Ticker

7/recent/ticker-posts

CHUMVI, UNGA WA SEMBE VYAWATOA TEMBO HIFADHINI NAMTUMBO

 

Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Issa Hassan Ndomondo 

 NA JIMMY KIANGO-NAMTUMBO

Amini usiamini ila ndivyo ilivyo. Pamoja na sababu nyengine nyingi, lakini chumvi na unga wa sembe navyo vinatajwa kuwa sehemu kubwa ya sababu za kuwatoa tembo hifadhini na kuingia kwenye maeneo ya binadamu.

 

Imeelezwa kuwa tembo wakikosa vitu vyenye ladha ya chumvi hifadhini hufunga safari kwa umbali mrefu kwa ili kuitafuta na hapo ndipo huingia kwenye maeneo ya binadamu na kula mazao na wakati mwengine  kuvunja vyoo na majiko.

 

Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Issa Hassan Ndomondo ndie amewaambia hayo Waandishi wa Habari za Mazingira waliosafirishwa na Chama cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migogoro baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ) na serikali ya Tanzania kwenda Namtumbo mkoani Ruvuma kuwaongezea uelewa wananchi.

 

Ndomondo, anasema tembo anapenda vitu vyenye ladha ya chumvi, anapoikosa hifadhini huhakikisha anaitafuta kwa namna yeyote ile na mahali popote pale.

 

“Unajua tembo ana uwezo mkubwa wa kunusa harufu kwa umbali mrefu, hali hiyo inamfanya kufika popote penye kitu anachokitaka.”

Anasema tembo anapoingia kwenye makazi ya watu mara nyingi huvunja vyoo au majiko  kwa sababu ya kutafuta ladha ya chumvi.

 

“Wanavunja vyoo kwa sababu ya kwenda kuramba udongo uliojaa ‘mikojo’, si unajua ‘mikojo’ ina ladha ya chumvi chumvi, na kwenye majiko wanatafuta chumvi au kuramba majivu ambayo yana ladha ya chumvi.

 

“Kwenye nyumba nako wanavunja kwa lengo la kutafuta chumvi, lakini pia tembo wanakula mahindi yaliyovunwa na kuhifadhiwa ndani pamoja na unga wa sembe, wanavunja nyumba au majiko, wakikutana na unga wa mahindi wanakula,”amesema Ndomondo.

 


Kwa upande wa mashambani, Ndomondo amesema zipo dawa zinazotumika kunyunyizia mimea, dawa hizo zina ladha ya chumvi chumvi ambayo ndio raha ya tembo.

 

AFRINEWSSWAHILI iliongea na Jenester Nchimbi mwananchi mkazi wa Kijiji cha Likuyusekamaganga juu ya suala la tembo kufuata chumvi kwenye makazi yao, ambapo alisema hakuwa akijua hilo, lakini alishawahi kushuhudia tembo wakivunja choo na kukanyagakanyaga eneo hilo.

“Sijui kwakweli kama tembo nao wanapenda chumvi, ila nilishwahi kushuhudia wakivunja choo na kukanyagakanyaga udogo kisha walikuwa ni kama wanafurahia jambo, sasa kama ndio walikuwa wanafurahia kuramba udongo wenye ‘mikojo’ sijui kwakweli,”amesema.


KUMLISHA TEMBO KINYESI CHAKE

Katika udhibiti wa tembo kuingia kwenye mashamba ya binadamu ili kupunguza migongano, Ndomondo alitoa ushauri kwa wananchi kuhakikisha wanatumia mbinu na njia mbalimbali wanazofundishwa na wataalamu ikiwemo ya kutumia vimiminika vya harufu inayotolewa na GIZ.

 

Aidha amesema katika tafiti zake mbalimbali za kutafuta namna ya kukabiliana na tembo wanaoingia kwenye maeneo ya binadamu, amegundua njia ya kumlisha tembo kinyesi chake inaweza kusaidia kuwafukuza.

 

Anasema njia ya kuwalisha tembo kinyesi chao ingawa ina ugumu hasa katika kupata malighafi, lakini amejaribu kuitumia na imeleta tija.

