Ticker

7/recent/ticker-posts

SIMBA HATARINI KUTOWEKA AFRIKA, ULINZI WA HARAKA UNAHITAJIKA


 
NA MWANDISHI WETU

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoadhimisha siku ya Simba duniani ndani ya wiki hii. Hatua hii inatajwa kuwa muhimu kwa sababu inachochea kasi ya kumlinda mnyama huyo wa porini ambae yuko kwenye tishio la kutoweka Afrika na duniani kwa ujumla.

 

Inakadiriwa kuwa Simba wanaelekea kutoweka kwenye zaidi ya nusu ya nchi za Afrika na sasa jitihada zinafanyika kurejesha asilimia 23 mpaka 33 ya baadhi ya spishi za mnyama huyo zilizo kwenye tishio na ili kulifanikisha hilo, kunahitajika ulinzi wa haraka ili kuwalinda hao wachache waliopo.

 

Katika Siku ya Simba Duniani iliyoadhimishwa Agosti 10,2025, imeripotiwa kuwa spishi hii maarufu zaidi barani Afrika imetoweka kabisa katika nchi 26 kati ya 48 za Afrika, huku idadi ya simba wa porini ikisalia katika asilimia 7 pekee ya eneo walilowahi kuishi kihistoria. 

 

Upotevu wa makazi, migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ujangili na mitego ya waya ni miongoni mwa visababisha vikuu vya janga hili. 

 

Tanzania ndio inatajwa kuwa nchi pekee yenye idadi kubwa zaidi ya Simba barani Afrika, na ina jukumu muhimu katika kuendeleza maisha ya mfalme huyo wa mbuga

 

Inaelezwa kuwa kulinda simba nchini Tanzania si kwa manufaa ya spishi hii pekee, bali pia kwa usawa wa ikolojia na urithi wa kitamaduni unaowakilisha thamani kubwa barani kote.

 

Kwa karne nyingi, simba wa Afrika wamekuwa ishara ya nguvu, ujasiri na uongozi, wakiwa na nafasi kubwa katika tamaduni, utambulisho na maisha ya kiroho ya Afrika. 

 

Taasisi ya Wild Africa inasisitiza kuwepo kwa udharura wa kulinda simba kupitia suluhu shirikishi zinazosaidia wanyama na jamii za wenyeji.

 

Kulingana na Takwimu za LionAid 2025 kuhusu Idadi ya Simba Afrika, idadi ya simba wa porini ipo katika kiwango cha hatari kubwa. 

 

Hata kama ni vigumu kuthibitisha idadi kamili, inakadiriwa kuwa ni simba 13,014 pekee ndio wamesalia Afrika Mashariki na Kusini, na simba 342 pekee ndio wamebaki katika nchi za Afrika Magharibi na Kati na haya ndio maeneo yenye aina tofauti za kijenetiki na yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kutoweka kwa Simba.

 

Takwimu nyingine kutoka Orodha ya Spishi Zilizoko Hatarini ya kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasili (IUCN) zinathibitisha kuwa idadi ya simba inaendelea kupungua. 

 

Hali ya urejeaji wa spishi hiyo imetajwa kuwa “imepungua kwa kiasi kikubwa” na kiwango cha urejeshaji wake unasomeka kati ya asilimia 23–33 pekee.


 Sababu kuu za hali hiyo ni kupotea kwa makazi ya asili. Zamani, simba walikuwa wanapatikana kuanzia Ulaya hadi ncha ya Kusini ya Afrika na kutoka Afrika Magharibi hadi India, lakini upanuzi wa makazi ya binadamu, kilimo, miundombinu na matumizi ya ardhi kumesababisha kupungua kwa eneo lao hadi asilimia 7 pekee. 

 

Uchafuzi wa makazi haya pia umepunguza wingi wa wanyama wa porini wanaowindwa na simba. Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa katika Conservation Science and Practice umebaini kuwa upungufu wa wanyama wa porini wanaowindwa ni sababu kubwa ya kupungua kwa idadi ya simba.

 

VITISHO VINGINE:

Migongano kati ya binadamu na wanyamapori: Simba huawa ili kulinda mifugo au kulipiza kisasi kwa tishio linalodhaniwa.

