Ticker

7/recent/ticker-posts

HAYATI RAIS GEINGOB ALIUPINGA UKOLONI BILA WOGA NI MSHIRIKA MKUBWA WA SAM NUJOMA

 Leo Taifa la Namibia, Afrika na dunia kwa ujumla imeingia kwenye simanzi baada ya kumpoteza Rais wan chi hiyo, Hage Gottfried Geingob aliyefariki dunia asubuhi ya leo kwenye moja ya Hospitali zilizopo jijini, Windhoek alikokuwa akipatiwa matibabu ya saratani.

 

Taarifa za kifo cha Mwanamajumui huyo zilitolewa mapema leo asubuhi na Makamu wa Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba ambaye sasa ndie atakalia kiti cha urais hadi utakapokamiliki uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Novemba mwaka huu.

 

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alikuwa akiugua saratani na yeye mwenyewe aliueleza umma juu ya tatizo hilo mwezi uliopita. 

Geingob ni Rais wa tatu wa nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1990 kutoka kwa wakoloni, akitanguliwa na Rais wa kwanza wa Namibia huru Sam Nujoma ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 15, kuanzia Machi 21,1990-Machi 21,2005.

 

Hifikepunye Pohamba ni Rais wa pili wa Namibia ambaye aliingoza nchi hiyo kwa awamu mbili kutoka Machi 21,2005-Machi 21,2015 wote wakiwa chini ya chama cha siasa cha SWAPO.

 

Geingob ni mmoja wa wafuasi na washirika wa karibu wa Nujoma ambaye anatambulika kama Baba wa Taifa la Namibia.

 

Ikumbukwe kuwa historia ya Namibia inahusu zaidi eneo la Kusini mwa Afrika ambalo wakazi wake ndio wanaunda Jamhuri ya Namibia, lakini haiwezi kukamilika bila ya kuhusishwa moja kwa moja kwa Nujoma. 

 


 

Nujoma na Geingob wanatajwa kuwa ni sehemu ya watu waliotoka kwenye kizazi cha wakazi wa kwanza wa eneo hilo ambao ni wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi ambao walishika utawala na hatimaye kuwa wengi kuliko wenyeji wanaodaiwa kuwa walikuwa ni wawindaji. 

 

Historia ya Hayati Geingob inakwenda sambamba na hekaheka na mateso waliyoyapata Wanamibia kutoka kwa wakoloni.

Kimsingi Namibia ya sasa ilianzishwa katika karne ya 19 kama koloni la Ujerumani kwa jina la Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani. 

 

Maeneo yake yaliunganishwa mara ya kwanza kwenye mwaka 1884, wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilivamiwa na Uingereza na Afrika Kusini. 

 

Pamoja na makoloni mengine ya Ujerumani iliwekwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa,  tangu mwaka 1919 ilikuwa eneo la kudhaminiwa kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa chini ya serikali ya Afrika Kusini. 

 

Afrika ya Kusini-Magharibi (kwa Kiingereza South-West Africa) ilikuwa jina la eneo hilo kuanzia mwaka 1922 hadi nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1990.

 

 

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wakati wa kuvunjwa kwa Shirikisho la Mataifa mwaka 1946, Umoja wa Mataifa ulichukua jukumu la kuratibu maeneo ya kudhaminiwa. 

 

Afrika Kusini haikutambua badiliko hilo ikatangaza ya kwamba hali ya udhamini ilikuwa ya Afrika ya Kusini-Magharibi tangu kuvunjwa kwa Shirikisho la Mataifa. 

 

Mwaka 1949 Bunge la Afrika Kusini lilitangaza sheria ya kufanya eneo hilo kuwa jimbo la tano la Afrika Kusini na kueneza siasa ya Apartheid (ubaguzi wa rangi) na ilipambana kulifanya eneo hilo kuwa sehemu kamili ya Afrika Kusini. 

 

 

Hata hivyo uamuzi huo haukukubaliwa na Umoja wa Mataifa na nchi nyingi duniani, baadaye mfumo wa Bantustans wa Afrika Kusini ulianzishwa pia huko ambako maeneo makubwa yenye rutuba yalitengwa kwa ajili ya Wazungu ilhali Waafrika walitakiwa kuwa na maeneo machache  ya makazi, katika maeneo mengine waliruhusiwa kukaa kama wafanyakazi kwa muda tu. 

