Ticker

7/recent/ticker-posts

TANROADS: RAIS SAMIA ANAZIDI KUUFUNGUA MKOA WA MOROGORO

Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogroro Mhandisi Razack Kyamba

 NA VICTOR MAKINDA-AFRINEWSSWAHILI- MOROGORO

Wakati tukiwa ndani ya maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani ya  Rais , Wakala wa Barabara             Tanzania (TANROADS), mkoa wa Morogoro, umefanikiwa kutekeleza miradi miwili mikubwa ya ujenzi wa barabara za lami na kusaini mikataba mipya minne.

Akizungumzia mafanikio ya TANROADS mkoa wa Morogoro kwa kipindi cha miaka mitatu ya  Rais Samia, Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogroro Mhandisi Razack Kyamba anasema kuwa Rais Samia ameonesha dhamira ya dhati kuhakikisha tatizo la miundombinu ya barabara mkoani Morogoro linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

 Mhandisi Kyamba, anasema kuwa  ipo miradi ya ujenzi wa barabara ambayo tayari imekamilika huku  TANROADS ikiwa imesaini mikataba mingine mikubwa ya ujenzi wa barabara muhimu  zinazounganisha wilaya za mkoa wa Morogoro ambapo kukamilika kwake kutachochea kasi ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.

“ Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, TANROADS Morogoro imetekeleza mradi wa barabara ya lami kutoka Rudewa mpaka Kilosa mjini barabara yenye urefu wa Kilometa 24  na madaraja matatu ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 32.9 zimetumika, mradi huo tayari umekamilika” Anasema Mhandisi Kyamba.

  Mhandisi Kyamba anautaja mradi  mwingine unaotekelezwa na TANROADS mkoa wa Morogoro kuwa ni mradi wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa Kilometa 66.9 kutoka Kidatu mpaka Ifakara wilayani Kilombero uliogharimu Shilingi Bilioni 104. 

Anasema kuwa mradi huo upo kwenye hatua za mwisho kukamilikaa ambapo kukamilika kwake kutakuwa chachu kubwa ya kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya ya Kilombero inayokaliwa na wakazi wengi ambao ni  wakulima wazalishaji wakubwa wa zao la mpunga, miwa na mazao mengine ya biashara na chakula.

 Anaongeza kuwa mradi wa barabara ya Kidatu Ifakara una umuhimu mkubwa katika kukuza shughuli za utalii kwa kuwa barabara hiyo inapita pembezoni mwa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa.

Barbara ya Kidatu -Ifakara

 MIKATABA YA MIRADI YA UJENZI WA BARABARA ILIYOSAINIWA

Mhandisi  Kyamba anasema kuwa katika mwaka huu wa fedha, TANROADS mkoa wa Morogoro imesaini mikataba mipya minne ya ujenzi wa barabara za lami ambazo  ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa watu wa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.

“ Tumekwisha saini mkataba ya ujenzi wa barabara ya kutoka Ifakara kwenda Mbingu, wilayani Kilombero barabara  yenye urefu wa Kilometa 62.5  tayari mkandarasi   HEGO amekwisha anza kazi. 

Sambamba na ujenzi wa barabara hiyo hiyo kutoka Mbingu kwenda Chita Kilometa 37.5 ambapo pia mkataba umekwisha sainiwa.” Anasema Mhandisi Kyamba.

 Anautaja  mkataba mwingine wa ujenzi wa barabara uliokwisha sainiwa ni barabara ya kutoka Bigwa mpaka  Kisaki kilometa 78 Wilaya ya Morogoro.

“Upo mkataba mwingine wa ujezi wa barabara ya kutoka Ubena Zomozi kwenda Ngerengere Kilometa 10 ambao tayari umesainiwa na mkandarasi anatarajia kuanza kazi hivi karibuni.” 

Mhandisi Kyamba anasema kuwa  sambamba na ujenzi wa barabara hizo za lami TANROADS Morogoro  inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa  madaraja korofi ambayo hufurika maji wakati wa masika na kupelekea wananchi kushindwa kuvuka ambayo ni daraja la Nguyani na Chakwale yaliyopo wilayani Gairo.

 Anasema kuwa Rais Samia amekwisha ridhia ujenzi wa madaraja hayo muhimu na tayari kibali cha ujenzi kimetoka, zabuni za ujenzi huo itatangazwa hivi karibuni na atakapo patikana mkandarasi ujenzi utaanza mara moja.

UJENZI WA BARABRA KUINGIA STESHENI YA TRENI YA RELI YA MWENDOKASI

Injinia Kyamba anasema kuwa TANROADS mkoa wa Morogoro illipokea maelekezo ya serikali ya kujenga  barabra za kuingia kwenye kituo cha treni ya Mwendokasi (SGR) mkoa wa Morogoro.

 Katika kutekeleza agizo hilo wakala huo upo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba kwa kuwa zabuni za ujenzi wa barabara za lami kuingia stesheni hiyo zilikwisha tangazwa.

“ Ujenzi wa barabara ya kuingia stesheni ya treni ya mwendokasi mkoa wa Morogoro yenye jumla ya Kilometa 13 unatarajiwa kuanza hivi karibuni tukitarajia kuwa ujenzi huo utarahisisha abiria  na mizigo kuingia na kutoka stesheni hapo “. Anasema Mhandisi Kyamba.

Mhandishi Kyamba  anasema kuwa TANROADS mkoa wa Morogoro inampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake ulitukuka unaojali maslahi ya wananchi na wao TANROADS watazidi kumuunga mkono kwa kutekeleza wajibu wao kwa  weledi, bidii na maarifa.

“ Tanroads mkoa wa  Morogoro tutandelea kusimamia miradi yote ya ujenzi wa barabara na tuko tayari wakati wote kupokea maagizo ya serikali na kuyatekeleza kwa viwango stahiki ili kwa pamoja tuendelee kuiunga mkono dhamira njema ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi”. Anasema Injinia Razack Kyamba. 

 

Post a Comment

0 Comments