Mtanzania ambaye ni frateri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, Melkiori Mahinini (27) ametekwa nyara na watu wasiojulikana nchini Nigeria.
Mseminari huyo aliyepelekwa Nigeria na Shirika la Wamisionari wa Afrika kwa ajili ya mwaka wa uchungaji kabla ya kuanza masoko la teolojia, ni mzaliwa wa Parokia ya Kabanga mkoani Kigoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Joseph Mlola, mseminari huyo alikamatwa Agosti 4 mwaka huu katika jimbo la Minna huko Nigeria akiwa na mwenzake, Padri Paul Sanogo, raia wa Burkina Faso.
“Walitekwa na kundi la watu wasiojulikana mapema usiku wa kuamkia Agosti 3, 2023 katika Parokia ya Mtakatifu Luka Gyedna, jimbo la Minna nchini Nigeria. Mseminari wetu huyu alikuwa katika mwaka wake wa uchungaji kabla ya kuanza masomo ya teolojia.
Kufuatia ya taarifa hiyo ambayo imesambaa pia mitandaoni, gazeti hili lilimtafuta Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana ambaye alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanachukua hatua mbalimbali kuhakikisha Mtanzania huyo pamoja na mwenzake wa Burkina Faso wanaachiwa huru.
Balozi Bana amesema taarifa alizozipata ni kwamba watekaji wanataka Naira 100 milioni (sawa na Sh325.1 milioni) ili kuwaachia huru wote wawili. Alisema wamepiga hesabu na kuona kwamba kila mmoja anatakiwa kulipiwa karibu Dola 70,000 za Marekani 70,000 (zaidi ya Sh170 milioni).
“Tunahitaji kuwa waangalifu katika jambo hili kwa sababu watu hawa si wazuri, wakijua kwamba Serikali italipa wataongeza dau hadi Naira 500 milioni. Kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na wenzetu wa Shirika la Wamissionari wa Afrika ambao tayari wametoa taarifa polisi,” alisema.
0 Comments