NA MWANDISHI WETU-AFRINEWSSWAHILI-DSM
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanikiwa kuwaua mamba watatu na boko wawili waliokuwa hatarishi kwa maisha ya watu na mali zao ndani ya Bwawa la Mtera linalohusisha mkoa wa Iringa na Dodoma.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo mamba na boko kujeruhi na wakati mwengine kusababisha vifo kwa wananchi hususan wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Bwawa la Mtera.
Hali hiyo inatajwa na TAWA kuibua hofu na adha kwa wananchi wanaotegemea bwawa hilo kwa shughuli zao za kijamii na za uzalishaji mali.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAWA iliyotolewa leo Aprili 2,2023 na kusainiwa na Afisa Habari Kitengo cha Uhusiano kwa Umma, Beatus Maganja, ongezeko hilo la mamba na boko, limetokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hali inayosababisha mtawanyiko wa wanyamapori kwenye maeneo ya mito na mabwawa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamba wanaoongezeka kwenye bwawa la Mtera wanatoka katika mto Ruaha Mkuu na Kizigo.
Aidha TAWA imetoa elimu ya kukabiliana na wanyama hao kwa wananchi 271 wakiwemo wavuvi 40 katika vijiji vilivyopo Kata ya Migoli.
Pia TAWA imeanzisha kituo cha kudumu cha kudumu cha Askari katika Kijiji cha Migili,kituo hicho kina jumla ya watumishi 20 na kimepatiwa vitendea kazi muhimu kwa ajili ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.
Pamoja na mambo mengine TAWA imewataka wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida isipokuwa wachukue tahadhari wanapokuwa kwenye mabwawa, mito, na madimbwi.
Aidha wanatakiwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa uhifadhi ikiwemo kuacha kuogoa au kufua ndani ya bwawa na wavuvi kuacha kutumia mitumbwi hatarishi inayoongeza uwezekano wa kushambuliwa na mamba au book na badala yake watumie nyenzo za kisasa katika shughuli za uvuvi na endapo itabainika uwepo wa wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo mamba na boko taarifa itolewe haraka kwa wataalam wa uhifadhi au serikali za vijiji ili hatua stahiki zichukuliwe.
0 Comments