NA MWANDISHI WETU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia SuLuhu Hassani jana Mei 8,2024 amezindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umelenga kutunza mazingira sanjari na kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na hewa chafu ya mkaa na kuni.
Katika uzinduzi huo Rais Dkt.Samia ameitaka Wizara ya Nishati kukaa na wadau ili kubaini maeneo ambayo yakifanyiwa maboresho yatasaidia upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi huo uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amesema kuwa asilimia 90 ya watanzania bado wanatumia Nishati ambayo sio rafiki, huku akisisitiza umuhimu wa kusimamia utekelezaji wa mkakati huo ili kufikia malengo ya asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi hadi kufikia mwaka 2030.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka kuleta teknolojia rahisi itakayowezesha wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao pamoja na kulipia kulingana na matumizi kama inavyofanyika katika umeme.
Rais Samia amesema lengo la Mkakati huo likitekelezwa na kutimia litapunguza gharama ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuongeza upatikanaji na uwekezaji wa nishati safi.
Rais Samia amebainisha kuwa Mkakati huo wa kitaifa pia utachangia jitihada za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa misitu ambao huchangiwa na shughuli za kibinadamu.
Amesema kuwa kwa sasa, inakadiriwa kuwa takribani hekta 469,000 za misitu hupotea kila mwaka ambapo nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha kutoweka kwa misitu hiyo.
Akisoma taarifa ya Makakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amesema kuwa mradi huo utagharimu shilling trilioni 4.6 ambao utadumu kwa muda wa miaka 10 mpaka 2034, huku akifafanua kuwa umefata sera za Kitaifa na Kimataifa ili kuleta tija.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa lengo la mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2030 asilimia 80 ya watanzania wanatumia Nishati Safi pamoja na kusimamia kikamilifu Mkakati huo ili kuleta matokeo ya haraka na kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi.
Kwa épande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo, amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabia nchi.
0 Comments