwahakikishia wadau hao kuwa jukwaa hilo litakuwa na manufaa kwao katika kukuza uchumi wa vikundi vyao, kuwa na sauti ya pamoja na muhimu zaidi ni kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata sapoti ya moja kwa moja ya serikali.
Hata hivyo baadhi ya washiriki walionesha wasiwasi wao juu ya uwezekano wa jukwaa hilo kuwa endelevu kutokana na kuhusisha pande mbili za muungano ambazo changamoto zao katika masuala ya uchumi wa buluu ni tofauti.
Katika kuhakikisha wadau hao wanaondoa hofu juu ya jukwaa hilo na kuliona ni mkombozi kwao, Makala haya yatachambua faida, umuhimu na namna ya kuliendesha jukwaa hilo kwa tija.
| Mgeni rasmi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Christian Nzowa |
UMUHIMU WA JUKWAA
Wadau wa jukwaa hilo wanapaswa kujua kuwa Jukwaa la Kitaifa la Vikundi vya Ujasiriamali wa Kazi za Uchumi wa Bluu ni mpangilio wa pamoja unaolenga kuunganisha vikundi vya wajasiriamali, jamii za pwani, vyama vya wavuvi, wakulima wa mwani (seaweed), sekta ya utalii wa baharini, wazalishaji wa samaki, waandaaji wa teknolojia za bahari, taasisi za utafiti na serikali.
Lengo ni kukuza Uchumi wa Buluu kwa njia endelevu, kuongeza thamani ya rasilimali za bahari na kuboresha maisha ya wahusika wa ngazi ya msingi.
MADHUMUNI NA MALENGO YA JUKWAA
Wadau hawapaswi kuwa na hofu, badala yake wanapaswa kujua kuwa madhumuni ya jukwaa ni kukuza biashara na ukuaji wa uchumi unaotokana na rasilimali za bahari kwa vikundi vya ujasiriamali.
Kuelekeza sera, kutoa mafunzo, msaada wa kitekniki na kuongeza upatikanaji wa masoko,kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali baharini kupitia mbinu zinazoendana na mazingira.
Kuunganisha upande wa Tanzania Bara na Zanzibar katika mikakati ya pamoja ya Uchumi wa Buluu kwa kuheshimu muundo wa muungano.
UMUHIMU WA JUKWAA KWA VIKUNDI NA TAIFA
Jukwaa litawasaidia kuwafanikishia kwa urahisi upatikanaji wa maarifa na mafunzo ya kitaalamu, ufugaji wa samaki, uzalishaji wa mwani, maendeleo ya bidhaa za thamani.
Urahisi wa kupata masoko ya ndani na kimataifa kupitia muungano wa vikundi, ufahamu wa sheria, vibali na taratibu zamsaada wa kisheria.
Upatikanaji wa fedha za mradi, mikopo nafuu na usimamizi wa fedha (financial literacy), sambamba na uwezeshaji wa wanawake na vijana kupitia programu maalum.
Aidha jukwaa litaongeza mapato ya nje kupitia mauzo ya bidhaa za baharini zenye thamani ya juu, ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa jamii za pwani na usimamizi bora wa rasilimali baharini, kupunguza uharibifu na kuhifadhi biontaka.
Kuimarisha uwezo wa taasisi za utafiti na uvumbuzi (blue technologies), kuchangia malengo ya maendeleo endelevu na kuendeleza uchumi wa kitalii wa baharini.
FAIDA MAALUM ZA JUKWAA
Endapo wadau watafanikiwa kuliunda jukwaa hilo kwa ridhaa zao litawasaidia kujenga mtandao wa ushirikiano (networking) wa vikundi, sekta binafsi, NGOs na serikali.
Kupunguza kigezo cha rasilimali kupitia mipango ya pamoja ya usimamizi wa rasilimali, kuzalisha vugu vugu la biashara, kuongeza thamani kwa usindikaji, uchapishaji wa alama ya biashara (branding) na vyeti (standards) na kuleta uwekezaji wa mwelekeo kupitia ‘profiling’ ya miradi ya blue economy.
| Mwakilishi IUCN Tanzania, Charles Oluchina. |
USHAURI KWA WADAU WA JINSI YA KULIENDESHA
Ili kuepusha sintofahamu ni vema Jukwaa likawa na Sekretarieti ya kudumu (Permanent Secretariat) yenye wafanyakazi wa kitaalamu (coordination, mafunzo, biashara, M&E), Kamati ya Uendeshaji (Steering Committee) yenye uwakilishi wa Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wizara zinazohusika (Mifugo na Uvuvi, Mazingira, Viwanda, Biashara, Utalii), sekta binafsi, wawakilishi wa vikundi, watafiti na NGOs na bodi ya Ushauri (Advisory Board) ya kimataifa na kitaifa kwa sera na miongozo ya kiteknolojia.
SHERIA NA NYARAKA ZA MSINGI
Wadau wanapaswa kuhakikisha kunakuwa na Mkataba wa Mahusiano / Memorandum of Understanding (MoU) baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaoweka kanuni za ushirikiano, upangaji wa rasilimali, na mchakato wa maamuzi na wanaielewa vizuri na namna rahisi ni mikataba hiyo kuwekwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Ili kuhakikisha Jukwaa linakuwa endelevu ni vema kuwepo na Kanuni ndogo za uendeshaji (Bylaws) za jukwaa zinazoelezea majukumu, utoaji wa huduma, usimamizi wa fedha, uwakilishi, mchakato wa kufanya maamuzi na utawala wa maadili.
