Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko |
A. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kufuatia Taarifa iliyowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa mwaka 2024/25.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema na fursa ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2024/25. Aidha, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama kama Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati katika Serikali ya Awamu ya Sita (6) na kuwasilisha Hotuba hii, kwa namna ya kipekee napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Uteuzi huu ni dhamana na heshima kubwa kwangu katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Nishati inakidhi matarajio ya Watanzania ya kupata umeme wa uhakika pamoja na kuendeleza rasilimali za mafuta na gesi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi yetu. Nitumie fursa hii kuahidi, na kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha, kutekeleza majukumu yangu kwa weledi na uadilifu mkubwa kwa kushirikiana na Bunge lako Tukufu pamoja na wadau wengine katika Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Februari, 2024 Taifa letu lilimpoteza aliyekuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ali Hassan Mwinyi. Aidha, kabla ya hapo, tarehe 10 Februari, 2024 Taifa lilimpoteza aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa. Kwa masikitiko makubwa naungana na Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, familia, ndugu, jamaa, marafiki na watanzania wote kwa ujumla kwa kuondokewa na viongozi wetu hawa, tuliwapenda lakini Mwenyezi Mungu amewapenda zaidi. Tunaomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za wapendwa wetu mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Spika, Julai mosi, 2023, Bunge lako Tukufu lilimpoteza Mhe. Francis Leonard Mtega, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali. Aidha, tarehe 8 Aprili 2024, Bunge lako lilimpoteza Mhe. Ahmed Yahya Abdulwakil aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani, Zanzibar. Naungana na Wabunge wenzangu kutoa pole kwa Bunge lako Tukufu, familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na misiba hiyo. Tunaomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi, Amina. Vilevile, naungana na Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla, kuwapa pole watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali katika mwaka 2023/24, ikiwemo yaliyotokana na mafuriko na maporomoko ya mawe na matope katika maeneo ya Hanang Mkoani Manyara; Kibiti na Rufiji Mkoani Pwani pamoja na Malinyi, Ulanga, Ifakara na Mlimba Mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Spika, kipekee nawashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), kwa uongozi na juhudi zao katika kuleta maendeleo ya Taifa letu na kwa ushirikiano wanaonipa katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya Wizara ya Nishati. Nikiri kuwa maelekezo na miongozo ya viongozi wetu hawa ni msingi wa mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Sekta ya Nishati. Aidha, napenda kumpongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kusimamia kwa umahiri utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza kwa dhati wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Hii ni heshima kubwa na Tunu kwa Watanzania wote kwa ujumla kwa kuthaminiwa na kutambuliwa katika medani za kimataifa. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu ili azidi kukupa nguvu na hekima zaidi katika kutekeleza majukumu yako.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii tena kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuliongoza Bunge letu Tukufu kwa umahiri mkubwa. Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Bi. Nenelwa Mwihambi, Katibu wa Bunge kwa usimamizi wa shughuli za Bunge. Ni dhahiri kuwa, chini ya uongozi wenu Bunge letu limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo katika kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza wajibu wa kuwaletea wananchi maendeleo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri na manaibu Waziri walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nampongeza Mhe. Jerry William Silaa (Mb), aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. Deogratius John Ndejembi (Mb), aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (Mb), aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo; Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi; Mhe. Dunstan Luka Kitandula (Mb), aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii; Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.) aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati; Mhe. Daniel Baran Sillo (Mb), aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb), aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nawatakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza, Mhe. Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa jimbo la Mbarali kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo kuwa mwakilishi wa wananchi katika jimbo hilo. Hakika ni heshima kubwa uliyopewa na wananchi wa Mbarali na ninakutakia kila la kheri katika kutekeleza jukumu lako la uwakilishi katika Bunge letu Tukufu.
Mheshimiwa Spika, kipekee nampongeza Mhe. Dkt. David Mathayo David (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mhe. Kilumbe Shaban Ng’enda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Vilevile, nawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushauri na maoni yao katika kuendeleza na kusimamia Sekta ya Nishati kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu na watu wake.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.), Naibu Waziri wa Nishati kwa kuendelea kunisaidia kwa karibu katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, napenda kumshukuru Katibu Mkuu Mha. Felchesmi Jossen Mramba kwa utendaji kazi wake mahiri na ushirikiano anaonipa katika kutekeleza shughuli zangu za kila siku za Wizara. Nampongeza pia, Dkt. James Peter Mataragio kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati. Nawashukuru pia Wakuu wa Idara na Vitengo, Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Watumishi wote wa Wizara kwa ujumla kwa ushirikiano na juhudi zao katika kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa, nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Bukombe kwa kuendelea kunipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu kama Mbunge wao. Kutokana na majukumu ya kitaifa kama Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuna wakati wananikosa jimboni, lakini kwa wema wao wanaendelea kunivumilia na kunipa ushirikiano mkubwa. Nawaahidi kuendelea kuwa mtumishi wao mwaminifu katika kutekeleza shughuli za maendeleo. Aidha, namshukuru mke wangu mpendwa Benadetha Clement Mathayo kwa maombi na upendo wake wa dhati kwangu na watoto wetu. Amekuwa mvumilivu katika kipindi chote ninapokuwa natekeleza majukumu yangu ya Ubunge, Uwaziri na Unaibu Waziri Mkuu na kukubali kubeba na kutekeleza baadhi ya majukumu ya kifamilia.
