Ticker

7/recent/ticker-posts

KUFUNGWA KWA NJIA YA KWENDA KWENYE MGODI WA BILIONEA LAIZER WACHIMBAJI 580 WAKOSA KAZI

Bilionea Laizer akiwa ameshikilia madini ya Tanzanite aliyoyachimba mgodini kwake mwaka 2020.

*Amuomba Rais Samia amsaidie, wachimbaji wenzake wamenyan’ganywa njia ya mgodi uliovunja rekodi Mererani kwa kutoa madini makubwa ,wachimbaji wake 580 wakosa ajira

 NA MWANDISHI WETU-AFRINEWSSWAHILI-MARERANI

 

Rais Samia Suluhu Hassan ameombwa kuingilia kati, mgogoro wa kufungwa njia ya mgodi wa bilionea Saniniu Laizer ambao  mwaka 2020 ulivunja rekodi ya kutoa madini makubwa zaidi ya Tanzanite tangu kugunduliwa madini hayo miaka zaidi ya 50 iliyopita .

 

Kutokana na kufungwa njia ya mgodi huo, tangu Desemba 10, 2023 uliosajiliwa  ML 543/2015 vijana 580 waliokuwa wanafanyakazi wamekosa ajira huku, pia serikali ikipoteza mapato ikiwepo kodi zaidi ya millioni 500 hadi sasa.

 

 Juni 23 mwaka 2020 Laizer alitangazwa kuvunja rekodi ya upatikanaji madini Mererani, baada ya kupata mawe ya madini makubwa moja likiwa na kilo 9.27 na jingine kilo 5.103 ambayo yalinunuliwa na serikali kwa zaidi y ash 7.8 bilioni.

 

Mchimbaji huyo, baadae alipata jiwe jingine  lenye uzito wa kilo6.33  na kuiuzia serikali kiasi cha sh 4.86 bilioni na katika mauzo ya madini hayo makubwa,  serikali iliweza kupata kodi na malipo mengine zaidi y ash 800 milioni.

 

Hata hivyo, tangu kupatikana madini hayo, mchimbaji huyo, alikuwa akifatiliwa na wachimbaji wengine na kutafuta njia ambayo ametumia kufikia madini hayo, lakini hata hivyo wamekuwa wakikwama kwani amechimba Zaidi ya kilomita 1.5 kufuata mikondo ya madini  na sasa  waendeshaji wa mgodi wa Kitalu C wamevamia na “kuteka” njia ya mgodi huo na kudai ipo katika eneo lao.

 

Bilionea Laizer akizungumzia kupokonywa njia ya mgodi wake, alisema bado anaimani kubwa  na serikali itamtendea haki kwani ametumia mabilioni ya fedha kuchimba madini katika njia hiyo na amekuwa akishirikiana na serikali kwa miaka yake yote ya uchimbaji wake.

 

“Mimi napenda haki, tangu nimeanza kuchimba nimekuwa na serikali na maafisa wa madini wanajua  njia hii ambayo nachimba miaka yote ,hawajawahi kusema nivunja sheria. Kwani tumekuwa nao, kodi nimekuwa naongoza kwa kulipa na kusaidia jamii hadi kujenga shule sasa ambacho kimetokea namshitakia Mungu lakini najua haki yangu ipo siku itapatikana”alisema

 

 Meneja msaidizi wa mgodi huo, Paulo Jacob alisema njia muhimu ya mgodi huo, ambao ulikuwa unazalisha imefungwa na  kampuni ya Franone Minning and Gems  Ltd, ambayo imekodishwa na serikali kuendesha eneo la kitalu C.

 

Jocob alisema wameshangazwa na kufungwa njia ya mgodi huo, ambao ulikuwa umbali za zaidi ya mita 700 chini ya ardhi,kwani hawajawahi kutobozana na mgodi wa KItalu C  na hawajawahi kuna na mgogoro kwa miaka zaidi ya mitano.

 

“Sisi tumeanza kuchimba muda mrefu, lakini ilikuwa jumapili usiku desemba 10 mwaka jana, wachimbaji wa Franone walivamia mgodi wetu, baada ya kupitia katika mgodi ya  Tanzanite Explores Ltd ambao tunapakana nao”alisema

 

Alisema baada ya kuvamia mgodi huo, waliziba njia na wamezua vifaa vyao vya kazi na mashine zote, vifaa ambavyo ni mashine za kuingiza hewa mgodini( moter 6, Gear box 6, blower,Diggers,mfumo wa waya za umeme, nyundo, tindo na vingine kadhaa vikiwa na thamani ya Zaidi y ash 500 milioni.