 

“Unachokifanya ni kukusanya kinyesi cha tembo na kukikoroga mpaka kilainike, kisha unakimwagia kwenye mimea au mazao, hapo tembo hawezi kugusa. 

  

“Kitu nilichokigundua, hakuna mnyama anaeweza kula kinyesi chake, si ngombe, mbuzi, kuku wala kondoo ambae anaweza kula kinyesi chake na hivyo ndivyo ilivyo kwa tembo, mnyama akila kinyesi chake anadhurika,”alisema.

 

Akijibu swali la ni wapi kinyesi cha tembo kinaweza kupatikana kwa wingi na kwa urahisi hadi kutengenezwa dawa ya kuwafukuza, alisema si jambo rahisi, lakini kwa maeneo mengi ya vijiji vya Namtumbo tembo wanapatikana na wanamwaga vinyesi.

 

Juu ya kufanyia maboresho utafiti wake huo ili kutoa nafasi kwa wataalamu kutengeza mfano wa kinyesi cha tembo maabara, Ndomondo alisema hiyo inaweza isilete tija maana kitakachotumika hakitakuwa kinyesi chake bali ni mfano wa kinyesi cha tembo na mnyama huyo anaakili za kujua kuwa hiki ni kinyesi chake na hiki si chake.

 

KAULI ZA WATAALAMU JUU YA TEMBO NA CHUMVI

Mtafiti wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ambae hakutaka jina lake liandikwe, amesema ni kweli tembo wanapenda chumvi na inawezekana uhitaji wa chumvi ukawatoa nje ya hifadhi.

 

“Tembo kama Wanyama wengine wengi, wanahitaji madini ya sodium (chumvi) kwa ajili ya kazi za mwili kama vile udhibiti wa maji mwilini, shughuli za neva na usawa wa elektroni.

 

“Katika mazingira ya asili tembo mara nyingi wanatafuta vyanzo vya chumvi kama vile maji ya chumvi au madini yaliyopo kwenye udongo. Wanaweza hata kuchimba udongo kwa kutumia mikonga yao ili kupata chumvi kwa sababu ni sehemu muhimu ya mlo wao.”

Mtaalamu wa Wanyamapori, Dkt. Elikana Kalumanga

Kwa upande wake mtaalamu wa Wanyamapori aliyebobea kwenye tembo, Dkt. Elikana Kalumanga, aliiambia AFRINEWSSWAHILI kuwa ni kweli tembo wanahitaji chumvi kwani utengenezaji wa mifupa na meno ya kiumbe yeyote unahitaji madini joto (mineral contents) ambayo ni Sodium, Calcium, Iron na madini mengine muhimu.

 

“Mnyama yeyote akiwa na mimba, uhitaji wa madini joto unaongezeka. Ndiyo maana hata binadamu wa kike wanahitaji udongo ili kupata madini joto wakiwa wajawazito.

‘Sio kila udongo una madini joto yanayohitajika mwilini. Kuna sehemu maalumu - Salt lick sites au Geophagic sites. Utafiti niliofanya kwenye hifadhi ya Ugalla niligundua kuwa tembo wanakula udongo kwenye vichuguu pekee yake. 

 

“Udongo wa vichuguu ulikuwa na madini joto mengi mara 20 kuliko udongo wa kawaida na kwenye mimea. Sio kila kichuguu pia kina udongo wenye madini joto mengi. Inategemea na aina ya mchwa uliotengeneza hicho kichuguu. Kwa kifupi maeneo yenye madini joto kwa maana ya chumvi wanayohitaji wanyama sio mengi. 

 

“Pia, sio lazima haya maeneo yawe hifadhini. Maeneo ya hifadhi yanaamuliwa na binadamu na mipaka yake inaweza kuacha vitu muhimu wanavyohitaji wanyama nje ya mipaka ya hifadhi,”amesema Dkt. Kalumanga.

 

Timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira waliofanya ziara wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Haruna Mang'uli (wa nne kutoka kulia) na Mkurugenzi wa JET, John Chikomo (wa nne kutoka kushoto).

Post a Comment

0 Comments