Ticker

7/recent/ticker-posts

UCHUMIWA BULUU WAKOMBOA WANAWAKE PANGANI, IUCN KITOVU CHA FURAHA YA WANAWAKE NDANI YA JANGWA LA WACHAWI

 

Mwenyekiti wa kikundi cha BMU chenye makazi yake Pangani Magharibi, Sofia Waziri, akifanya mahojiano na Waandishi wa Habari za Mazingira néant ya Jangwa la Wachawi lililopo, Pangani mkoani Tanga.

NA JIMMY KIANGO

 

Ukilisikia jina la Jangwa la wachawi unaweza kupata mshtuko na ukipata nafasi ya kwenda lilipo kama huna ujasiri basi utakachokifanya ni kuishia usoni mwa jangwa hilo.


Ndio, ni jangwa haswaa lililotandawaa mdomoni mwa bahari ya hindi na mkiani mwa Ziwa Pangani.


Jangwa la wachawi lina maajabu yake, kama huna uzoefu na umekosa ujasiri unaweza kufika mahali ukaamua kusimama katikati ya tope ukisubiri wenyeji waje wakusaidie kwenda mbele au kurudi nyuma.

 

Eneo hilo halina ujuaji, kwa asie na uzoefu nalo, kama ni mgeni ukijitia ujuaji ni lazima utapotea na salama yako ni kuwasiliana na wenyeji ili wakufuate au wakuelekeze njia sahihi ya kurudi barabarani, kumbuka kuna zaidi ya njia 100 za kuingia na kutoka ndani ya Jangwa la Wachawi.

 

Pamoja na simulizi hilo gumu la Jangwa la Wachawi ambalo safari yake kubwa imetawaliwa na tope, ukweli ni kwamba eneo hilo limebeba furaha ya Wanawake 16 wanaoishi Pangani mjini, mkoani Tanga.

 

Furaha ya wamama hao imenogeshwa zaidi na uwepo wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN).

 

IUCN imewapelekea wanawake hao wanaounda kikundi cha BMU, wakisaidiana kwa karibu na wanaume tisa katika kufanya urejeshaji wa miti ya mikoko ambayo imekatwa kwenye eneo hilo.

 

Ukataji wa mikoko kwenye eneo hilo ndio umesababi kuwepo kwa Jangwa, ni jangwa haswaa.

 

Safari ndani ya Jangwa la Wachawi.


Ni mwendo wa zaidi ya dakika 30 kutoka barabara ndogo ya vumbi hadi kukifikia kitalu namba tatu cha mikoko ambacho kimeoteshwa pembezoni mwa jangwa hilo.

 

Wahusika wakuu ni wanawake 16 na wanaume tisa ambao wameamua kuwa watetezi wa mazingira ya Bahari, wao wanatunza mikoko na dhamira yao kuu ni kuhakikisha Uchumi wa Buluu unaotegemea Bahari, Mito na Maziwa unawanuafaisha wao na vizazi vyao.

 

Safari ni ngumu, tope zito limeipamba njia, kuanzia mwanzo hadi mwisho ni tope tupu, ni tope zito jeusi lililojuu ya mwamba mgumu.

 

Wanawake wako peku peku wanawaacha watoto wao majumbani kwenda Jangwa la Wachawi ambalo limetokana na shughuli za binadamu za utengenezaji wa chumvi. 

 

Inaelezwa eneo hilo lilijaa mikoko, lakini majahili wamekata mikoko yote katika eneo kubwa la zaidi ya hekta 10, eneo lote hilo ni tupu kabisa, halina hata kisiki cha mkoko.

 

Wamama hao wanasema ingawa hawapati fedha za kukidhi mahitaji yao ya kijamii wao wanaamini kukiwa na mikoko ya kutosha pembezoni mwa ufukwe ni wazi hakutakuwa na samaki wa kutosha,fukwe zitaharibika, joto litaongezeka na matumbawe yatapotea.

 

"Sisi tunafanya kwa lengo la kulinda mazingira, suala la kipato litakuja lenyewe pale mikoko itakapokuwa ya kutosha." Amesema Mwenyekiti wa kikundi cha BMU chenye makazi yake Pangani Magharibi, Sofia Waziri.

 


Anasema pamoja na ugumu wa mazingira yao ya eneo wanalofanya urejeshaji wa mikoko, lakini kazi yao wanaipenda na kamwe hawataiacha kwa sababu wanaamini ina tija kubwa sana kwao na inawapa furaha.

 

Sofia, anasema Jangwa la Wachawi ni eneo lao la furaha na ujio wa IUCN umewaongezea furaha zaidi kwa sababu awali walikuwa wanaifanya shughuli ya urejeshaji mikoko kienyeji,jambo ambalo lilikuwa halifanikiwi.

 

"Tulikuwa tunafanya kienyeji sana, hatukuwa tunajua lolote juu ya upandaji wa mfumo wa Mwiba wa Samaki ambao ni rafiki sana kwa eneo hili la jangwa kwa sababu ya mwamba uliopo, baada ya kupata elimu ya upandaji mikoko wa aina hii ya mwiba wa samaki, tumefanikiwa sana, miche ya mikoko sasa haifi," alisema.

 

Aliongeza kuwa ujio wa IUCN umeongeza furaha kwenye jangwa la Wachawi kwa sababu sasa angalau kuna mgao mdogo unapatikana kutoka kwenye kazi hiyo wanayoifanya.

Post a Comment

0 Comments