 

Mfumo huo wa kibaguzi haukutekelezwa kwa ukali, tofauti na ilivyokuwa ndani ya Afrika Kusini yenyewe. 

 

Umoja wa Mataifa ulioendelea kudai ya kwamba Afrika Kusini ilipaswa kuachia eneo hilo kuwa huru,  mwaka 1966 Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa  uliamua kuondoa mamlaka ya Afrika Kusini na kuweka eneo moja kwa moja chini ya Umoja wa Mataifa. 

 

Hata hivyo azimio hilo halikuweza kutekelezwa kwa sababu Afrika Kusini ilikataa,  hapo ndipo harakati za eneo hilo kujikomboa ziliposhika kasi, ambapo wanamgambo wa chama cha SWAPO walichukua silaha wakajaribu kupigania uhuru wao. 

 

Azimio la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa  la mwaka 1968 lilibadilisha jina la eneo hilo kutoka lile la awali na kuwa Namibia. 

 

Mwaka 1971 Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikaamua ya kwamba utawala wa Afrika Kusini si wa haki. 

 

Mwaka 1978 Umoja wa Mataifa uliamua ya kwamba Afrika ya Kusini-Magharibi inapaswa kupewa uhuru wake, hapo serikali ya Afrika Kusini ikaanza kuchukua hatua za kuandaa uhuru wa eneo hili, hata hivyo vita kati ya jeshi lake, SWAPO na wanajeshi wa Angola na Kuba iliendelea. 

 

Baada ya miaka ya vita vya kupigania uhuru, mchakato wa kimataifa wa kuelekea uhuru ulianza na kufikia mapatano ya kuacha mapigano mwaka 1988. 

 

Hatimaye mwaka 1990 nchi ilipata uhuru wake kwa jina la Namibia na Samuel Shafiishuna Daniel Nujoma aliyezaliwa Mei 12,1929 kwenye mji wa Etunda, katika eneo la Owamboland, wakati huo chini ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani alikabidhiwa nchi.

 

 

Nujoma ni mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi na mwanasiasa ambaye aliiongoza Namibia kwa mihula mitatu akiwa ndie  Rais wa kwanza wa eneo huru  baada ya kupata uhuru kutoka kwa utawala wa ukoloni wa Afrika Kusini. 

 

Nujoma alipata elimu ya kisiasa kwa msaada wa Umoja wa Kisovyeti na ndiyo maana alikuja na nadharia za kisoshalisti. 

 

Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, Nujoma alihamia mji wa Windhoek, mji mkuu wa Namibia, na alianza kufanya kazi za vibarua.

 

Hii ilimpa fursa ya kukutana na wafanyakazi wenzake na viongozi wa kisiasa ambao walimhamasisha kujihusisha zaidi katika harakati za ukombozi. 

 

Katika miaka ya 1950, Nujoma alijiunga na vikundi vya vijana wa Namibia (OYGN) na kushiriki katika shughuli za kisiasa na maandamano ya kupinga utawala wa kikoloni wa Afrika Kusini. 

 

Ndie mwanachama mwanzilishi wa Shirika la Watu wa Namibia (SWANU) mwaka 1959, chama cha kwanza cha kitaifa cha kisiasa kilichotetea uhuru wa Namibia. 

 

Nujoma alikuwa mwanachama mwanzilishi na rais wa kwanza wa Jumuiya ya Watu Kusini Magharibi mwa Afrika Kusini (SWAPO) mnamo 1960, ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Shirika la Watu wa Ovambo (OPO). 

 

Nujoma aliongoza SWAPO wakati wa vita vya Uhuru vya Namibia, ambavyo vilidumu kutoka mwaka 1966 hadi 1989,alianzisha Jeshi la Watu wa Ukombozi wa Namibia (PLAN) mwaka1962 akazindua vita dhidi ya serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini Agosti 1966 huko Omungulugwombashe, baada ya Umoja wa Mataifa kuondoa agizo la Afrika Kusini kudhibiti eneo hilo. 

 

Kupitia uongozi wake, SWAPO iliendeleza vita vya msituni dhidi ya utawala wa kikoloni wa Afrika Kusini na ulifanya jitihada za kidiplomasia kupata uhuru kwa Namibia. 

