Paulo Himid John (23) na Athuman Misanya(31) wakiwa chini ya ulinzi na nyama ya twiga waliyokamatwa mayo. |
NA MWANDISHI WETU
Kikosi kazi maalum cha kupambana na ujangili kwenye eneo la Hifadhi ya Jamii ya Burunge kinachoundwa na Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -TAWA, askari wa Burunge WMA, Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na askari wa Taasisi ya Chemchem ambayo imewekeza katika eneo hilo, kimefanikiwa kuwakamata majangili wawili walioua twiga.
Majangili hao ambao ni Paulo Himid John (23) na Athuman Misanya(31) ambao kwa pamoja wametiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.
Wawili hao waliokamatwa Februari 2,2024 wakiwa kwenye eneo la Burunge WMA, wakiwa na nyama ya twiga na mzoga wa mnyamapori huyo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50.
Akisoma hukumu hiyo juzi, Hakimu wa Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Victor Kimario alisema mahakama imewatia hatiani baada ya kujiridhisha na Ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Hakimu alisema adhabu hiyo imelenga kutoa mfano kwa watu wengine ambao wanajihusisha na matukio ya ujangili ambayo kimsingi yana lengo la kuhujumu uchumi.
Mbali na kuhukumiwa kifungo hicho pia vifaa vilivyotumika kutekeleza uhalifu huo ikiwemo pikipiki vimetaifishwa na serikali.
Awali Waendesha mashtaka ambao ni Maofisa kutoka TAWA, Getrude William Kariongi na Shahidu Kajwagya wakisaidiwa na wakili wa serikali Mwanaidi Chuma waliomba mahakama kutuoa adhabu kali kwa wahalifu hao.
Kwamba kosa walilofanya majangili hao ni la kuhujumu uchumi kwa kuua twiga ambao ni kivutio kikubwa cha utalii na nembo ya Taifa.
Watuhumiwa walikuwa wanatetewa na Justine Jackson ambaye kabla ya kupangwa siku ya hukumu aliwasilisha maombi ya kutaka mahakama kuwaita upya mashahidi wawili wa Jamhuri ili awaulize maswali baada ya kupitia Ushahidi, hoja ambayo ilipingwa na mahakama.
Waendesha mashtaka waliiomba mahakama kutupa maombi hayo kwani wakati shahidi wa Jamuhuri namba moja na namba mbili wakitoa ushahidi juu ya kukamatwa kwa majangili hao watuhumiwa walikuwepo na mahakama iliwapa nafasi ya kuwadodosa maswali (cross-examination).
Kariongi alisema ,watuhumiwa walipewa fursa ya kuwauliza maswali mashahidi lakini walisema hawana maswali.
Alieleza kwa mujibu wa kifungu cha 147 kidogo cha 4 cha sheria ya ushahidi inazungumzia maswali zaidi ( further cross-examination or examinations in chief )ni kwa maana ya kwamba kama watuhumiwa walisema hawana maswali yaani hawakuuliza maswali kabisa na kwa mujibu wa sheria hiyo ni kuwe na swali lililoulizwa na wakili apate nafasi ya kuendelea kuuliza maswali mengine kutokea pale lilipo ulizwa swali la awali.
Katika kukazia hoja yake, alinukuu uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi katika kesi ya Bakari Yahaya Ausen dhidi ya Jamuhuri kesi namba 646/2016 na maamuzi ya Kesi yaliyotolewa na mahakama ya rufaa kwenye kesi ya Shomari Mohamedi Mkwama dhidi ya Jamuhuri kesi namba 606 mwaka 2021 iliyoketi Dar es salam ambayo ilieleza mazingira ya mashahidi kuitwa tena.
Baada ya hoja hizo, Hakimu mfawidhi Kimario alitoa uamuzi mdogo na kukataa ombi la upande wa utetezi kwani wakati wa ushahidi wa mashahidi hao watuhumiwa walipewa nafasi ya kuuliza maswali na walisema hawana.
Pamoja na kushiriki katika kukamata Taasisi ya Chemchem imewekeza shughuli za Utalii wa picha na hoteli na inatumia zaidi ya sh 450 milioni kupambana na ujangili na kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.
0 Comments