Mheshimiwa Spika, nitumie pia fursa hii kuvishukuru na kuvipongeza Vyombo vya Habari vikiwemo redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/24. Vyombo hivyo vimekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia kwa karibu miradi na shughuli zinazotekelezwa na Wizara ya Nishati na kuelimisha pamoja na kuhabarisha umma kuhusu mafanikio yaliyopatikana. Ni matumaini yangu kuwa, ushirikiano huu utazidi kuimarika katika Mwaka wa Fedha wa 2024/25 kwa manufaa ya Taifa letu na wananchi kwa ujumla katika upatikanaji wa taarifa kuhusu Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, Hotuba hii imeandaliwa kwa kuzingatia maudhui ya Hotuba ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2023/24 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2024/25.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka 2023/24, pamoja na Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2024/25.
A. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA 2023/24
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2023/24 uliongozwa na vipaumbele mbalimbali. Vipaumbele hivyo vilijikita katika kukamilisha miradi mbalimbali ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na kuendelea kuchukua hatua nyingine za kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini; kuendelea kupeleka umeme vijijini, vitongojini, katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, maeneo ya kilimo na viwanda na katika shule na mahakama za mwanzo vijijini; pamoja na kutekeleza mikakati na programu mbalimbali za kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking) nchini.
Mheshimiwa Spika, vipaumbele vingine vilikuwa ni kuanza maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG); kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima - Uganda Hadi Tanga – Tanzania (EACOP), shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Kimkakati, usambazaji wa gesi asilia viwandani, majumbani na nchi jirani, kuimarisha matumizi ya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas-CNG)katika magari pamoja na kunadi vitalu vilivyo wazi katika maeneo ya nchi kavu na baharini ili viendelezwe. Aidha, Wizara ilielekeza pia nguvu katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli, kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja kuimarisha ufanisi katika kushughulikia bidhaa hizo.
Mheshimiwa Spika, sehemu B ya Hotuba yangu ukurasa wa 8 hadi 119 inaelezea kwa kina utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2023/24 pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na shughuli za utafutaji, uendelezaji, usambazaji na matumizi ya mafuta na gesi.
Bajeti ya Matumizi ya Wizara na Mtiririko wa Fedha kwa Mwaka 2023/24
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24, Wizara ya Nishati iliidhinishiwa kutumia jumla ya Shilingi Trilioni Tatu na Bilioni Arobaini na Nane, Milioni Mia Sita Thelathini na Mbili, Mia Tano Kumi na Tisa Elfu (Shilingi 3,048,632,519,000) ambapo Shilingi Trilioni Mbili, Bilioni Mia Sita na Tisa, Milioni Mia Moja Hamsini na Sita, Mia Moja Ishirini na Nane Elfu (Shilingi 2,609,156,128,000) ziliidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Shilingi Bilioni Themanini na Saba, Milioni Mia Tisa Ishirini na Tisa, Mia Sita Tisini na Nane Elfu (Shilingi 87,929,698,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2024, Wizara ilipokea jumla ya Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Nane Kumi na Tatu na Milioni Ishirini na Sita, Mia Moja Arobaini na Saba Elfu, Mia Moja Hamsini na Sita (Shilingi 1,813,026,147,156), ambapo Shilingi Bilioni Ishirini na Saba na Milioni Sabini na Tisa na Ishirini na Sita Elfu, Mia Saba Kumi na Sita (Shilingi 27,079,026,716) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Saba Themanini na Tano, Milioni Mia Tisa Arobaini na Saba, Mia Moja Ishirini Elfu, Mia Nne Arobaini (Shilingi 1,785,947,120,440) ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
SEKTA NDOGO YA UMEME NA NISHATI JADIDIFU
Uzalishaji wa Umeme
Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme, mafanikio yafuatayo yalipatikana katika mwaka 2023/24:
a) Uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia MW 2,138 Machi, 2024 kutoka MW 1,872.1 zilizozalishwa mwaka 2022/23, ikiwa ni ongezeko la asimia 14.2;
b) Kuanza kwa uzalishaji wa umeme kupitia Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 ambapo tayari uzalishaji umeanza kwa MW 235 kupitia mtambo Namba 9. Aidha, matarajio ni mradi huu kukamilika Desemba, 2024 kwa mitambo yote nane (8) yenye uwezo wa kuzalisha MW 235 kila moja kuwa inazalisha umeme;
c) Kukamilisha ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo kwa sasa mitambo yote minne (4) inafua umeme kiasi cha MW 40 kila mmoja na hivyo kuwezesha uzalishaji wa umeme kuingizwa katika gridi ya Taifa;
d) Kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Rusumo (MW 80)unaliojengwa kwa ushirikiano wa nchi tatu (3) za Tanzania, Burundi na Rwanda kwa mgawanyo sawa wa umeme kwa kila nchi. Kukamilika Mradi kunaiwezesha nchi yetu kupata MW 27 katika Gridi ya Taifa;
e) Ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa jua Mkoani Shinyanga wa MW 150 unaendelea na matarajio ni umeme huo kuanza kuzalishwa ifikapo Januari, 2025;
Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na Malagarasi – MW 49.5, Ruhudji – MW 358, Rumakali – MW 222, Kakono – MW 87.8 na Kikonge – MW 321 ambapo hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake ni kama inavyofafanuliwa katika Hotuba yangu.
