Ticker

7/recent/ticker-posts

VIJANA WATAKIWA KUTUMIA FURSA YA UMEME KUFIKA VIJIJINI

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akiwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Zahanati ya Lundomato Kijiji cha Ukata Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake kikazi wilayani humo Oktoba10, 2023.

Na. Zuena Msuya na MayLoyce Mpombo-Ruvuma

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amewataka Vijana kuchangamkia fursa ya kuomba mikopo ili kuwekeza katika sekta ya Nishati inayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini(REA) kwa nchi nzima.

Mhe. Kapinga amesema hayo wakati wa semina iliyoandaliwa na REA kwa Jumuia ya Wazazi na Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma tarehe 9 Oktoba 2023.

Aliwaeleza washiriki wa semina hiyo kuwa fursa ya mikopo hiyo nafuu inalenga ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini, ambapo amewataka vijana hao na wazazi kuomba mikopo hiyo ili waweze kujenga Vituo vya Mafuta ambavyo pia vitawaongezea kipato.

Alifafanua kuwa mkopo huo unaotolewa ni wa shilingi milioni 75 ambazo zinatolewa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza na ya pili kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa kituo, na awamu ya tatu ni kwa ajili ya kuagiza mafuta na kuanza biashara, ambapo marejesho yanachukuwa muda wa miaka saba kumaliza mkopo huo

“Wazazi wangu na Vijana wenzangu nimeona nikutane na ninyi hapa ili tuunge mkono Ajenda ya Mhe. Rais ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia inayolenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na kulinda afya zetu, na kwa kutumia ajenda hii vijana watatumia fursa zinazopatikana ambazo vijana na wazazi mnaweza kuzitumia,” alisema Mhe. Kapinga.

Kwa upande wake Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA, aliyekuwa akitoa semina kwa wajumbe hao aliwaeleza kuwa fursa hiyo ni ya watanzania wote wanaoishi vijijini.

Katika hatua nyingine Mhe. Kapinga amekagua miundombinu ya usambazaji wa umeme katika vijiji vya Mtawa, Mkumbi na Kitongoji cha Magingo na pamoja na kuzungumza na wananchi ambapo pamoja na mambo mengine amewahakikishia kuwa umeme utafika katika maeneo yao na wanachotakiwa sasa ni kusuka nyaya katika nyumba zao ili umeme utakapofika waweze kuunganishwa.

 

Post a Comment

0 Comments