Ticker

7/recent/ticker-posts

ASKARI UHIFADHI WA KIJIJI WILAYA YA NAMTUMBO ‘WALIA NJAA’

 

VGS, Nasoro Matwika Askari wa Uhifadhi wa Kijiji cha Mtelawamwahi akielezea changamoto zinazowakabili kwa waandishi wa Habari za Mazingira (hawapo pichani)

 

NA JIMMY KIANGO-Aliyekuwa Namtumbo

 

Askari Uhifadhi wa Kijiji (VGS) waliopo katika vijiji nane vinavyokabiliwa na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kukosa posho, vifaa maalum vinavyostahili kutumika katika kurejesha Wanyama hasa tembo hifadhini, pamoja na usafiri.

 

Kimsingi askari hawa wapo kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Wildlife Conservation Act) ya mwaka 2009, kifungu cha 8 cha sheria hiyo kinaeleza wazi kuhusu uundaji wa askari wa uhifadhi wa Kijiji ambao watahusika katika kulinda rasilimali za wanyamapori kwenye maeneo ya vijiji, chini ya mwongozo wa serikali za mitaa na mamlaka za uhifadhi. 

 

Askari hawa wanapewa mamlaka maalum ya kuhakikisha usimamizi bora wa wanyamapori katika maeneo yao ya utawala.

 

Hata hivyo pamoja na kutambuliwa na sheria, bado askari hao hawapewi nguvu inayostahili ya kutekeleza majukumu yao jambo linalowafanya kushindwa kuwajibika ipasavyo kutokana na kukabiliwa na ukata.

 

Katika vijiji vya Likuyuseka, Kitanda, Mtelawamwahi na Ligunga ambavyo vilitembelewa na timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira waliokuwa chini ya mwamvuli wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ) na serikali ya Tanzania changamoto ya ukata iliibuliwa na VGS wengi waliopata nafasi ya kuzungumza.

 


VGS wengi waliiomba serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi kuona namna ya kuwapatia posho ya kila mwezi itakayowasaidia kukabiliana na ugumu wa Maisha na kuwafanya kuwa na utayari wa kushiriki kazi ya kuhangaika na wanyamapori kila wanapoingia kwenye mashamba au makazi ya watu.

 

Pia waliomba kuwasaidia vifaa vya  kisasa ili kuongeza nguvu ya kudhibiti wanyamapori wanaotoka hifadhini na kuingia kwenye maeneo ya watu.

 

Hoja yao ni kuwa kwa sasa wanafanya kazi hiyo kwa kujitolea huku wakiwa hawajui hatma za maisha yao kwani kuna nyakati wanalazimika kutumia muda mwingi kuhangaika na wanyamapori na kuacha shughuli zao za kujiingizia kipato.

 

Juma Kindamba, Mohamed Nihamba, Rashid Kahunde na Hassan Mkonde ni miongoni mwa Askari Uhifadhi wa Kijiji cha Likuyuseka waliotoa kilio chao kwa waandishi wa Habari wakisema kuwa pamoja na kupata mafunzo ya kukabiliana na wanyamapori, lakini wanakosa vitendea kazi pamoja na motisha.

 

Nihamba alisema pamoja na kuhitaji posho, pia wanahitaji mabomu baridi yenye uwezo wa kutoa kishindo kinachokwenda mbali, mabuti, sare, usafiri na mahema ambayo watayatumia pindi wanapoamua kuweka kambi msituni.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitanda ambao waliomba VGS wa kijiji chao wawezeshwe.

 
“Vifaa tunavyotumia sasa kukabiliana na wanyamapori wanaoingia kwenye makazi ya watu havina uwezo wa kudhibiti makundi ya wanyamapori hasa tembo.

“Mabomu tuliyonayo hayana uwezo wa kishindo chake kwenda mbali hali inayowalazimu kuyatumia kwa kuwasogelea tembo hatua inayohatarisha maisha yao.

“Tembo nso wanajihami, akikuona unazidi kumsogelea lazima atakukimbiza ili akudhuru.”

 

Hata hivyo VGS hao wameishukuru GIZ kwa kugharamikia mafunzo yao ya  namna ya kukabiliana na wanyamapori na uwepo wao angalau una tija kwani wameweza kuwapa mafunzo ya namna ya kutengeneza vimiminika vyenye harufu ambavyo vinasaidia kufukuza tembo.

 

VGS, Nasoro Matwika, Mussa Nchimbi, Erick Mgala na Joby Mhagama waa Kijiji cha Mtelawamwahi wanasema uhaba wa posho na vyombo vya usafiri hasa pikipiki unasababisha kuifanya kazi yao kuwa ngumu.

 

Matwika anasema wanachelewa kwenda kudhibiti makundi ya tembo pale wanapopata taarifa kwa sababu wanalazimika kutembea kwa miguu kwa umbali mrefu hatua inayowafanya kupishana na matukio.

 

“Maeneo ya mashamba ambako tembo huingia huko ni mbali kutoka kijijini mpaka huko, hivyo inapotokea tembo wameonekana mahali na kupewa taarifa, inatuchukua muda mrefu kufika kwa sababu hatuna usafiri wa uhakika.