Usafirishaji na Usambazaji Umeme
Mheshimiwa Spika, umeme ukishazalishwa, hauna budi kusafirishwa na kusambazwa ili uweze kuwafikia watumiaji, hivyo ni muhimu kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme. Kutokana na hatua zilizochukuliwa katika mwaka 2023/24 za kuimarisha miundombinu hii, yalipatikana mafanikio yafuatayo:
a) Miundombinu ya kusafirisha umeme imeongezeka na kufikia jumla ya urefu wa kilomita 7,745.4 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.7 ikilinganishwa na kilomita 6,363.3 za mwaka 2022/23;
b) Kuanza kutumika kwa njia ya kusafirisha umeme wa Kilovoti 400 kutoka JNHPP hadi Chalinze pamoja na kituo kipya cha kupoza umeme cha Chalinze cha Kilovoti 400/220/132 kinachotumika kupoza na kusafirisha umeme unaotoka JNHPP na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa;
c) Kukamilika kwa asilimia 99 kwa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dodoma kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya umeme (SGR Lot II);
d) Kukamilika kwa asilimia 99.4 kwa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga. Aidha, ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Arusha hadi Namanga yenye urefu wa kilomita 114.3 umefikia asilimia 97.5 na kituo cha kupoza umeme cha Lemugur kimekamilika kwa asilimia 100 na kuwashwa;
e) Miundombinu ya kusambaza umeme imeongezeka na kufikia kilomita 176,750.9, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.9 ikilinganishwa na kilomita 168,548.5 za mwezi Mei, 2023;
f) Jumla ya wateja 4,784,297 wameunganishiwa umeme hadi kufikia Machi, 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.4 ikilinganishwa na wateja 4,319,258 waliokuwa wameunganishiwa umeme Juni, 2023;
Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya usafirishaji wa umeme iliyoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 220 kutoka Rusumo hadi Nyakanazi; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma (TAZA); ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Projects) – Gridi Imara.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kuimarisha utoaji wa huduma ya umeme kwa wananchi kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupanua kituo cha huduma kwa wateja (Call Center) kwa kuongeza vifaa na wapokea simu kutoka mawakala 63 hadi 100; kuanzisha mfumo unaomuwezesha mteja kuhudumiwa kwa haraka zaidi bila kupiga simu kwa njia ya ujumbe wa simu (CHATBOT) na kuanzisha mfumo utakaowawezesha wateja kupata taarifa maalumu za hali ya upatikanaji wa umeme kwa haraka kwa njia ya ujumbe wa simu ambayo ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.
Upelekaji wa Nishati Vijijini
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kuchukua hatua za kuimarisha upatikanaji wa nishati vijijini ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2024 jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishwa na umeme. Aidha, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi vijijini, jumla ya taasisi 63,509 zinazotoa huduma kwa jamii ikiwemo Elimu, Biashara, Pampu za Maji, Vituo vya Afya na Nyumba za Ibada zilikuwa zimeunganishiwa umeme ikilinganishwa na taasisi 43,925 za Aprili, 2023. Vilevile, Serikali iliendelea kuchukua hatua za kupeleka umeme vitongojini, katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, viwanda na kilimo na katika shule na mahakama za mwanzo Vijijini ambapo mafanikio yaliyopatikana ni kama inavyofafanuliwa katika Hotuba yangu.
