Ticker

7/recent/ticker-posts

CHANGAMOTO ZA UPATIKANAJI WA TAKWIMU KATIKA MASUALA YA UHAMAJI NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Washiriki wa mjadala ambao ni wadau wa mazingira



NA SIDI MGUMIA, DAR ES SALAAM

Takwimu sahihi, za kuaminika, na zinazopatikana kwa wakati ni msingi wa kupanga na kutekeleza mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazochanganya mazingira, mabadiliko ya tabianchi, na uhamaji wa watu. Bila takwimu bora, serikali na wadau wa maendeleo hukosa msingi thabiti wa kufanya maamuzi, hali inayoweza kudhoofisha utekelezaji wa sera na mipango ya kitaifa.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uhamaji na mabadiliko ya tabianchi wamebainisha kuwa changamoto za ukusanyaji, uhifadhi, na uchambuzi wa data bado ni kubwa tatizo ambalo si la Tanzania pekee, bali ni la kimataifa.

Wameonya kwamba hali hii inaweza kuhatarisha uwezo wa kupanga na kutekeleza sera zenye tija. Kauli hizo zilitolewa katika Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Utekelezaji wa Azimio la Mawaziri wa Kampala (KDMECC) uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Sabira Coelho, Mtaalamu wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi kutoka IOM Tanzania

Jyri Jantti, Afisa Utafiti na Ushirikiano wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) kwa Ukanda wa Mashariki, Pembe ya Afrika na Kusini mwa Afrika, amesema changamoto kubwa hutokea hasa pale matukio yanayoathiri uhamaji yanapoanza taratibu. Mfano ni ukame wa muda mrefu unaosababisha watu kuhama.

“Ni vigumu wakati mwingine kutambua kama mtu alihama kwa sababu ya ukosefu wa kipato baada ya misimu mitatu ya ukame, au alihama moja kwa moja kutokana na athari za tabianchi,” alisema Jantti. “Data mara nyingi haitakuwa kamilifu, lakini inapotuonyesha taswira pana ya hali, inaweza kutusaidia kupanga hatua stahiki.”

Jantti aliongeza kuwa Tanzania na nchi nyingine za kanda zimekuwa zikifanya juhudi kukusanya taarifa kuhusu uhamaji unaohusiana na tabianchi kupitia tafiti za kitaifa na miradi ya kikanda. Takwimu hizi husaidia kutambua makundi yaliyo hatarini zaidi, kama wanawake na watoto, ambao mara nyingi huathirika zaidi na majanga kama maporomoko ya ardhi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka takwimu hizo katika hifadhidata ya kitaifa, akitaja Somalia na nchi nyingine kama mifano ya mafanikio ambayo IOM iko tayari kushirikisha na Tanzania.

Washiriki wa mdahalo

Kuhusu mapungufu ya rasilimali na uhifadhi wa takwimu, Reuben Mbugi ambaye ni Afisa Mpango Msaidizi wa IOM Tanzania, alisema changamoto za takwimu ni za dunia nzima. Alitoa mfano wa kipindi cha janga la COVID-19 ambapo Tanzania ilitumia mfumo wa majaribio Zanzibar kufuatilia mienendo ya uhamaji, hatua iliyosaidia kutoa msaada kwa walioathirika. Hata hivyo, alisema mradi huo haukuendelezwa kutokana na changamoto za rasilimali. 

“Changamoto kubwa ni upungufu wa takwimu na kutokuwepo kwa uhifadhi rasmi wa taarifa. Ni muhimu tushirikiane kuhakikisha taarifa zilizopo zinaingia kwenye mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa majanga,” alisisitiza Mbugi.

Kwa upande wake, Sabira Coelho, Mtaalamu wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi kutoka IOM Tanzania, alisema changamoto zinazokumba mzunguko mzima wa usimamizi wa data zinajumuisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, usahihi wake, uhifadhi, na uchambuzi. Alieleza kuhusu matumizi ya ‘Displacement Tracking Matrix (DTM) ambao ni mfumo wa kufuatilia uhamaji na mahitaji ya watu waliopoteza makazi.

DTM hutumia mbinu nne kuu: Ufuatiliaji wa mtiririko wa watu katika vituo muhimu. Ufuatiliaji wa njia za uhamaji.  Tafiti za kina kuhusu mahitaji na sababu za kuhama na Usajili wa jamii zilizoathirika.

Coelho alisema IOM pia imeanza kutumia zana za kuchambua uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na afya, ili kuboresha utabiri na mipango ya kukabiliana na majanga.

Katika mjadala huo, hoja muhimu iliyojitokeza ni kuhusu wakimbizi. Kisheria, hawahesabiwi kama wahamiaji wa tabianchi, lakini mara nyingi migogoro inayowalazimisha kuondoka inahusiana na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha wanajumuishwa katika mipango ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, si kama wahanga pekee bali pia kama wadau wanaoweza kuchangia suluhu.

Kilichosisitizwa ni kwamba upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye viwango vya kimataifa ni msingi wa mipango madhubuti ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake katika uhamaji wa watu. Ushirikiano wa karibu kati ya serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, na jamii ni muhimu ili kuziba pengo la taarifa na kujenga mifumo imara ya usimamizi wa data.

Aidha, mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar Es Salaam kuanzia Agosti 5-6, 2025 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mazingira nchini umeweka msingi wa hatua za Tanzania kuelekea utekelezaji wa kitaifa wa Azimio la Kampala, kwa kuangazia vipaumbele, hatua za utekelezaji, na mchango wa wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za uhamaji unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

 


 

Post a Comment

0 Comments