 

“Lakini pia kama tunakuwa kwenye shughuli za kujiingizia kipato napo panakuwa na ugumu kwa sababu huwezi kuacha hela na kukimbilia kukimbiza tembo huku ukijua hakuna utakachokipata,”alisema Mtwika.

 

Abasi Sowo na Amani Ponera ambao ni miongoni mwa askari wa hifadhi wa Kijiji cha Kitanda walisema wanapokuwa lindoni wanalazimika kulala kwenye maeneo ambayo si salama na kuhatarisha maisha yao kwa kukosa mahema.

 

“Kukosa vifaa na fedha kunatulazimisha kuiona kazi ni kama haina maana, haitufanyi tupate morali Zaidi wa kuendelea nayo ingawa tumeisomea, hatuna hela, hatuna chakula na hatuna vifaa.”

 

Sowo anasema ziko nyakati wanalazimika kuchangishana pesa ili kutafuta usafiri au kujinunulia chakula,

 

Ombi lao kwa serikali VGS wengi wameiomba serikali iwakumbuke na kuwaweka katika mipango ya kuwapa posho za kila mwezi, ili ziwasaidie kutunza familia zao na hata kumudu kujihudumia chakula wanapokuwa kwenye kutekeleza majukumu yao.

 

Pamoja na mambo mengine wengi wa askari hao waliishukuru GIZ kwa kuwapa mafunzo na mbinu za kisasa za  kudhibiti wanyamapori ambayo yanawasaidia kukabiliana na wanyamapori na kwamba msaada wao huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

 

Mtendaji wa Kata ya Likuyuseka, Neema Mwakatimbo,

Akizungumzia changamoto ya VGS wa kijiji cha Likuyuseka, Mtendaji wa Kata ya Likuyuseka, Neema Mwakatimbo, alisema wanazijua na harakati za kuhakikisha wanawasaidia zinaendelea na wanakaribisha wadau kusaidiana nao kama walivyofanya GIZ.


Mwakatimbo alisema GIZ imekuwa ikisaidia kulipa posho na hata kusaidia chakula, lakini bado kuna uhitaji zaidi wa kuwawezesha VGS hao ili kuipenda kazi yao.


Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Haruna Mang’uli aliwaambia Waandishi wa Habari za Mazingira kuwa wilaya hiyo imekuwa na mikakati mbalimbali ya kupunguza migongano hiyo kwa kushirikiana na wadau wakiwemo GIZ na miongoni mwake ni kuwatumia VGS.

 

“Ujio wa GIZ umekuwa na tija kubwa, hali sasa si mbaya kama ilivyokuwa huko nyuma, mambo yalikuwa ni magumu. Mwendelezo wa kuwajengea uelewa wananchi wetu utasaidia kuondokana na migongano hiyo, ni kweli kuna watu wanafanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi na sharia zinafuatwa na napenda kusisitiza kuwa sharia zitaendelea kuchukuliwa kwa wanaozivunja., Zaidi tunawaomba wadau waendelee kutusaidia.” 

 

Kuhusu changamoto ya vifaa na posho kwa VGS, Mang’uli alitoa wito kwa wadau Zaidi kujitokeza ili kusaidiana na serikali ya wilaya kuwawezesha askari hao wa uhifadhi wa Kijiji.

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Haruna Mang’uli 

Kwa upande wake Mratibu Mshauri wa GIZ, Wilaya ya Namtumbo, Chrian Zimbaiya, alisema wanashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutatua changamoto za askari hao ikiwamo upungufu wa sare za vitendea kazi hasa sare, Mabuti, mahema, usafiri, tochi na mahema.

“Ni kweli kuna upungufu wa sare za kazi kwa VGS, lakini naomba ieleweke kuwa hilo si jukumu letu, sisi tuna bajeti kidogo, yapo maeneo tunasaidia, lakini mengine ni ya serikali na wadau wengine, hata hivyo kwa sasa tupo katika mchakato wa kuongeza sare 11 na mahema matatu kwa maaskari wa wilaya na baadaye tutafika na huko kwingine,” alisema.

 

Zimbaiya aliwataka wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi kutumia mbinu mbalimbali walizofundishwa katika kuwafukuza wanyamapori wanaoingia kwenye maeneo yao hasa tembo.

 

Mratibu Mshauri wa GIZ Wilaya ya Namtumbo, Chrian Zimbaiya,

Askari uhifadhi wa kijiji wanatambulika kisheria ni askari maalum ambao wanateuliwa na mamlaka za vijiji kwa lengo la kusaidia kulinda maliasili, kama vile misitu na wanyamapori, ndani ya maeneo yao. 

 

Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori  ya mwaka 2009, pamoja na sheria na sera nyingine zinazohusiana na maliasili, zinatambua jukumu la askari hawa katika kulinda rasilimali za vijiji na kusaidia juhudi za uhifadhi.

 

Askari hawa wanaweza kushirikiana na mamlaka za serikali, kama vile Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) au Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), katika kusimamia maeneo ya uhifadhi. 

 

Kimsingi wanatoa mchango mkubwa katika kulinda maliasili kwa kupambana na ujangili, uharibifu wa mazingira, na shughuli zingine haramu ndani ya hifadhi.

 

Post a Comment

0 Comments