Nishati Safi ya Kupikia
Mheshimiwa Spika, kutokana na athari za matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na athari za kiafya kwa wananchi wetu, uharibifu wa mazingira pamoja na athari nyingine za kiuchumi na kijamii, Serikali iliendelea kutekeleza mikakati mahsusi ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliidhinisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034, unaolenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya watanzania kuwa wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Malengo ya Mkakati huu ambao unabainisha majukumu ya wadau mbalimbali ni pamoja na kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia; kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia; kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia; pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na wadau Wizara iliratibu na kushiriki katika mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai mwezi Novemba-Desemba, 2023. Kupitia Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Programu ya Nishati Safi ya kupikia itakayowawezesha Wanawake Barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme-AWCCSP) kutumia nishati safi ya kupikia. Aidha, mwezi Mei, 2024 kutafanyika mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika, Paris Ufaransa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wa Norway, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nishati Duniani (International Energy Agency-IEA) na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Mkutano huo pamoja na mambo mengine, unalenga kujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuimarisha Sera, ugharamiaji na ushirikiano katika kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia Barani Afrika.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa na Wizara kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ni pamoja na kusambaza kwa wananchi mitungi ya gesi ya LPG, gesi asilia na majiko banifu; kutekeleza program mbalimbali za kuhamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kuendesha kongamano la wanawake la nishati safi ya kupikia lililofanyika Mkoani Dodoma tarehe 9 Machi, 2024; na kushirikiana na Jeshi la Magereza ili kuwezesha Jeshi hilo (Magereza, Kambi za Makazi ya Watumishi, Ofisi, Vyuo, Shule na Hospitali) kutumia nishati safi ya kupikia.
SEKTA NDOGO YA MAFUTA NA GESI ASILIA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24 Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuendeleza Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia nchini katika maeneo ya utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta na gesi, ambapo utekelezaji ulikuwa kama ifuatavyo:
a) Majadiliano ya Mikataba ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia Kuwa Kimiminika (LNG) yaliendelea ili kuboresha rasimu za awali za Mikataba hiyo kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Taasisi nyingine za Serikali;
b) Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati vya Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi– Wembere, Songo Songo Magharibi na Vitalu Namba 4/1B na 4/1C ziliendelea kwa kuchukua hatua mbalimbali kama inavyofafanuliwa katika Hotuba yangu. Aidha, Serikali iliridhia kutolewa kwa leseni ya uendelezaji wa gesi asilia iliyogunduliwa katika eneo la Ntorya katika kitalu cha Ruvuma kwa TPDC kwa niaba ya mwekezaji (kampuni ya ARA Petroleum). Uendelezaji wa gesi iliyogunduliwa Ntorya unatarajiwa kuiwezesha nchi kupata gesi ya takribani futi za ujazo milioni 60 kwa siku katika kipindi cha awali cha miaka miwili na kuongezeka hadi kufikia uzalishaji wa Futi za Ujazo Milioni 140 kwa siku baada ya kipindi hicho na hivyo kuimarisha upatikanaji wa gesi asilia nchini;
c) Kufanikisha ununuzi wa asilimia 20 ya hisa za Kampuni ya Wentworth kwenye Mkataba wa Uendeshaji wa Kitalu cha Uzalishaji gesi asilia cha Mnazi Bay kilichopo Mtwara. TPDC imeongeza uwekezaji katika kitalu hicho kwa asilimia 20;
d) Miradi ya usambazaji wa gesi asilia viwandani, katika taasisi na majumbani iliendelea kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kujenga bomba la gesi asilia lenye urefu wa kilometa 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach Dar es Salaam lililowezesha kuunganishwa kwa miundombinu ya gesi asilia kwenye viwanda na hoteli mbalimbali na kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka BVS 3 kuelekea Kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo mkoani Lindi lenye urefu wa kilomita 10.04 lililowezesha kuunganisha nyumba 209 na gesi asilia. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kukamilisha taratibu za kumpata Mkandarasi wa kujenga miundombinu ya kuunganisha nyumba 451 mkoani Lindi (Kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo) na nyumba 529 mkoani Pwani (Mkuranga);
e) Ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia (Compressed Natural Gas-CNG) katika magari uliendelea kwa kushirikisha pia Sekta Binafsi. TPDC na GPSA ziliendelea na taratibu za kumpata Mshauri Mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa michoro ya kihandisi na Tathmini ya Athari ya Mazingira na Jamii ili kuwezesha GPSA kujenga vituo vya CNG katika bohari za Dar es Salaam na Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuwezesha vyombo vya moto vinavyomilikiwa na Serikali kutumia CNG. Aidha, Sekta Binafsi iliendelea kutumia fursa ya matumizi ya CNG katika vyombo vya moto kwa kujenga vituo vya CNG Dar es Salaam na Pwani pamoja na karakana nane (8) za kubadilisha mifumo ya matumizi ya CNG kwenye magari ambayo ni nyenzo muhimu ya kuchochea matumizi ya CNG katika magari. Hatua hizi zimeendelea kuimarisha matumizi ya gesi asilia asilia (CNG) katika magari;
