Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA YAKARIBISHA KAMPUNI ZA UINGEREZA KUWEKEZA KWENYE NISHATI JADIDIFU


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amezikaribisha Kampuni kutoka nchini Uingereza kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati hasa eneo la Nishati Jadidifu ili kutimiza lengo la Serikali la kuingiza umeme mwingi kwenye gridi ya Taifa unaotokana na Nishati Jadidifu.

Amesema hayo jijini Dodoma wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania ukiongozwa na Bw. Euan Davidson, Kiongozi wa Timu ya Ustawi Endelevu ambapo kikao hicho kililenga kujadili maeneo ya ushirikiano.

 

Mhandisi Mramba ameueleza ujumbe huo kuhusu mahitaji ya uwekezaji kwenye miradi ya nishati jadidifu ikiwemo umeme jua kwa ajili ya matumizi ya majumbani hasa kwenye sehemu zilizo nje ya gridi pamoja na uwekezaji mkubwa wa umeme Jua utakaoingia katika  gridi ya Taifa.

 

Amesema kuwa, tayari uwekezaji kwenye nishati ya umeme jua umeanza kupitia mradi wa Kishapu-Shinyanga (150MW) na uwekezaji mwingine utafanyika kwenye maeneo mengine nchini ikiwemo Mkoa wa Dodoma (200 MW).

 

Kuhusu uwekezaji katika umeme unaotokana na upepo amesema kuwa, kuna maeneo tayari yameshatambuliwa ambayo yanaweza kuzalisha umeme huo ikiwemo Dodoma, Singida, Mbeya, Makambako, Same, Mara na Arusha anbayo yanahitaji ushirikiano katika uwekezaji.

 

“ Tanzania tumebarikiwa  vyanzo vingi vya Nishati Jadidifu kwani pia tuna hazina kubwa ya Jotoardhi katika maeneo takriban 52 ambayo yakiendelezwa yatazalisha umeme kuliko nchi ya Kenya ambayo sasa inazalisha umeme wa Jotoardhi takriban megawati 1000.” Ameeleza Mramba

 

Aidha, ameeleza nia ya Tanzania kutumia nishati safi zaidi kuzalisha umeme ikiwemo nishati ya blue hydrogen inayotokana  na rasilimali ya Gesi Asilia, bila kusahau matumizi ya nishati ya bayogesi hasa katika maeneo ya vijijini yenye mifugo mingi.

 

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Mhandisi Mramba ameueleza ujumbe huo juhudi zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia iliyo safi kupikia ifikapo mwaka 2034, ameeleza  kuwa hii yote ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ambao utekelezaji wake unashirikisha Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo Sekta binafsi.

 

Kuhusu usambazaji umeme mijini na vijijini, Mhandisi Mramba amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye eneo hilo na kwa usambazaji umeme vijijini asilimia 99 ya vijiji vimefikiwa na umeme na kwamba ifikapo mwezi Disemba mwaka huu kila Kijiji kitakuwa kimefikiwa na huduma ya umeme.

 

Kwa upande wake, Bw. Euan Davidson, Kiongozi wa Timu ya Ustawi Endelevu kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, ameshukuru kwa kupata taarifa za kina kutoka Wizara ya Nishati ambazo zitatumika na nchi hiyo kuangalia maeneo wanayoweza kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati.

Ameeleza kuwa mazungumzo ya viongozi hao yamekuwa na umuhimu kwani Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele na Uingereza katika masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji. Mazungumzo ya viongozi hao pia yamegusia Kongamano la Kimataifa la Nishati litakalofanyika Tanzania mwaka 2025 ambapo Uingereza imeonesha nia ya kushiriki.

 

 

Post a Comment

0 Comments