Baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumteua Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Mbeya (CCM) Bahati Keneth Ndingo kuwania ubunge wa jimbo la Mbarali, hatimae mwanasiasa huyo amejiuzulu nafasi hiyo ili sasa agombee rasmi ubunge wa Jimbo hilo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Bahati amejuzulu nafasi hiyo kwa mujibu wa lbara ya 149 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Katika barua yake kwa Spika, ameeleza sababu za kujiuzulu ni kuangalia namna nyingine ya kuwatumikia Watanzania katika Bunge.
"Ninakusudia kushiriki kwenye mchakato wa Uchaguzi Mdogo wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Mbarali unaotarajiwa kufanyika Septemba 19,2023."
Bahati aliteuliwa juzi na Kamati Kuu ya CCM Taifa iliyokutana Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Uchaguzi mdogo wa jimbo la Mbarali unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Francis Mtega aliyefariki dunia Julai 1,2023.
0 Comments