Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya GCA, Ban- Ki-moon
NA.JIMMY KIANGO- AFRINEWS, JET- DSM
JITIHADA za serikali ya Tanzania, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yameisukuma dunia kumteua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Kimataifa cha Uhimilivu wa mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptation -GCA).
Taarifa ya uteuzi huo iliwasilishwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki-moon ambaye ndie Mwenyekiti wa bodi hiyo.
Moon alilitekeleza hilo alipokutana na Rais Samia pembeni ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu mabadiliko ya Tabianchi, uliofanyika jijini Nairobi, nchini Kenya.
Uteuzi huo unatajwa kuwa ni heshima kubwa kwa Rais Samia na nchi kwa ujumla na umechangiwa na uongozi mahiri wa serikali ya Awamu ya Sita katika jitihada za. Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika na duniani kote ambako Tanzania ni kinara wa utekelezaji wa miradi mbambali inayogusa eneo hilo.
Rais Samia ataungana na Rais wa Jamhuri ya Senegal, Macky Sall,Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinumwi Adesina na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Fedha wa Kimatifa (IMF) Kristalina Georgieve.
GCA ni taasisi kubwa duniani inayosimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, ambapo hadi sasa imeweza kufanikisha upatikanaji wa zaidi yad ola za Marekani bilioni 50.
Tanzania ni nchi za kwanza zitakazonufaika na fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Serikali ya Tanzania chini ya ofisi ya Mkamu wa Rais (ORM) kwa kushirikiana na Shirika la umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP) imeshaanza kutekeleza mradi wa kujenga uwezo wa utayari wa nchi katika kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Mradi huo unahusisha kuandaa mpango wa Kitaifa wa kuhuisha masuala ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya nchi iliyopewa jina la National Adaptation Plan (NAP).
Tayari Serikali inaendelea kuandaa vikao vya wataalamu kwa ajili ya kupitia na kuridhia taarifa mbili za mradi huo ambazo ni Mwongozo wa kufundishia wataalamu mbalimbali nchini ili kuwajengea uelewa wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na Mkakati wa Utekelezaji wa Mradi huo (NAP Framework).
0 Comments