Afisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Reuben Magandi
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWS SWAHILI-BAGAMOYO
Kila miaka inavyosogea ndivyo binadamu wanaongezeka na kuongeza kwa kasi shughuli zao za kibinadamu ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia kuharibu mazingira.
Uharibifu huo wa Mazingira unachangia pakubwa mvurugiko wa misimu hali inayozalisha athari kadha wa kadha zikiwemo za ukame wa muda mrefu, mafuriko, vimbunga na hata matetemoko ya ardhi nchi kavu na baharini.
Athari za suala hilo zimekuwa zikionekana katika maeneo mbalimbali yanayogusa maisha ya binadamu.
Wataalamu wanaeleza kuwa mabadiliko hayo yamekuwa na visababishi vingi ikiwa ni pamoja na uvamizi wa maeneo ya misitu na mapori.
Afisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Reuben Magandi amebainisha kuwa
miongoni mwa athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ni pamoja kukosekana kwa maji kunakochangiwa na kuharibiwa kwa vyanzo vya maji.
Magandi ameyasema hayo Februari 15, 2024 katika semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari za Mazingira iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Vitendo vya wananchi kuvamia maeneo ya misitu kwa shughughuli za kilimo, ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, mbao na uchomaji wa mkaa imekuwa ni changamoto kubwa inayorudisha nyuma juhudi za TFS na chanzo cha hayo yote ni kukosekana kwa vyanzo halali vya kujipatia kipato.
Moja ya maeneo ya msitu yaliyoharibiwa |
“Kitendo cha wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi za misitu na kufanya shughuli za uchomaji mkaa, upasuaji mbao na nyingine kinachangiwa na umasikini, watu hawana vyanzo sahihi vya mapato,” amesema Magandi.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo TFS wamekuwa wakiishirikisha jamii zinazozunguka misitu kupata njia mbadala za kujipatia kipato halali bila kuathiri misitu.
“Tumekuwa tukigawa miche ya miti ikiwamo ya matunda kwa jamii zote zinazozunguka misitu asili kwa vikundi, taasisi na mtu mmoja mmoja.
“Tunawapa mizinga ya ufugaji nyuki, haya yote tunayafanya kwa lengo la kuwaondoa kwenye fikra za kuvamia misitu na kufanya shughuli za uharibifu.”
Kuhuhusu miti ya asili yenye hatari ya kutoweka, alisema TFS inapambana kuhakikisha inaendelea kuwepo ingawa ipo changamoto ndogo inayochangiwa na wakataji wa miti kwa ajili ya mkaa.
“Suala la uvunaji wa mkaa ni changamoto, hata hivyo TFS kwa kushirikiana na wananchi tunapambana kukabiliana na changamoto,” anasema.
Athari za Mabadiliko tabia nchi zinagusa kila kiumbe hao na kwamba kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kukabiliana nazo, iko siku baadhi ya mimea, wanyama na viumbe hao wengine vitatoweka.
Hayo yamethibitishwa na Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dkt. Elikana Kalumanga.
Dkt. Kalumanga amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinagusa kila eneo na mbinu za kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na kuhifadhi shoroba ili kuruhusu wanyama kuendelea kutafuta malisho na maji bila kikwazo.
Mkurugenzi wa JET, John Chikomo akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari za Mazingira (hawapo pichani) |
Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amebainisha kuwa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ni wa miaka mitano na unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyama na viumbe hai nchini Tanzania.
“Kupitia mafunzo haya, waandishi wa habari wanapata maarifa, ujuzi na mtazamo chanya wa kuripoti taarifa za uchunguzi kuhusu uhifadhi wa viumbe hai na mabadiliko ya tabianchi kwa usahihi zaidi.
“Hivyo, JET kwa kushirikiana na wadau wengine jukumu letu ni kuwajengea uwezo wanahabari katika eneo la uhifadhi wa shoroba ili kujua namna ya kuchunguza, kuripoti na kuchambua uhusiano wa wanyamapori, uhifadhi wa bahari na misitu, biashara haramu na ujangili sanjari na kukuza uhifadhi wa wanyamapori na masuala ya utalii,” amesema Chikomo.
0 Comments