Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda amesema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameahidi kumjengea nyumba mama yake mtoto Alhaji Yahaya ambaye ni Mjane aliyepo mkoani Kigoma. Makonda amebainisha hayo ikiwa ni siku moja baada ya kupokea changamoto ya kijana Alhaji Yahya Abdallah ambaye anafanya biashara ya kuuza ndizi ili kumsaidia mama yake na wadogo zake wanne.
Aidha awali Makonda alimuahidi mtoto huyo kumsomesha na kumpatia kiasi cha Fedha kwaajili ya vitendea kazi na sare za shuleni ili aanza masomo, huku akisema Rais pia ameahidi kumsaidi mtoto huyo pamoja na mama yake.
"Leo 4 Februari, 2024 Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kuguswa zaidi na jambo hilo na kumsaidia mwanamama huyo mjane kwa kumpatia kiwanja na kumjengea nyumba ya kuishi na watoto wake na shughuli za ujenzi zitaanza Februari 9,2024."
Makonda amesema pia Rais Samia amempatia mwanamama huyo kiasi cha shilingi Milioni tano itakayokuwa inatolewa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kigoma Mjini kwaajili ya kufanya shughuli zake za biashara kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwasomesha watoto wote watano wa Mama huyo.
0 Comments