 

Katika miaka ya 1960, Nujoma alisafiri kwenda mataifa ya Ulaya, Afrika, na Mashariki ya Kati, akiongoza harakati za ukombozi za Namibia. 

 

Mwaka 1990, Namibia ilipata uhuru wake kufuatia mazungumzo ya amani na serikali ya Afrika Kusini na uchaguzi wa kidemokrasia ulifanyika na kumuingiza madarakani Nujoma, hata hivyo zipo nchi kadhaa ikiwemo Tanzania zilizoisaidia kwa kiasi kikubwa Namibia kupata uhuru wake.


Nujoma, Pohamba na hata Geingob ni miongoni mwa watu waliokuwa wakiitumia Tanzania kama sehemu yao ya kujiandaa na mapambano. Mathalani Pohamba, Kaukungwa na Moses Tjitendero ni baadhi ya askari wa SWAPO waliopatiwa mafunzo ya kijeshi, jijini Dar es Salaam.


Nujoma binafsi aliwahi kuokolewa na baadhi ya maofisa wa juu wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) baada ya kushtukia mpango wa kutaka kukamatwa na maofisa wa utawala wa kikoloni wa Uingereza. Nujoma aliushtukia mpango huo, ambapo alikimbilia Mbeya akitokea Ndola nchini Zambia, maofisa wa TANU walimsaidia kumtorosha hospitalini akipitia Njombe, Iringa, Dodoma hadi Dar es Salaam.


Kwa msaada wa maofisa wa TANU, Nujoma aliweza kuonana na Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Rais wa TANU na alimsaidia kupata hati ya kusafiria ya Tanzania ili we rahisi kwake kuendeleza harakati zake za ukombozi kwa kusafiri bila kikwazo.


Mbali ya kupatiwa hate ya kusafiria, pia Mwalimu Nyerere aliridhia mji wa Dar es Salaam utumiwe na Nujoma na wenzake kama kituo kikuu cha kijeshi cha wanamgambo wa SWAPO nje ya Namibia kwa jailli ya kutoa mafunzo ya kijeshi, pia  Nujoma aliitumia Tanzania kupitisha silaha kutoka Algeria kwa ajili ya jeshi lake.


Silaha hizo zilipitia Tanzania na kupelekwa kwenye mji wa Omugulugwombashe katika eneo la  Ovambaland nchini Namibia ilipokuwa ngome kuu ya jeshi la SWAPO. 

 

Hayati Hage Gottfried Geingob aliyezaliwa Agosti 3,1941 alilazimika kusubiri kuliongoza taifa hilo hadi  Machi 21,2015 baada ya Hefikepunye kumaliza muda wake madarakani.

 

Mbali ya kuwa Rais wa nchi pia Hayati Geingob alikuwa  Rais wa chama tawala cha SWAPO, ambapo alichaguliwa katika nafasi hiyo Novemba 2017. 

 

Kimsingi Hayati Geingob alikuwa ni mshirika wa karibu wa Rais Nujoma, kwani yeye ndie alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Namibia mara baada ya kupata viongozi huru Machi 21, 1990 hadi 28 Agosti 2002.

Pia alihudumu kama Waziri Mkuu kwa mara ya pili kutoka Desemba 4, 2012 hadi 21 Machi 2015 alipowania urais. 

 

Kati ya mwaka 2008 na 2012 Hayati Geingob aliwahi kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda. Mwaka 2015 alichaguliwa kuwa rais wa Namibia kwa kura nyingi. 

 

Novemba 2017, Hayati Geingob alikuwa Rais wa SWAPO baada ya kushinda kwa kiasi kikubwa cha kura kwenye Mkutano wa sita wa chama hicho. 

 

Agosti 2018, Hyati Rais Geingob alianza muhula wa mwaka mmoja wa kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). 

 

Alimaliza muhula wake wa kwanza wa Urais mwaka 2019, ambapo Novemba 2019 aliwania tena nafasi hiyo na kuchaguliwa kwa asilimia 56.3 ya kura zilizopigwa, kutoka asilimia 86 aliyopata katika uchaguzi wake wa kwanza.

Post a Comment

0 Comments