MFUMO WA UWAKILISHI
Ili kuepusha migogoro na kero za Muungano ndani ya Jukwaa ni salama ugawaji wa uwakilishi ukawa kwa msimamo wa 50:50bila kujali ukubwa wa eneo, aidha kuwe na uwakilishi wa kisera unaojumuisha Zanzibar (kwa kuzingatia mamlaka yake ya ndani) na Tanzania Bara.
Kila eneo linalogusa Uchumi wa Buluu (mwani, uvuvi, usindikaji, utalii wa baharini, vikingaji wa teknolojia) liwe na wawakilishi kwenye Kamati ya Uendeshaji.
UENDESHAJI WA KILA SIKU
Sekretarieti inapaswa kuwa na utayari wa kufanya mikutano ya kila mwaka, warsha za kitaalamu, na ripoti ya maendeleo na fedha kwa uwazi.
Kuwe na mfumo wa taarifa (M&E + MIS) kwa ukusanyaji wa data ya kisera, maonyesho ya miradi na uchunguzi wa athari za mazingira.
Kuandaliwe mfumo wa udhibiti wa ubora (standards) kwa bidhaa za baharini na huduma ili kufungua masoko makubwa.
FEDHA
Jukwaa linaweza kuanza kutafuta pesa kwa kukusanya ada za vikundi husika, ufadhili kutoka kwa wadau wa kitaifa na kimataifa, mikopo yenye mashariti nafuu pamoja na uwezeshwaji na serikali zote mbili.
Hata hivyo viongozi watakaopewa dhamana wasiogope kukaguliwa mara kwa mara.
MIKAKATI YA KUIMARISHA VIKUNDI NDANI YA JUKWAA
Njia pekee na salama ya kuimarisha Jukwaa ni kuanzisha mfululizo wa mafunzo ya vitendo (technical trainings) kwa uzalishaji, usindikaji, ufafanuzi wa soko, ‘packaging’, na usimamizi wa biashara.
Kuanzisha vikundi vya uzalishaji na vyama vya ushirika (cooperatives) vinavyoendana na soko, kutoa msaada wa kujenga alama (branding) za kibiashara za Kimkoa au Kinchi.
Kusaidia upatikanaji wa mikopo kupitia mfuko maalum wa jukwaa au kwa kushirikiana na benki za maendeleo, mipango maalum kwa wanawake na vijana (mentorship, seed grants).
KUKABILIANA NA CHANGAMOTO
Mamlaka na Sheria tofauti:
Ukweli ni kwamba Zanzibar ina serikali yake ya Mapinduzi yenye mamlaka katika masuala ya ndani na serikali ya Muungano una mamlaka kiasi tu, hii inaweza kuweka ugumu kidogo.
Hata hivyo ni vema kuwa na MoU rasmi na Mfumo wa kuratibu sheria unaoonyesha maeneo ya ushirikiano; kuna haja pia ya kupanga maamuzi kwa msingi wa masuala (masuala ya sera za kitaifa yachukuliwe kwa ushirikiano, masuala ya ndani ya Zanzibar yafuatwe kwa taratibu zao).
Usawa wa upatikanaji na uwakilishi:
Kuna utofauti wa eneo la kijiografia na kijamii, hata hivyo kunapaswa kuwa na mfumo wa uwakilishi wa kitaifa ambao utajumuisha uwakilishi wa mikoa, sehemu za pwani ndogo, na vipaumbele vya wasiojiweza na kusimamia mpango wa kuleta mafunzo kwenye eneo husika.
Utoaji wa Fedha na Uendelevu
Moja ya mambo yanayodhoofisha na kuua majukwa ya namna hii ni utegemezi wa fedha za mradi kutoka kwa wahisani zaidi bila kusaka vyanzo mbadala.
Ili kukabiliana na hili ni vema viongozi wakawa wepesi kutafuta vyanzo vingi vya mapato hasa katika maeneo ya (public-private partnerships, ada za usajili, huduma za ushauri kwa kampuni, uuzaji wa data/maendeleo ya soko) na kujikita katika kutambua jinsi ya kutengeneza miradi inayolipa (bankable projects).
Uendeshaji na Ushirikiano wa Taasisi
Kunaweza kuwa na changamoto ya uratibu kati ya Wizara, taasisi za utafiti na sekta binafsi, njia ya kukabiliana na hili ni kuwa na Kalenda ya pamoja ya shughuli, hoja za kitaasisi (institutional roadmap), na mshikamano kupitia mfumo wa taarifa za kawaida (portal ya jukwaa).
Mambo ya Mazingira na Uendelevu
Limekuwa na changamoto ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira, njia ya kukabiliana na hili ni kuanzisha vigezo vya matumizi endelevu, mfumo wa M&E wa mazingira, na kuunganisha maarifa ya jamii husika ‘local knowledge’ katika usimamizi.
Migogoro na Usuluhishi
Pamoja na mambo mengine suala la migogoro juu ya rasilimali, faida, au uwakilishi halitaepukika, njia ya kukabiliana na hali hii inapaswa kuwa imara kwa jukwaa kuwa na utaratibu wa utatuzi wa migogoro utakaosimamiwa na bodi ya uwakilishi na upatikanaji wa mwelekeo wa utetezi wa sera (policy advocacy) kwa msimamo wa pamoja.
Pamoja na mambo mengine jukwaa hili linapaswa kupokelewa kwa shangwe na wadau wa Uchumi wa Buluu na naamini wataalamu wamefanya upembuzi yakinifu na kuangalia namna sahihi za kuliendesha jukwaa hili hasa kwenye muundo wa uongozi na maeneo mengine muhimu ya kimaamuzi.
0 Comments