Ticker

7/recent/ticker-posts

DKT. NCHIMBI:WATEKAJI HAWANA NIA NJEMA NA CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi

 NA MWANDISHI WETU

Matukio ya utekaji na uuaji wa baadhi ya wananchi yaliyolikumba taifa hivi karibuni yametajwa kuwa na nia ovu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali na nchi kwa ujumla.

Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka matukio ya utekaji na uuaji yanayochafua taswira ya nchi na miongoni mwake ni tukio la kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ali Kibao.

Katika mazungumzo yake na Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini yaliyofanyika leo kwenye ofisi ndogo za chama hicho, zilizopo Lumumba, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema mtu yeyote anaeshiriki kuteka na kuua raia nia yake ni kuharibu taswira ya chama Chao mbele ya umma.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi akisalimiana na wahariri 

"Ni mwendawazimu pekee anaeweza kutamka kwamba CCM inaweza kufanya jambo la kujiumiza yenyewe, CCM sio chama cha watu wajinga, ni chama cha siasa kisichojitambua ndicho kinaweza kufanya matendo ya kujikosanisha na wananchi wake," aalisema.

KUKATAA KUFARAKANISHWA

Dkt. Nchimbi amevitaka vyama vya siasa kutokubali kufarakanishwa na genge la watu wanao husika na vitendo vya utekaji nchini na kuwapa ushindi.

Amesema, hivi karibuni Kiongozi wa Chadema (Ally Kibao) alitekwa na kuuawa kikatili, jambo hilo sio dogo na  ndio maana wameona walizungumzie ikizingatiwa kuwa  Ilani ya CCM ukurasa wa 156 inasema, moja ya mambo ambayo watayafanya ni kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendelea kudhibiti usalama wa raia na mali zao.

“Watu wenye nia mbaya ndio wanaoendesha magenge ya uhalifu nchini ili kukikosanisha chama chetu na wananchi na kufarakanisha Taifa, ni watu hawa wanasababisha watu wenye busara sana waongee maneno yasiyotarajiwa,”

KAULI YA MBOWE YAMSIKITISHA

Dkt. Nchimbi alisema amemsikia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitoa muda wa mwisho kwa Serikali kuwataja wahusika wa matendo hayo maovu na akisema ikifika Septemba 23,2024 iwapo hawajatajwa watachukua hatua.

"Kwa mtu kama Mbowe, mwenye hekima kubwa, akiwa amefikishwa hapo na genge la watekaji; naye kaamini, kwamba kiongozi unaweza kumpa rais muda wa mwisho, ukishafikishwa hapo, ujue genge la watekaji limefanikiwa sana,” alisema Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi alisema, kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha kwamba, genge hilo halifanikiwi kwenye mkakati wake wa kufarakanisha watanzania na kuwapa ushindi.

“Ni wajibu wetu sisi na vyama vya upinzani, kuhakikisha tunashirikiana kuhakikisha genge la watekaji halifanikiwi kwenye mkakati wa kutufarakanisha. Kosa kubwa kuliko yote, ni kuwapa ushindi  watekaji,” amesema Dkt. Nchimbi.

MFANO WA MAREKANI

Dkt. Nchimbi alitolea mfano tukio lililotokea nchini Marekani, ambapo Donald Trump ambaye ni Rais Mstaafu wa nchi hiyo na mgombea urais kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika Novemba, mwaka huu, ambae  alipigwa risasi kwenye jaribio la kutaka kumuua, ambapo tukio hilo halikusabababisha mgawanyiko ndani ya Taifa hilo.

“Kilichojitokeza, vyama vikuu vya upinzani vinavyojitambua, chama chake cha Republican kililaani vikali na kikataka hatua zichukuliwe, chama cha Democrat kililaani vikali na kikataka hatua zichukuliwe,”

“Hatujasikia Democrat wanawalaumu Republican, wala hatujasikia Republican wanawalaumu Democrat, kwasababu wamejua lengo la anayefanya madhara yale ni kuwafarakanisha kama Taifa, wamekataa kufarakanishwa,” alisema Dkt. Nchimbi.

Alisema, CCM kinaviomba vyama vya upinzani kuiga jambo hilo na kukataa kufarakanishwa kwani CCM imefanya  kila njia kukataa kujiingiza kwenye mijadala ambayo haina tija.

KAULI ZA VIJANA WA BAVICHA 

Dkt. Nchimbi alisema, amesikia kauli mbiu ya  vijana wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) ya  ‘SAMIA MUST GO,’ jambo ambalo haliwezekani, ikizingatiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, yupo kwenye nafasi hiyo Kikatiba na atamaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba.

“Moja ya sifa ya kijana anayeandaliwa vizuri, anapaswa kufundishwa kuheshimu Katiba, tunaweka uchaguzi miaka mitano mitano ili wale watakaokuwa hawaridhiki ndani ya hiyo miaka mitano wapate nafasi nyingine ya kuchagua,” alisema.

Aliongeza, haiwezekani katikati ya msimu kukazuka kauli za kutaka Rais aachie ngazi.

"Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema mpaka leo, kila zilipoanza kelele ndani ya Chadema kwamba ‘Mbowe Must Go,’ zilishindikana kwa sababu ni kinyume cha Katiba yao.”

Alisema, wanaolinda Katiba ya Chadema wanamlinda kwa nguvu zao zote na imeshatokea zaidi ya mara tatu Mbowe akitakiwa aachie Uenyekiti wa chama hicho, lakini bado yupo kwenye nafasi yake.

“Mbowe hajaenda popote na Samia atakuwepo,” alisem Dkt. Nchini.

Post a Comment

0 Comments