Ticker

7/recent/ticker-posts

WAKULIMA WATELEKEZA MASHAMBA KUKIMBIA TEMBO MWAKIJEMBE, WWF YAANDAA MPANGO WA KUSAIDIA

Tembo akiwa amevamia shamba la mkonge katika kijiji cha Mbuta

NA. JIMMY KIANGO-AFRINEWS SWAHILI-TANGA

 “HALI ya kilimo si nzuri hapa kijijini kwetu, hii inasababisha kuwa na hali mbaya ya chakula si nzuri, kuna ukame, mvua haijanyesha kwa muda mrefu sasa, tuna muomba Mungu angalau tupate mvua za kutoka mwaka huu, lakini mbaya zaidi Tembo wanatufanya tusilime kabisa,” hiyo ni kauli ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuta,  Emmanuel Simba.

Kijiji cha Mbuta kipo katika Kata ya Mwakijembe, wilayani Mkinga mkoani Tanga, moja ya changamoto kubwa zinazokikabili Kijiji hicho ni ukame na tembo ambao wamekuwa wakivamia mashamba.

 Akizungumzia suala hilo, Simba alisema ni jambo la kawaida kwa tembo kuvamia mashamba na kuharibu mazao.

 “Ni jambo la kawaida kwa tembo kuvamia kwenye mashamba yetu, na wanapovamia wanafanya uharibifu wa hali ya juu, watu wengi wameamua kutelekeza mashamba yao kwa sababu ya kuogopa tembo.

“Wanatia hasara sana, yaani mkulima anapambana kuandaa shamba, kupanda na kufanya palizi, vyote hivyo vinahitaji fedha, lakini mwisho wa siku tembo wanakuja na kuharibu mazao yote ndani ya muda mfupi, wengi wanaona ni mateso kwakweli, lakini pia ni wakali na wanaweza kuua,”alisema.

 Simba alisema madhila yanayowafika yanafahamika, lakini ni kama kumekuwa hakuna jitihada za kuwasaidia kukabiliana na tembo hao.

 Mmoja wa wafugaji wa ng’ombe kijijini humo Yahaya Fudende alisema uvamizi wa tembo hauwasumbui wakulima tu, bali hata wafugaji nao ni waathirika.

Moja ya mashamba ambayo yamevamiwa na tembo hivi karibuni
 “Tunalazimika kulisha mifugo yetu kwenye maeneo ya jirani na makazi yetu kwa sababu ya kuogopa tembo, hatuwezi kwenda mbali maana ukienda mbali ujiandae kuacha ng’ombe huko kwa sababu ya kukimbia tembo.

 “Ni wakali na wanadhuru, ukifanya uzembe pale unapokutana nao ni wazi watakudhuru,”alisema Fudende.

 Kaike Kinundu mkazi wa kitongoji cha Maya Kijiji cha Mbuta, ambaye ni mfugaji amekiri kupata usumbufu mkubwa kutoka kwa tembo.

“Ni kweli wakulima wanayakimbia mashamba yao, lakini hata sisi wafugaji nao tunakutana na wakati mgumu, ipo haja ya kusaidiwa kwenye kukabiliana na hili,”alisema Kindundu.

 Akizungumzia suala hilo Afisa Wanyamapori wa wilaya ya Mkinga, Erasto Kalisti alikiri kuwapo kwa uvamizi wa tembo kwenye Kijiji hicho na vijiji vilivyopakana na hifadhi ya Mkomazi kwa upande mmoja na hifadhi ya Tsavo iliyopo nchini Kenya.

 “Ni kweli hili suala la tembo kuvamia mashamba kwenye Kijiji cha Mbuta na vijiji vingine vilivyoakana na hifadhi ya Mkomazi lipo na nakiri linasumbua, lakini zipo jitihada zinafanyika kuhakikisha tunawarudisha kwenye maeneo yao.

 “Tumekuwa tukiwajengea uwezo wanakijiji ili kujua namna sahihi ya kukabiliana nao, na kikubwa tunachokifanya ni kuwapa mbinu za kufuga nyuki kwenye maeneo ambayo ndio mapito ya tembo.

Kundi la tembo likiwa katika maeneo ya mashamba kwenye kitongoji cha Maya wilayani Mkinga, mkoani Tanga. 
“Uwapo wa nyuki unasaidia kuwafanya tembo kutokaribia maeneo hayo, wote tunajua tembo anahitaji eneo kubwa sana la kujitafutia chakula na ndio maana wanavamia mpaka maeneo yenye mashamba.” 

Kwa upande wake mmoja wa maofisa wa WWF ambae ni msimamizi wa  Mradi wa Uongoaji wa Misitu ya Usambara Mashariki  kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Thomas Sawe, alisema moja ya mikakati yao ni kuhakikisha wanawasaidia wananchi kukabiliana na changamoto hiyo.

Sawe alisema moja ya njia ambayo wanaweza kuitumia ni kuwapanga wakulima kwenye mfumo wa mashamba ya pamoja (Block Farming), hatua ambayo itasaidia kuwa na mbinu ya pamoja ya kukabiliana na tembo.

 “Tunaamini tukifanya kilimo cha pamoja cha mashamba makubwa kitasaidia kukabiliana na tembo, maana hatua zitakazochukuliwa na wakulima zitakuwa ni za pamoja.

“Mfumo wao wa kilimo wa sasa unatoa nafasi kwa tembo kuwasumbua maana hauwezi kuleta nguvu ya pamoja ya kukabiliana na tembo au hatari yeyote itakayojitokeza kwani wako mbalimbali sana.”

Kwa upande wake Gladness Mtega ambae ni afisa wa WWF, ameliambia Afrinews Swahili kuwa wazo la kilimo cha pamoja limetolewa na kukubaliwa na wanakijiji wenyewe na WWF inaangalia namna ya kulifanikisha hilo. 



Post a Comment

0 Comments