Ticker

7/recent/ticker-posts

DKT. KALIMANGA: KASI YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA NI KUBWA

Dkt. Elikana Kalimanga

 

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-DSM

 

Kasi ya uharibifu wa mazingira kwa kukata miti, uharibufu wa vyanzo vya maji na uzalishaji wa hewa ukaa ni kubwa ndani na nje ya Tanzania hali inayofifisha uwezekano wa kuyarejesha katika uhalisia wake wa kawaida kwa haraka kama ilivyokuwa ikifanyika miaka milioni 445 iliyopita.

 

Hayo yamesemwa na Meneja Ushirikishwaji Sekta binafsi kutoka Shirika la RTI, Dkt. Elikana Kalumanga alipokuwa akitoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari za Mazingira wanaoshiriki mradi wa USAID Tuhifadhi Mazingira yaliyoanza Alhamisi ya Februari 15-16,2024, Bagamoyo mkoani Pwani.  

 

Dkt. Kalumanga, amesema suala la uharibifu wa mazingira yaliyochangia mabadiliko ya tabia yameanza miaka milioni 445 iliyopita, hata hivyo haikuwa rahisi athari zake kuonekana kwa haraka kutokana na kasi yake kuwa ndogo.

 

Amesema nyakati hizo ilikuwa ni rahisi kwa mazingira kujirekebisha yenyewe kwa sababu shughuli za kibinadamu hazikuwa nyingi kama ilivyo sasa.

 

“Suala la uharibifu wa Mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, hayakuanza leo, yalianza miaka milioni 445 iliyopita na katika nyakati hizi yalikuwa yakichangiwa zaidi na mambo ya asili na mazingira yalikuwa yanaweza kujirejesha yenyewe katika hali yake ya kawaida.

 

“Kwa sasa hali ni tofauti, mapinduzi ya teknolojia na kuongezeka kwa shughuli za kibidanamu kumekuwa ni tatizo kubwa na kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kuyarejesha mazingira kwenye asili yake ni wazi hali itakuwa mbaya zaidi miaka ijayo” amesema Dkt, Kalimanga. 

Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Mazingira Tanzania (JET),Det. Ellen Otaru akifungua mafunzo hayo, alisema anaamini Waandishi wa Habari wanaouwezo mkubwa wa kuongeza ushawishi kwa wananchi, wadau na watoa maamuzi ili kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira na uhifadhi wa wanyama pori. 

 

Mradi wa USAID Tuhifadhi Mazingira umelenga kuujua umuhimu wa kuhifadhi mapito ya wanyamapori maarufu kama shoroba.

 

Ikumbukwe kuwa shoroba ni muhimu kwa uhai wa wanyamapori, hizo ndizo zinawasaidia kutoka eneo moja kwenda jengine kujitafutia malisho.

 

Pasipo na shoroba ni wazi idadi kubwa ya wanyamapori itatoweka duniani, ikumbukwe kuwa wanyama wanahama kutoka eneo moja kwenda jengine kwa umbali mrefu, kimsingi wanyama hawana mipaka.

 

Na maeneo pekee yanayowasaidia kujua wanakokwenda na kuweza kurudi walikotoka ni shoroba, kwenye njia zao wanajiwekea alama kadha wa kadha zinazowasaidia kutopoteza mwelekeo na ndio maana inaeleelzwa Tembo huwa hasahau mapito yake hata awe amepita kwa miaka mingi nyuma, lakini iko siku atarejea hapo.

 

Elimu iliyotolewa inalenga namna ya kupambana na Uharibifu wa Misitu, Wanyamapori. Mabadiliko ya Tabianchi na uhifadhi wa viumbe hai. 

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo (kushoto) akitoa neno kwa Waandishi wa Habari

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa Tuhifadhi Maliasili ambao unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID). 

 

Mradi unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyama na viumbe hai nchini Tanzania. 

 

“Kupitia mafunzo haya, waandishi wa habari watajazwa maarifa, ujuzi na  mtazamo sahihi wa kuripoti taarifa za uchunguzi kuhusu uhifadhi wa viumbe hai na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

 

Chikomo alisema wanahabari wanajengewa uwezo kwenye eneo la uhifadhi wa shoroba ili kujua namna ya kuchunguza, kuripoti na kuchambua uhusiano wa wanyamapori, uhifadhi wa bahari na misitu, biashara haramu na ujangili na kukuza uhifadhi wa wanyamapori na masuala ya utalii.

Washiriki wa mafunzo ya mradi wa USAID Tuhifadhi Malisili wakiwa katika picha ya pamoja, Bagamoyo, mkoani Pwani.


 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments