Ticker

7/recent/ticker-posts

WANANCHI WAIOMBA SERIKALI KUWAADHIBU WANAOLIMA HIFADHINI

  

Timu ya Waandishi wa Habari za mazingira walio chini ya mwamvuli wa JET, wakifanya mahojiano na viongozi wa Kijiji cha Ligunga.

 NA JIMMY KIANGO-NAMTUMBO

 

Shughuli za kibinadamu katika maeneo mengi nchini hasa yale yenye hifadhi na kutosimamiwa kwa sheria kikamilifu kumetajwa kuwa kinara wa chanzo cha Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Namtumbo.

 

Kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Mwaka 2009 (Wildlife Conservation Act, 2009) inatoa mwongozo wa jinsi wanyamapori, ikiwa ni pamoja na tembo, wanavyopaswa kuhifadhiwa na kulindwa, pamoja na kuelekeza kiwango cha umbali wa mita 500 nje ya hifadhi ambao unaweza kutumika kwa shughuli za kilimo na kuelekeza adhabu zinazopaswa kutolewa kwa watakaoivunja sheria hiyo. 

 

Pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, ukiukwaji umeendelea kuwepo na kusababisha migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori. Hali hiyo imekisukuma Chama Cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongoao Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ) na serikali ya Tanzania kushiriki katika kuwapa elimu wananchi juu ya kupunguza migongano hiyo.

 

Septemba 16,2024, JET ilifanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma kwa lengo la kuangalia namna GIZ ilivyofanikisha kupunguza migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori katika vijiji nane vilivyomo ndani ya wilaya ya Namtumbo ambavyo ni Mtelawamwahi, Ligunga, Kilimasela, Mtonya, Likuyu, Likuyu Mandela, Nambecha na Kitanda hali imekuwa ikiimarika siku hadi siku.

 

Imeelezwa kuwa matukio ya wanyamapori hasa tembo kuingia kwenye makazi na mashamba ya watu yamekuwa yakipingua, lakini pia wananchi wameanza kuelewa umuhimu wa kufanya shughuli zao mbali na hifadhi. 

 

Hata hivyo bado wapo watu ambao pamoja na kupewa elimu, lakini wamekuwa ni wakaidi na kwa makusudi wamewauzia Wasukuma (Wafugaji) mashamba yao ya asili ambayo yako mbali na hifadhi na kuamua kwenda kuvamia hifadhi.

 

Hayo yamesemwa na Bi. Angelina Joseph Nchimbi ambae ni mkazi wa Kijiji cha Lugunga kilichopo Kata ya Lusewe wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.  Anasema ni kweli amekuwa akisikia tembo wameingia kwenye mashamba ama makazi ya watu, lakini hajawahi kushuhudia matukio hayo kwenye Kijiji chao.

 

Bi. Angelina Joseph Nchimbi (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na mwandishi wa Makala haya, Jimmy Kiango (kushoto) 

Amesema yeye ni mzaliwa wa Kijiji hicho na tangu ameanza kujielewa na hadi sasa ambapo amefikisha umri wa miaka 64 hajawahi kuona tembo wakivamia kwenye mashamba yao, kwa sababu mashamba na makazi yao yako mbali na hifadhi.

 

“Mimi nimezaliwa na kukua hapa Ligunga na hata uzee wangu umenikutia hapahapa, sijawahi kuona tembo wakivamia mashamba au makazi yetu, na hii ni kwa sababu sisi tunafanya shughuli zetu mbali na hifadhi.

 

“Wanaovamiwa na tembo ni wale waliowafuata, wameuza mashamba yao ya asili kwa Wasukuma na wao kukimbilia msituni huko kuvamia maeneo ya hifadhi, watu hawa wanapaswa kuadhibiwa kwa sababu wao ndio wachokozi.

 

“Huwezi kuacha kulima hapa Kijiji ambako kuna maeneo mengi makubwa, ukakimbilia Mtungo ambako ni karibu kabisa na hifadhi, huu ni uchokozi wa makusudi kwa wanyamapori.”alisema Bi. Angelina.