 

Ujangili: Simba huwindwa kwa ajili ya sehemu za miili yao ikiwemo mifupa, makucha, meno, mafuta na ngozi, zinazotumika katika tiba za jadi au kuuzwa kwenye masoko haramu.

 

Mitego ya waya: Mitego isiyochagua, inayokusudiwa kuwinda nyama pori, mara nyingi huwanasa, kuwajeruhi au kuwaua simba, na pia kuchangia upotevu wa wanyama wanaowindwa.

 

Simba ni muhimu sana kwa afya na usawa wa mifumo yote ya ikolojia. Wakiwa ni spishi muhimu (keystone species), ulinzi wao husaidia kudumisha utofauti wa viumbe haikuanzia mimea na miti hadi wanyama wanaowategemea. 

 


Vilevile, simba ni miongoni mwa wanyama wanaotafutwa zaidi na watalii wa safari. Utalii wa wanyamapori huchangia asilimia 8.5 ya Pato la Taifa Barani Afrika, huku karibu asilimia 80 ya wageni wa kimataifa wakisema wanyamapori ndiyo sababu kuu ya kutembelea bara hili.

 

Kwa kuongezeka kwa vitisho na hali duni ya urejeaji wa spishi, haijawahi kuwa muhimu zaidi kutekeleza mikakati madhubuti ya uhifadhi wa simba wa porini barani Afrika. 

 

Njia shirikishi inayoweka kipaumbele katika uhifadhi wa makazi, ushirikishwaji wa jamii, kuimarisha utekelezaji wa sheria dhidi ya uhalifu wa wanyamapori, na utalii endelevu inaweza kuleta mabadiliko chanya.

 

Wananchi pia wanaweza kuwa na mchango muhimukuanzia kuripoti uhalifu wa wanyamapori na kulinda makazi ya asili, hadi kutembelea hifadhi za taifa ambapo ada za kuingia zinaenda moja kwa moja kusaidia askari wanyamapori na miradi ya uhifadhi.

 

Muda unaisha kwa simba wa Afrika, na maisha yao yako mikononi mwetu. Katika Siku hii ya Simba Duniani, kasi ya kuongeza uelewa inahitajika, kuhakikisha simba wanaendelea kuishi porini, na kuhakikisha muungurumo wao unaendelea kusikika barani kote kwa vizazi vijavyo.

 

Taasisi ya Wild Africa inalenga kuwa taasisi yenye ushawishi mkubwa zaidi katika mawasiliano ya uhifadhi barani Afrika, ikihamasisha msaada wa umma na utashi wa kisiasa kulinda wanyamapori na maeneo ya asili ya Afrika milele. 

 

Wanaamini kuwa binadamu na wanyamapori wanaweza kuishi na kustawi pamoja, hivyo wanasambaza ujumbe wa uhifadhi kwa hadhira pana zaidi kuliko ilivyowahi kufanywa.

 

Kupitia kuibua sauti za viongozi wa maoni barani Afrika kutoka nyanja mbalimbali kupitia mtandao wa washirika wa vyombo vya habari na programu mbalimbali, wanalenga kukuza utalii wa ndani wa wanyamapori, miradi ya uhifadhi ya jamii, pamoja na kupitishwa na utekelezaji madhubuti wa sheria za uhifadhi.

 

Kupitia mawasiliano na msaada wa moja kwa moja, wanalenga kupunguza kwa kudumu uhalifu dhidi ya wanyamapori, mahitaji ya nyama pori haramu, migongano baina ya binadamu na wanyamapori, na upotevu wa makazi. 

 

Mtandao wetu unajumuisha zaidi ya vyombo 25 vya matangazo vya kitaifa na kimataifa, pamoja na redio, magazeti, mabango, PR na kampuni za mitandao ya kijamii, zinazofanya kazi nasi bila malipo kuongeza sauti zao na kukuza masuala ya uhifadhi na mazingira.

 

Tunashirikiana na mabalozi zaidi ya 199 kutoka muziki, michezo, filamu, televisheni, biashara, dini na serikali kutoka Nigeria, Zimbabwe, Afrika Kusini, Rwanda, Ghana, Namibia na Somaliland.

 

Post a Comment

0 Comments