Ticker

7/recent/ticker-posts

ASKOFU KKKT AKEMEA RUSHWA YA NGONO KATIKA KUTOA AJIRA

Na. VICTOR MAKINDA:MOROGORO

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo, ameiasa jamii  kutojihusisha na rushwa ya ngono kwa lengo la kutoa upendeleo wa ajira kwani kufanya hivyo kuna madhara makubwa katika ustawi wa jamii.

Askofu Mameo aliyasema hayo Novemba 28,2023 mjini Morogoro wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano   la uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na kanisa hilo na kuwahusisha maafisa ustawi wa jamii, wanasheria na waandishi wa habari.

Askofu Mameo alisema kuwa kuna baadhi ya watu kwenye jamii ambao wanapungukiwa  maadili na hofu ya Mungu, hushawishi kupatiwa rushwa ya ngono ili waweze kutoa upendeleo kwenye ajira.

 “Kuna ugumu wa kupata ajira kwa wakati tulio nao, wasomi ni wengi na ajira ni chache. Wapo baadhi ya watu hutumia mwanya huo kushawishi kupatiwa rushwa ya ngono ili waweze kutoa upendeleo wa kuajiri”. Alisema Mameo.

Alisema kuwa tabia hiyo ni mbaya  kwa kuwa husababisha wasio na uwezo kuajiriwa na kuwaacha wenye uwezo na sifa stahiki matokeo yake kupunguza ufanisi na kuzorotesha kasi ya maendeleo.

Katika hatua nyingine Mameo aliwaasa wenye mamlaka  kuacha tabia ya kuwakandamiza, kuwanyanyasa na kuwaumiza wengine kimwili na kihisia kwani vitendo hivyo si tu ni kinyume  na  sheria na taratibu za nchi  bali pia ni kiunyume na mafundisho ya dini zote.

“Vitabu vitakatifu vinaeleza kuwa tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, hivyo ni lazima maisha yetu yaenzi kusudi la uumbaji wa Mungu la kuishi kwa upendo,  furaha na kuwa sababu ya wengine kufurahia maisha.” Alisema Mameo.


Alisema kuwa jamii ya Kitanzania na kote duniani iungane na kusema hapana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani vitendo hivyo huacha makovu makubwa yasiyofutika kwa wahanga.

Akizungumza kwenye kongamano hilo Mratibu wa Mipango wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Yona Kitua, alisema kuwa jamii iendelee kuelimishwa  kwa lengo la kubainisha vitendo vipi vinaangukia katika ukatili wa kijinsia, madhara na nini kifanyike kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia visiendelee kutokea.

“Ili jamii iwe salama pasipo vitendo vya ukatili wa kijinsia, lazima tuendelee kutoa elimu kwa mbinu mbali mbali na bila kuchoka, kwani elimu ndio njia pekee inayoweza kubadili tabia na mienendo isiyofaa  kwenye jamii.” Alisema Yona.

Afisa Ustawi wa Manispaa ya Morogoro, Fidna Mathias, alisema kuwa hakuna sababu ya jamii kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwataka watu  wote wanaofanyiwa vitendo hivyo au wanaoshudia mtu anafanyiwa  vitendo hivyo kuripoti kwenye mamlaka husika.



Post a Comment

0 Comments