 

Kwa upande wake Bi. Anastazia Jimson Mapunda ambae ni mkazi wa Ligunga, amesema yeye anafanya shughuli zake za kilimo katika maeneo yao ya asili, hajauza maeneo yake kwa Wasukuma (wafugaji) kama walivyofanya wengine.

 

“Mwanangu nikwambia ukweli, hawa wanaolalamika kuvamiwa kwenye mashamba au makazi yao, wengi wameyafuata maeneo ya hifadhi, kwa tamaa zao wameuza maeneo yao ya asili na kwenda kuvamia hifadhini na hao ndio wanakutana na tembo kwa sababu nao ni viumbe na vinatafuta chakula kwenye maeneo yao, unajua tembo wana akili sana, sasa ukiwafuata ni lazima wakuoneshe kuwa umewachokoza,”amesema Bi. Mapunda.

 

AFRINEWSSWAHILI iliongea na Suna Kassim ambae ni mmoja wa watu ambao wamekutana na kadhia ya tembo kuvamia shamba lake, ambae amesema si kama wao ndio wamewafuata tembo, bali tembo ndio wanawafuata wao.

 

“Sio kweli kuwa mashamba yetu yamevamiwa kwa sababu ya kulima hifadhini ama karibu na hifadhi, wengi wa tuliokumbwa na tatizo la tembo kuvamia mashamba yetu tuko mbali kidogo na hifadhi.”

 

Kuhusu madai ya wengi wa wanaovamiwa ni wale waliouza mashamba yao ya asili kwa wafugaji na kuvamia maeneo ya hifadhi au yaliyokaribu na hifadhi, Kassim alisema ni keli wapo waliouza, lakini si wote walioathirika walikuwa na mashamba ya asili kijijini hapo.

 

Kilimanjaro Magute (Mfugaji)

WAFUGAJI: NI KWELI TUNAUZIWA MAENEO

Kilimanjaro Magute ni mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Ligunga ambae ni wa jamii ya Wasukuma ambao wengi ni wafugaji. Kwa kauli yake ameiambia AFRINEWS SWAHILI kuwa ni kweli wanauziwa maeneo na wenyeji kwa ajili ya kufanya shughuli zao.

 

“Ndugu mwandishi sisi tunapokutana na fursa hatuwezi kuziacha, kama wenyeji wanatuuzia maeneo sisi kosa letu liko wapi, ni kweli tunanunua na kufanya uwekezaji kwa kulima mpunga na hata kufuga, sasa kama wanakwenda kuvamia maeneo ya hifadhi, hilo sisi hatujui,”alisema Magute.

 

KAULI YA MWENYEKITI WA KIJIJI

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ligunga, Paulo Tawale amesema migongano baina ya Binadamu na Wanyapori ipo na wanajitahidi kukabiliana nayo kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu wananchi na kuweka vizuizi vya kufukuza tembo wanavyofundishwa na wataalamu mbalimbali wakiwemo GIZ.

 

Tawale, alikiri kuwepo kwa wanakijiji waliouza maeneo yao na kutafuta maeneo mapya nje ya eneo la Kijiji na kwamba wanachokifanya ni kuwapa elimu ili kuepukana na madhara wanayoweza kuyapata.

 

“GIZ imetusaidia sana kupunguza migongano hii, ambayo inahusisha pande mbili, elimu tuliyopewa pamoja na kuwepo kwa askari wa uhifadhi wa Kijiji (VGS) kumesaidia kuepusha madhara ingawa changamoto bado zipo.”  

 

KAULI YA SERIKALI YA WILAYA

Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Issa Hassan Ndomondo


Akizungumzia namna GIZ ilivyosaidia kupunguza migongano hiyo, Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Issa Hassan Ndomondo, alisema ujio wa mradi wa kupunguza migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori umesaidia kuongeza uelewa kwa wananchi hali iliyosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa matukio hayo.

 

“GIZ wamesaidia sana kufanikisha mpango wa kupunguza migongano, kwa sababu kabla ya ujio wao hali ilikuwa mbaya, lakini sasa kuna afadhali ambapo kulikuwa na kesi 46 mwaka 2023, lakini hadi kufikia  Agosti mwaka huu kumeripotiwa kesi 15.” 

 

Kwa upande wake Afisa Misitu wa Wilaya hiyo, Gravas Mwalyombo amesema wamekuwa wakishughulika na watu wanaovamavia maeneo ya misitu ya hifadhi, ingawa kwa wilaya ya Namtumbo matukio si mengi. Mwalyombo amesema kuwa ujio wa GIZ umesaidia kuwapa vitendea kazi, hatua iliyoboresha utendaji wao.

 

Nae Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Haruna Mang'uli aliwaambia Waandhishi wa Habari za Mazingira kuwa wilaya hiyo imekuwa na mikakati mbalimbali ya kupunguza migongano hiyo kwa kushirikiana na wadau wakiwemo GIZ.

 

“Ujio wa GIZ umekuwa na tija kubwa, hali sasa si mbaya kama ilivyokuwa huko nyuma, mambo yalikuwa ni magumu. Mwendelezo wa kuwajengea uelewa wananchi wetu utasaidia kuondokana na migongano hiyo, ni kweli kuna watu wanafanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi na sharia zinafuatwa na napenda kusisitiza kuwa sharia zitaendelea kuchukuliwa kwa wanaozivunja., Zaidi tunawaomba wadau waendelee kutusaidia.” 

 

Afisa Misitu wa Wilaya hiyo, Gravas Mwalyombo 

SHERIA 

Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Mwaka 2009 (Wildlife Conservation Act, 2009) inatoa mwongozo wa jinsi wanyamapori, ikiwa ni pamoja na tembo, wanavyopaswa kuhifadhiwa na kulindwa. 

 

Sheria hii inazuia uwindaji haramu na ujangili, inazuia uwindaji wa tembo bila kibali, na inatoa adhabu kali kwa yeyote anayekamatwa akihusika katika uwindaji haramu au biashara ya pembe za ndovu.

 

Inazuia biashara haramu ya wanyamapori, ambapo inapiga marufuku biashara ya sehemu yoyote ya mwili wa tembo, kama pembe za ndovu, na inaratibu usafirishaji wa wanyamapori nje ya nchi.

 

Aidha sheria hiyo inatambua na kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanyamapori, kama vile mbuga za kitaifa na hifadhi za misitu, ambako tembo wanaweza kuishi kwa usalama bila usumbufu wa shughuli za kibinadamu.

 

Ikumbukwe kuwa Tanzania pia ni sehemu ya mikataba ya kimataifa kama vile CITES (Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora), ambayo inazuia na kudhibiti biashara ya kimataifa ya pembe za ndovu ili kulinda tembo kutokana na ujangili na biashara haramu.

 

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Haruna Mang'uli 

Katika kuhakikisha wanyamapori wanalindwa na kuhifadhiwa sheria imewataka wakulima kufanya shughuli zao umbali wa angalau mita 500 nje ya mipaka ya hifadhi na anaekaidi basi anakabiliwa na adhabu mbalimbali kwa mujibu wa sheria za uhifadhi na mazingira. 

 

Sheria ya Uhifadhi wa Mazingira na Sheria ya Misitu zinaelekeza kuwa shughuli za kilimo ndani ya maeneo ya hifadhi ni kosa la jinai. Adhabu zinazoweza kutolewa ni pamoja na Faini, Mkulima anaweza kutozwa faini kulingana na ukubwa wa madhara aliyosababisha katika hifadhi.


Mkulima anaweza kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu gerezani kwa mtu anayepatikana na hatia ya kufanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi na kutaifisha mali vikiwemo vifaa vya kilimo au mali nyingine zinazohusiana na shughuli hiyo. 

 

Post a Comment

0 Comments