Ticker

7/recent/ticker-posts

MAVUNDE ASIMAMISHA LESENI ZA KAMPUNI ILIYOTOROSHA MADINI

 WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesimamisha leseni zote uchimbaji na uuzaji madini  za Kampuni ya Nadoyoo Mineral Trading.

Kampuni hiyo imeingia matatani baada ya kukamatwa kwa mmoja wa wahusika wa kampuni hiyo akidaiwa kutorosha dhahabu yenye uzito wa zaidi ya kilo 4.3 zikitajwa kuwa na  thamani ya zaidi ya Sh Milioni 562.3.

Mzigo huo wa dhahabu umekamatwa katika operesheni ya kushtukiza  iliyofanywa usiku  na Mavunde.

Akizungumzia tukio hilo, Mavunde amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, haitakubali kuona watu wachache wanajihusisha na vitendo hivyo viovu. 

"Tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote tutakayemkamata akijihusisha na utoroshaji wa madini.


"Nilipoingia Wizara ya Madini mwezi mmoja uliopita nilisema, ukitaka kufahamu sura yangu nyingine basi jaribu kutorosha madini.

"Kuanzia leo mtu yeyote atayekamatwa kwa kosa la kutorosha madini, tutakwenda kusimamisha leseni zake zote nchi nzima wakati tukisubiri hukumu ya vyombo vya sheria," amesema.

Amewataka wafanyabiashara wa madini kuwa wazalendo kwa kufuata taratibu zilizopo na kulipa tozo, ada na kodi mbalimbali ili kuiwezesha serikali kupata mapato na kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara, umeme, afya na elimu.


"Nipo tayari  kukaa na wafanyabiashara wa madini ili kwa pamoja wanieleze hasa ni nini wanadhani inaweza kuwa ni changamoto kubwa inayosababisha  baadhi yao kufikia hatua ya kujihusisha na vitendo vya utoroshaji madini, hatua hii itasaidia Serikali kuchukua njia sahihi kushughulikia suala hilo."

Aidha ameeleza kuwa pamoja na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watoroshaji wa madini, pia madini yote yatakayokamatwa yatahifadhiwa na serikali na kupelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kusubiri uamuzi wa mahakama.

Post a Comment

0 Comments