f) Hali ya upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli nchini iliendelea kuwa nzuri, ikiwemo kutengamaa kwa bei za mafuta ikilinganishwa na mwaka uliopita pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa Dola za Marekani kwa ajili ya kulipia mafuta yaliyoagizwa nchini;
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima - Uganda hadi Tanga - Tanzania (East African Crude Oil Pipeline – EACOP) kwa kukamilisha malipo ya fidia ya Shilingi bilioni 34.93 kwa wananchi 9,823 kati ya 9,904 waliopisha utekelezaji wa mradi, sawa na asilimia 99.2; kukamilika kwa ujenzi wa nyumba 340 sawa na asilimia 100 ya makazi mbadala kwa wananchi 294 waliopoteza makazi na kupisha mkuza; kukamilika kwa ujenzi wa karakana ya kuweka mfumo wa upashaji joto kwenye mabomba; na kuendelea na ujenzi wa maeneo 14 ya makambi. Aidha, mabomba yenye urefu wa Kilomita 400 yameshawasili nchini na zoezi la kuwekewa mfumo wa kupasha joto, usalama na mawasiliano wa bomba (thermal insulation and fiber optic cables) linaendelea. Vilevile, hadi kufikia Machi, 2024, Serikali ilikuwa imelipa jumla ya Dola za Marekani milioni 289.78 sawa na asilimia 94 ya kiasi kinachotakiwa kuchangiwa kama mtaji katika Kampuni ya EACOP Ltd. Utekelezaji wa Mradi kwa ujumla umefikia asilimia 27.1.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliendelea kusimamia na kudhibiti Sekta ya Nishati ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za Sekta hiyo unazingatia sheria na taratibu zilizopo pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. PURA iliendelea na maandalizi ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kupitia Duru ya Tano (5) kwa kuandaa rasimu ya Mkataba Kifani wa Ugawanaji Mapato (Model Production Sharing Agreement-MPSA) wa mwaka, 2024 (MPSA, 2024) kwa ajili ya kutumika katika zoezi hilo na kukamilisha Mwongozo wa Kupata Kampuni za Kijiofizikia zitakazoshirikiana na PURA katika zoezi la kunadi vitalu ambapo taratibu za kupata kampuni hizo zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji katika rasilimali zilizopo katika maeneo yao, Serikali kupitia PURA na TPDC imeandaa rasimu ya Miongozo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi asilia inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni, 2024. Aidha, maandalizi ya rasimu yamehusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.
Mheshimiwa Spika, EWURA iliendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za mafuta, gesi na umeme ambapo Mamlaka hiyo ilitoa leseni 34 kwa kampuni za mafuta kwa ajili ya kuagiza na kuuza mafuta kwa jumla; vibali vya ujenzi (construction approvals) 237 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta, miundombinu ya kuhifadhia LPG, matumizi binafsi na ghala ya kuhifadhia mafuta na leseni 1,163 kwa wataalamu wenye sifa za kufunga mifumo ya umeme. Aidha ili kuimarisha usimamizi, udhibiti na utoaji wa huduma, EWURA iliboresha Kanuni (Rules) mbalimbali ikiwemo The Petroleum (Wholesales Storage Retail and Consumer Installation) Rules, 2023; The Petroleum (Retail Operations in Townships and Villages) (Amendment) Rules, 2023 na the Energy and Water Utilities Regulatory Authority (Petroleum Products Price Setting) (Amendment) Rules, 2023.
CHANGAMOTO ZILIZOPO NA UTATUZI WAKE
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2023/24, Sekta ya Nishati ilikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme na gesi asilia kutoendana na mahitaji kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme. Kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali, ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme pamoja na kukarabati na kufanya matengenezo ya miundombinu ya umeme, hali ya upatikanaji wa umeme nchini unaokidhi mahitaji imeendelea kuimarika na kuwa nzuri kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine iliyopo ni vitendo vya hujuma/uhalifu katika miundombinu ya umeme, ambapo Serikali iliendelea kuwachukulia hatua za kisheria waliobanika kutekeleza vitendo hivyo. Aidha, niendelee kutoa wito kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wote watakaobainika kufanya vitendo vya hujuma/uhalifu katika miundombinu ya umeme, kunakosababisha hasara na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyobainisha awali, tulikabiliwa pia na changamoto ya upatikanaji wa Dola za Marekani kwa ajili ya kulipia mafuta yaliyoagizwa nchini, hali ambayo ilisababisha wafanyabiashara kupunguza kiasi cha mafuta kilichokuwa kinaagizwa. Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na wadau wengine ilichukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya mikataba ya kuagiza mafuta na kuruhusu matumizi ya fedha za kigeni zikiwemo fedha ya Uingereza (British Pound), Umoja wa Ulaya (Euro) na Umoja wa Nchi za Uarabuni (Dirham). Aidha, Wizara ya Nishati kupitia EWURA iliimarisha ukaguzi katika vituo vya mafuta ili kuhakikisha mafuta yanapatikana wakati wote katika maeneo yote nchini.
B. MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2024/25
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka 2023/24, sasa napenda kuwasilisha Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2024/25.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25 utekelezaji wa majukumu ya Wizara utaongozwa na vipaumbele mbalimbali vinavyojikita katika kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kufikisha gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia; kupeleka nishati vijijini, ikiwemo katika vitongoji; kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwemo mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG Project) na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (East African Crude Oil Pipeline - EACOP). Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza na kusimamia shughuli za utafutaji na uendelezaji katika vitalu vya kimkakati na wawekezaji; usambazaji wa gesi asilia viwandani, katika taasisi na majumbani na kuimarisha matumizi ya CNG katika magari.
Mheshimiwa Spika, vipaumbele vingine ni kuendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking) nchini pamoja na upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini kupitia uanzishwaji wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo; kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja na ufanisi katika kushughulikia upatikanaji wa bidhaa hizo; kuimarisha uwekezaji na ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na uzalishaji na usambazaji wa umeme na kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma, tija na ufanisi katika uendeshaji wa Taasisi/Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya TANESCO, TPDC, EWURA, PURA na PBPA pamoja na Kampuni Tanzu. Wizara pia itaendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi asilia pamoja na rasilimali watu ya Wizara ya Taasisi zake na upatikanaji wa vitendea kazi muhimu.
Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2024/25 pamoja na mambo mengine, umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) 2021/22 – 2025/26, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Maagizo ya Viongozi wa Kitaifa katika Sekta ya Nishati, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2024/25 pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26). Miongozo mingine iliyozingatiwa ni Sera, Mikakati na Programu mbalimbali za Kisekta na Kitaifa pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ya mwaka 2030 kuhusu masuala ya nishati.
Mheshimiwa Spika, sehemu C ya Hotuba yangu ukurasa wa 119 hadi 173 inatoa maelezo na ufafanuzi wa kina kuhusu programu, miradi, mikakati na kazi zitakazotekelezwa katika mwaka 2024/25. Kwa ufupi Wizara itatekeleza yafuatayo:
SEKTA NDOGO YA UMEME NA NISHATI JADIDIFU
Miradi ya Kuzalisha Umeme
Mheshimiwa Spika, moja ya kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa na umeme unaotosheleza mahitaji ya sasa na siku zijazo, umeme wa uhakika na unaotokana na vyanzo mbalimbali (energy mix). Hii ni kwa kuzingatia umuhimu wa nishati hiyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi yetu na Taifa lolote. Ili kutimiza azma hiyo, Wizara imepanga kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme kwa utumia Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambapo kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la mitambo (power house) na ufungaji wa mitambo saba (7) ya kuzalisha umeme ambayo kwa sasa ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 19.2 kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi kwenda Gongolamboto hadi Mbagala Jijini Dar es Salaam na kufunga transfoma maeneo ya Gongolamboto na Mbagala.
Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya uzalishaji wa umeme itakayotekelezwa ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Malagarasi – MW 49.5; mradi wa kuzalisha umeme jua Shinyanga – MW 150; ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Hale; mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Kakono – MW 87.8; na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya mto Kikonge–MW 321. Aidha, Serikali pia itaendelea kuelekeza nguvu katika uzalishaji wa umeme jotoardhi ambapo itakamilisha uchorongaji wa visima vitatu (3) vya uhakiki (exploratory wells) ili kuhakiki hifadhi, kiwango na ubora wa rasilimali ya jotoardhi katika mradi wa Ngozi (Mbeya) wenye uwezo wa kuzalisha MW 30 kwa awamu ya kwanza pamoja na kuanza ujenzi wa mtambo mdogo wa kuzalisha umeme (wellhead generator) wa MW 5. Vilevile, Serikali itaanza utekelezaji wa programu ya uchorongaji wa visima vinne (4) vya uhakiki katika mradi la Kiejo Mbaka (Mbeya) wenye uwezo wa kuzalisha MW 60.
