Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Bima imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi na kusimamia soko kwenye Sekta ya Bima.
Hayo yote yatafanyika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Hayo yamebainishwa na Kamishina wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana Septemba 19,2023 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Saqware amesema mamlaka inapenda kuona soko la Bima lisilokuwa na udanganyifu, lenye ushindani, soko linalofuata weledi na faida.
"Mamlaka kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Bima itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye Sekta hiyo.
"TIRA kwa kushirikiana na wadau wa Bima inaendelea na utekelezaji wa Mipango na mikakati ya Taifa ambayo ni pamoja na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (FYDPII-2020-2025).
"Mpango Mkuu wa Taifa wa kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDMP2020-2030), Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025), Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar, Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia Bunge mwezi April2021, maelekezo ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Bima Septemba 2022 na Maelekezo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba 2022 wakati wa semina ya Elimu ya Bima na Usalama Barabarani kwa Waheshimiwa Wabunge." amesema na kuongeza kuwa.
Baadhi ya mipango ijayo ya Mamlaka ni pamoja na Kuanzisha na kutekeleza Mpango wa kitaifa wa Bima ya Kilimo
(Tanzania Agriculture Insurance Scheme); Uanzishwaji wa bodi ya wataalamu wa Bima, Hifadhi ya Jamii na Takwimu Bima; Kuunganisha mifumo ya kidigitali na Taasisi mbalimbali za umma ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, LATRA, NIDA, TASAC, TRA, PTA, ZRA.
"Lengo ni kuongeza usimamizi na maendeleo ya soko la Bima; Kuendelea na utoaji wa elimu ya bima kwa umma na wadau mbalimbali.
Kwa mfano Mamlaka imeandaa Semina ya Pili ya Makatibu Wakuu wote Nchini kwa lengo la kutoa elimu ya umuhimu wa ukataji bima. Semina imepangwa kufanyika tarehe 27 Oktoba 2023.
"Kufungua ofisi za Bima Mtawanyo za Kikanda ambazo Serikali ya Tanzania inamiliki hisa za moja kwa moja au kupitia Taasisi zake ili kampuni hizo ziweze kufungua ofisi nchini kwa utaratibu wa Mikataba ya Uenyeji (Hosting Agreements) na Kuendelea kukusanya maoni ya wananchi kwa lengo la kuhuisha Sheria ya Bima Sura 394." amesema.
Katika hatua nyingine amesema, Mamlaka inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta. Lengo ni kufikia asilimia 80%ya watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya kumi na nane(18) ifikapo mwaka 2030.
"Lengo la mkakati ni utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa Serikali, Idara, Taasisi za Umma ili ziweze kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1)hadi(3), kif.140 na Sheria ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011, kif. 4 (2) (b). Hadi mwezi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo; Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na TAMISEMI. Mkakati huu ni endelevu na utazifikia Wizara, Idara na Taasisi
mbalimbali za Umma.
"Kulinda haki za mteja wa Bima, Mamlaka imeendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki. Hadi sasa ulipaji wa madai na fidia stahiki kwa wateja wabima yamefikia asilimia 95 hivyo kupungua kwa malalamiko.
Hata hivyo asilimia 5 ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho."amesema Saqware.
Tira ni mamlaka iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bima ya mwaka 2009 Sura Na.h 394 ikiwa na majukumu ya kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima; kuandaa na kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia soko la bima na Kurekebisha Sheria, kutoa elimu ya bima kwa umma, kulinda haki za mteja wa Bima na kushauri Serikali kuhusu mambo ya Bima.
0 Comments