Ticker

7/recent/ticker-posts

MRADI WA USAID TUHIFADHI MALIASILI WACHOCHEA USAWA WA KIJINSIA





Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Doroth Nyoni akitoa mada mbele ya Waandishi wa Habari za Mazingira (Hawapo pichani) 

NA JIMMY KIANGO- AFRINEWSSWAHILI-BAGAMOYO

Kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakitengwa ama kujitenga katika kushiriki kwenye baadhi ya shughuli za kuleta maendeleo ambazo zimepewa mtizamo hasi kuwa ni za kiume.

Hali hiyo imechangia pakubwa wanawake wengi hasa waliopo kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi ama mapori ya akiba kujiona hawastahili kuwa walinzi wa maliasili hizo.

 

Dhana hiyo imechangia pakubwa akina mama kutazamwa kama ndio washiriki wakuu wa ukataji miti wenye lengo la kutafuta kuni.

 

Kwa kuliona hilo Shirika la Misaada la Marekani kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Mazingira kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya  usawa wa kijinsia kwenye usimamizi maliasili mbalimbali zikiwemo shoroba saba ambazo kwa sasa zimo ndani ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha unawaongezea uelewa wanawake katika kulinda shoroba ili ziendelee kuwa salama na kuwapa fursa wanyama kuhama kutoka eneo moja kwenda jengine kwa kupita kwenye njia zao za asili.

 

Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Doroth Nyoni ameyaeleza mafanikio hayo juzi Februari 16,2024 alipokuwa akiwasilisha mada kwa Waandishi wa Habari za Mazingira walioshiriki katika mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika, Bagamoyo mkoani Pwani.

 

Wasilisho la Doroth lililenga kwenye umuhimu wa kuzingatia jinsia kwenye utekelezaji wa miradi ambayo inahusu uhifadhi na mazingira.

 

Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Doroth Nyoni akiwasilisha mada mbele ya Waandishi wa Habari za Mazingira

Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa katika shoroba za Kwakuchinja, Amani Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chato umezingatia usawa wa kijinsia ambao umesaidia makundi yote kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

 

Doroth amesema katika ufuatiliaji na tathmini ambayo wamefanya wameona ushirikishwaji wa makundi yote wakiwemo wanawake, vijana, watoto na walemavu  inasababisha rasilimali zote zinazopatikana kwenye hifadhi kuwa salama na kila mwana jamii kujiona ni mnufaika.

 

“Ili fursa zinazopatikana kwenye uhifadhi ziwe endelevu ni lazima ushirikishwaji wa kijinsia uzingatiwe, hatua hiyo inasaidia hifadhi kutunzwa na kuwa endelevu,” amesema.

 

Amesema Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umeshirikiana na wananchi waliopo karibu na shoroba ili kuhakikisha wananufaika na fursa zilizopo, ikiwemo kuanzisha vikoba, ujasiriamali na kupata tija nyengine.

 

Doroth amesema katika kusimamia misingi ya usawa wa kijinsia wamehakikisha makundi yote yanashiriki katika uongozi ili wawe sehemu ya maamuzi kuhusu rasilimali zao.

 

Taarifa za kitafiti zinaonesha wanawake na vijana ndio waathirika wakuu wa uharibifu wa mazingira, hivyo uamuzi wa kuzingatia usawa wa kijinsia utawanufaisha zaidi.

“Kampeni ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiachwa kwa kundi moja, hatari itakuwa kubwa, sisi USAID Tuhifadhi Maliasili tumehakikisha jinsia inapewa nafasi.

“Kwenye shoroba ya Amani Nilo iliyopo wilayani Muheza mkoani Tanga tumefanya kampeni kuanzia ngazi ya shule za msingi, hali ambayo imewezesha hata watoto kutambua faida za hifadhi na hivyo kulizinda. 

 

“Kwakuchinja mkoani Manyara kuna Program ya Twende Porini nayo imefanikiwa kwa kuwa imejikita kwenye suala la kijinsia,” amesema.

 

Amesema kuwa kabla mradi huo haujaanza kushirikisha makundi yote, kulikuwa na hali ya baadhi makundi kuona wanatengwa, ila kwa utaratibu wa sasa  hali imekuwa nzuri.

 

“Kwenye baadhi ya shoroba tayari watu wameshaanza kunufaika na ardhi yao. Tumezingatia misingi ya kuwezesha uhifadhi ambao wananchi wananufaika na rasilimali hiyo ya shoroba. Mfano GFP amewezesha wakulima wa viungo wilayani Muheza kunufaika.”

 

Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa Habari za Mazingira (hawapo pichani) na kushoto ni  Doroth Nyoni. 


Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema uamuzi wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kuzingatia misingi ya kijinsia unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa ndio mwelekeo wa dunia.

 

Dkt. Otaru amesema dunia kwa sasa inapigania usawa wa kijinsia, hivyo ni muhimu waandishi wa habari kueleza kwa kina kuhusu miradi ambayo inazingatia hayo.

Post a Comment

0 Comments