Miradi ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme
Mheshimiwa Spika, miundombinu imara ya kusafirisha na kusambaza umeme ndiyo msingi thabiti wa kuwa na umeme wa uhakika. Hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika mwaka 2024/25 ni pamoja na kukamilisha mradi wa kusafirisha umeme kutoka Julius Nyerere Hydro Power Plant hadi Chalinze – Kilovoti 400 na Kituo cha Kupoza Umeme, Chalinze ambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kumalizia kazi zilizobaki katika kituo cha kupoza umeme ikiwemo majengo, barabara, njia ya kusafirisha umeme na marekebisho mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze na Dodoma. Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha kusafirisha umeme unaotoka katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere kupitia Chalinze, kwenda mkoani Dodoma na kuusambaza katika Mikoa mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, Miradi mingine ya usafirishaji wa umeme itakayotekelezwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze - Kinyerezi – Mkuranga; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze – Segera na msongo wa Kilovoti 220 Segera – Tanga; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 220 kutoka Chalinze – Bagamoyo hadi Ununio Dar es salaam na ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli Shinyanga Kilovoti 400/220/33; ujenzi wa njia ya kusafirishaumeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma ( TAZA) na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) – Gridi Imara kwa kuendelea na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupoza umeme. Serikali pia itaendelea kufanyamatengenezo katika mitambo ya kuzalisha umeme, miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme pamoja na vituo vya kupoza umeme ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana wakati wote.
Miradi ya Nishati Vijijini
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2024/25, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kuchukua hatua za kupeleka nishati vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo. Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ununuzi wa wakandarasi wa kutekeleza mradi, kufanya usanifu wa kina wa mradi na kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi. Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji katika Mkoa wa Songwe na Kigoma kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme Msongo Mdogo, kufunga transfoma na kuunganisha wateja. Vilevile, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 3,060 (vitongoji 15 kila Jimbo) kwa kujenga miundombinu ya mradi, kufunga transfoma na kuunganisha wateja.
Mheshimiwa Spika, miradi mingine itakayotekelezwa ni mradi wa ujazilizi Awamu ya Pili B; mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili C; mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Vijijini-Miji; mradi wa kusambaza umeme katika Migodi Midogo, Maeneo ya Kilimo na Viwanda; mradi wa kupeleka umeme katika minara ya mawasiliano ya simu na mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua kwenye makazi yaliyopo Visiwani na yaliyopo mbali na Gridi ya Taifa.
Nishati Safi ya Kupikia
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25 Serikali itaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuimarisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia nchini. Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 kwa kupatia ufumbuzi vikwazo vya matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo gharama kubwa, upatikanaji hafifu na uhaba wa miundombinu yake na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya nishati zisizo safi na salama za kupikia. Aidha, Wizara itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya Nishati Safi ya Kupikia inayolenga Kuwawezesha Wanawake Barani Afrika Kutumia Nishati Safi ya Kupikia (African Women Clean Cooking Support Programme – AWCCSP.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye Kaya zilizopo katika maeneo ya Vijijini na Vijiji-Miji; kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya ununuzi wa mashine zitakazotumika katika uzalishaji wa mkaa huo; kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ujenzi wa miundombinu ya nishati ya kupkia katika maeneo 211 pamoja na kuendelea na usambazaji wa gesi asilia majumbani, hususan katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia na kuendeleza Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi kwa kuchukua hatua mbalimbali, lengo likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta hii katika maendeleo ya Taifa letu unaimarika. Serikali itaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati na kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka kitalu cha Ruvuma (Ntorya) hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 34.2 na uwezo wa kubeba futi za ujazo milioni 140 kwa siku. Aidha, Serikali inatarajia kukamilisha majadiliano ya Mikataba ya mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia Kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) ili utekelezaji wake uanze.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, usanifu wa kihandisi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga pamoja na Kongani ya Viwanda ya Kwala Mkoani Pwani; kukamilisha ujenzi wa vituo vya CNG (Kituo Mama katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Vituo vidogo vya Kairuki na Muhimbili) mkoani Dar es Salaam; na ununuzi wa vituo vitano (5) vya CNG vinavyohamishika (mobile CNG stations) vitakavyotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, Sekta Binafsi itaendelea kushiriki katika ujenzi wa vituo vya CNG pamoja na karakana za kubadilisha mifumo ya matumizi ya nishati ya gesi asilia (CNG) kwenye magari. Vilevile, TPDC itakamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa usambazaji wa gesi asilia chini ya ufadhili wa REA ambapo nyumba 980 zitaunganishwa katika mikoa ya Lindi na Pwani; na kuanza awamu ya pili ya mradi huo kwa kuendelea kusambaza gesi asilia maeneo ya Mkuranga, mkoani Pwani.
MheshimiwaSpika, miradi mingine itayakayotekelezwa ni mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima - Uganda hadi Tanga - Tanzania (East African Crude Oil Pipeline – EACOP); ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani na ujenzi wa miundombinu ya hifadhi ya kimkakati ya mafuta.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia PURA inatarajia kuendesha Duru ya Tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa lengo la kutangaza kwa wawekezaji vitalu vilivyo wazi katika eneo la bahari na nchi kavu. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni zitakazoongoza mnada wa vitalu, kufanya maonesho ya kitaalamu kuhusu vivutio vya vitalu na kuzindua Duru ya Tano (5) ya kunadi vitalu. Aidha, EWURA itaendelea kusimamia udhibiti wa huduma za nishati nchini kwa kuwasimamia watoa huduma kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora na uhakika.
C. USHIRIKIANO WA KIKANDA NA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa majukumu yake, Wizara ya Nishati inashirikiana na Washirika mbalimbali wa Maendeleo, Jumuiya za Kikanda, nchi wahisani na wadau wengine. Kwa niaba ya Serikali, napenda kuwashukuru Washirika wa Maendeleo, Jumuiya na nchi wahisani ambao wameendelea kushiriki katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara na maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa ujumla. Napenda kutambua mchango wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB); Benki ya Dunia (WB); Arab Bank for Economic Development in Africa (BADEA); Mfuko wa Uendelezaji wa Economic Development Cooperation Fund (EDCF - Korea); Jotoardhi (Geothermal Risk Mitigation Facility - GRMF) pamoja na Taasisi na Mashirika ya JICA (Japan), KfW (Germany), AFD (Ufaransa); Shirika la Fedha Duniani (IMF); Sida (Sweden), NORAD (Norway); Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Mitaji ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCDF), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA) na USAID (Marekani); OPEC Fund for International Development; Abu - Dhabi Fund for Development (ADFD); na Saudi Fund for Developmnet (SFD).
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kutoa shukrani kwa Serikali za Afrika Kusini, Algeria, Burundi, Canada, China, DRC Congo, Ethiopia, Falme za Kiarabu, Iceland, India, Japan, Kenya, Korea ya Kusini, Malawi, Marekani, Misri, Morocco, Msumbiji, Namibia, Norway, Rwanda, Sweden, Ufaransa, Uganda, Uingereza, Ujerumani, Zambia, na nchi nyingine kwa ushirikiano wao katika kuendeleza Sekta ya Nishati. Nazishukuru pia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) kwa ushirikiano katika masuala ya kikanda yanayohusu Sekta ya Nishati.
D. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa nishati katika kuchochea na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu, katika mwaka 2024/25 Wizara ya Nishati itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia, kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Nishati, kwa lengo la kuhakikisha Sekta hii inachangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa letu na watu wake kama inavyotarajiwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia mijini na vijijini ili kulinda afya za wananchi na mazingira. Aidha, Wizara itaendelea kuipatia suluhu ya kudumu changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, kuimarisha usambazaji wa nishati hiyo pamoja na kuimarisha uzalishaji wa gesi asilia unaoendana na mahitaji, kwa kuzingatia kiwango cha ugunduzi wa nishati hiyo hadi sasa nchini na hatua za utafutaji zinazoendelea kuchukuliwa. Wizara pia itaendelea kuelekeza nguvu katika kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi zake.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Nane Themanini na Tatu, Milioni Mia Saba Hamsini na Tisa, Mia Nne Hamsini na Tano Elfu (Shilingi 1,883,759,455,000) kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake. Mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:
(i) Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Saba Tisini na Nne, Milioni Mia Nane Sitini na Sita, Mia Nane Thelathini na Mbili Elfu (Shilingi 1,794,866,832,000) sawa na asilimia 95.28 ya Bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Tano Thelathini na Sita na Milioni Ishirini, Mia Mbili Sabini na Nne Elfu (Shilingi 1,536,020,274,000) ni fedha za ndani na Shilingi Bilioni Mia Mbili Hamsini na Nane, Milioni Mia Nane Arobaini na Sita, Mia Tano Hamsini na Nane Elfu (Shilingi 258,846,558,000) ni fedha za nje; na
(ii) Shilingi Bilioni Themanini na Nane, Milioni Mia Nane Tisini na Mbili, Mia Sita Ishirini na Tatu Elfu (Shilingi 88,892,623,000) sawa na asilimia 4.72 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni Sitini na Tisa, Milioni Mia Tano Ishirini na Nne, Mia Mbili na Moja Elfu (Shilingi 69,524,201,000) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) na Shilingi Bilioni Kumi na Tisa, Milioni Mia Tatu Sitini na Nane, Mia Nne Ishirini na Mbili Elfu (Shilingi 19,368,422,000) ni kwa ajili ya Mishahara (PE) ya Watumishi wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukrani zangu za dhati kwako na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.nishati.go.tz. Vilevile, Hotuba hii ina vielelezo mbalimbali ambavyo vimeambatishwa kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala muhimu yanayohusu Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
0 Comments