 

Alisema licha ya kuandika barua za malalamiko, ofisi za madini hadi wizara ya madini bila majibu na  Februari 29 mwaka huu, walituma barua nyingine kwa Afisa madini mkazi Mererani, Nchagwa Marwa kutaka kupatikana suluhu ya mgogoro huo hawajawahi kuhojiwa wala kupewa majibu yoyote.

 

“Hawataki kujibu barua na wanatujibu kwa maneno tukae kumalizana na Franone sasa imekuwa ngumu kupata suluhu ya mgogoro huu”alisema

 

Mwenyekiti mtahafu wa chama cha wachimbaji madini Mererani, Jeremiah Sumari alisema anaomba serikali kutenda haki katika mgogoro huo na kujali maisha ya maelfu ya wakazi wa Mererani ambao sasa wanataabika kutokana na kukosa kazi ya kuchimba madini.



AFISA MADINI MERERANI AKWEPA KUTOA MAJIBU

 

Afisa Madini mkazi Mirerani, Nchagwa Marwa alikiri  kupokea  barua ya malalamiko ya Bilionea Saniniu Laizer lakini hata hivyo,alisema suala hilo linashughulikiwa na Katibu wa Tume ya Madini.

 

“Mimi sio msemaji wa jambo hili, naomba mumtafute Katibu Tume ya Madini ndio anaweza kuzungumzia ”alisema

 

Kwa upande wake,Mmiliki wa kampuni ya Franone Onesmo Mbise, amekuwa akiwatuhumu  wachimbaji  wadogo  wanachimba eneo lake la Kitalu C.

 

WACHIMBAJI, WANAWAKE WALIA KUFUNGWA KWA MGODI


Baadhi ya  Wachimbaji wadogo na Wakazi wa Mererani, wameomba Rais kuingilia kati kutatua mgogoro huo, kwani sasa mji wa Mererani, unakufa kutokana na vijana Zaidi ya 1000 kukosa ajira, kukosekana fedha  na hivyo wizi kuibuka.

 

Wakazi wa Mererani  Zaituni Said alisema wanawake na vijana wamekuwa waathirika wakubwa baada ya kufungwa migodi ya wachimbaji wadogo ambayo inazalisha kwa tuhuma kuwa inachimba eneo la kitalu C.

 

“Tunamuomba Mama Samia Rais wetu, aingilie kati kumaliza mgogoro huu, kwani tunajua kuna vigogo wapo nyuma ya mgogoro huu kwa maslahi yao, mji wa Mererani unakufa, wizi, umeongezeka, Wanawake wametelekezewa familia kwa sababu hakuna fedha tena:”alisema

 

Kanaeli Minja alisema kwa miaka yote mji wa Mirerani unategemea  wachimbaji wadogo lakini tangu migodi yao kufungwa kwa tuhuma za kuchimba eneo la kitalu C, maisha yamekuwa magumu sana Mererani.

 

“Tunalia na Rais kwani tunajua kuna watu wapo nyuma ya mgogoro huu, mbona hawa ambao wanabebwa hatuelezwi hata kodi ambayo wanalipa serikalini, hakuna mapato yanayojulikana, huyo Laizer ndiye dunia nzima wanajua amevunja rekodi ya kupata madini makubwa hao wanaobebwa madini yao yapo wapi”alisema

 

Alisema wanawake wa Mererani ndio waathirika wakubwa na wanajipanga kufanya maandamano ha Amani hadi mgodini ili kulia haki ipatikane kwa wachimbaji wote na wanawake na vijana wanufaike kuliko sasa mji wa Mererani umegeuka magofu, watu wanahama kutokana na hali ngumu ya maisha.

 

  Mchimbaji wa mgodi huo, Erick Sekawa kufungwa kwa njia ya mgodi huo, imeaathiri sana kwani wanashindwa kuendesha familia na wanashangazwa na ukimya wa Wizara ya madini kwani tangu tukio kutokea hadi sasa hawajawahi kwenda katika mgodi huo kupima na kujua ukweli.

 

“Tunajua ni “mchezo mchafu” lakini tunaumia sisi vijana tunashindwa kusomesha watoto, maisha yamekuwa magumu sana”alisema

 

Wachimbaji Saimon Siriya na Sinyoki Laizer, waliomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo ili kuokoa maisha ya maelfu ya watu, kuliko kutetea mgodi mmoja ambao haunufaishi wananchi wengi.

 

“Tunaomba Serikali ije kukaa na wachimbaji wadogo, kutatua migogoro Mererani imekuwa shamba la bibi sisi, wakazi wa Mererani hatunufaiki na madini kwa sasa”alisema.

Post a Comment

0 Comments