Obeid Francis mwanakijiji wa kijiji cha Kasenyi aliyenusurika kuliwa na mamba baada ya kuyatumia vema mafunzo ya kukabiliana na havari ya mnyamapori huyo yöliyotolewa na TAWA. |
NA MWANDISHI WETU
Si jambo rahisi kuamini kama yupo mtu anaweza kukabiliana na mamba hadi kufikia hatua ya kuyanusuru maisha yake, Obeid Francis amelifanikisha hilo. Obeid (44) ni mkazi wa kijiji cha Kasenyi kilichopo wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, ni mmoja kati ya watu wapambanaji kijijini hapo.
Anasimulia kilichomkuta siku ya tukio ambalo anakiri wazi kuwa kamwe hatalisahau na kwamba kama isingekuwa elimu aliyoipata kutoka kwa maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, huenda sasa angekuwa ni marehemu n ahata mwili wake usingeonekana.
Ilikuwaje? Obeid anasema tukio la kuweza kuikoa nafsi yake mbele ya mamba lilitokea Oktoba 25, 2023 kijijini kwake Kasenyi majira ya jioni.
Ilikuwa ni kawaida yake kwenda pembezoni mwa ziwa Victoria kwa ajili ya kuoga, hakuwa na wasiwasi kwa sababu aliamini hakuna mnyamapori yeyote anaeweza kufika kwenye eneo hilo, ambalo kwake lilikuwa ni la mazoea.
Akiwa ameshaanza zoezi lake la kuoga kama ilivyo kawaida yake na pengine kawaida ya wakazi wengi wa Kijiji hicho, ghafla alishtukia mkono wake wa kushoto umepigwa kumbo zito.
Obeid akiwa na Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja
Hakujua nini kinaendelea, ila kumbo hilo liliishia kumtupa ndani ya maji marefu na baadae kuibuliwa, haraka alipata ufahamu kuwa tayari yuko kwenye himaya ya mamba.
“Yule mamba alikifanya kitendo kile cha kunizamisha na kuniibua juu mara kadhaa, nilihisi tayari nimeshakuwa chakula cha mnyamapori huyo.
“Jambo la kushukuru ni kuwa nilishawahi kupata elimu ya kukabiliana na hatari kama hiyo kutoka TAWA, nilichokifanya ni kuikumbuka na kuifanyia kazi, nilipata ujasiri na kukaza kidole changu kikubwa (gumba) kisha nikamchoma jichoni, kitendo kile kilimuumiza mamba na hatimae aliniachia ili kujinusuru, hatua ambayo ilisaidia kuninusuru na mimi pia,”alisema.
Anasema baada ya mamba kumuachia alipata ujasiri wa kutoka majini na kujikokota hadi nchi kavu huku akiwa na majeraha kwenye mkono wake na baadhi ya maeneo.
Matukio ya wananchi kupata madhara yatokonayo na wanyamapori wakali na waharibifu hasa wale waishio pembezoni mwa maziwa na mito yamekuwa yakitokana na vitendo vya wananchi hao kufanya shughuli zao karibu na maji kama vile kuogelea/kuoga, kufua na kufanya uvuvi usio rafiki mambo ambayo yamekuwa yakihatarisha maisha yao.
TAWA imekuwa ikifanya jitahada endelevu za kutoa elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko katika maeneo mbalimbali nchini kwa wananchi ili kuwapatia mbinu za kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na wanyamapori hao na inasisitiza wananchi kuzingatia elimu hiyo ili waendelee kuwa salama.
0 Comments