Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, John Noronha akielezea umuhimu wakuwalinda wanyamapori |
Ujangili uliokuwa ukisababisha mauaji ya tembo kwenye maeneo yote yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) sasa umekwisha kabisa.
Awali kulikuwa na kasi ya mauaji ya tembo vilivyotokana na ujangili, ambapo kwa mwaka 2013 tembo 50 waliuawa tofauti na mwaka juu wa 2023 ambapo hakuna kifo hata kimoja cha tembo kilichotokana na ujangili.
Ofisa Wanyamapori daraja la kwanza wa TAWA, Tryphon Kanon aliyasema hayo Bagamoyo mkoani Pwani Julai 19,2023 kwenye semina iliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) na kushirikisha wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
JET iliendesha semina hiyo ambayo ni sehemu ya mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Mtaalam huyo amesema kupungua kwa ujangili, kunatokana na jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi ndani na nje ya nchi.
Kanon amesema biashara ya ujangili inahusisha makundi matano ya watu ambao wako kwenye ngazi tofauti za kipato.
John Chikomo, Mkurugenzi wa JET |
"Hawa jamaa wana nguvu sana na ni wengi wako kwenye ngazi tofauti za kipato, kukabiliana nao kunahitaji vifaa vya kisasa na mbinu zaidi.
“Tuliongeza doria katika hifadhi zetu, tukaongeza askari wapelelezi waliosaidia kubaini wauzaji wa pembe hizo, tunashirikisha jamii ili kuuona umuhimu wa kulinda rasilimali zao."
Aidha amefafanua zaidi kuwa kwa sasa meno ya tembo yanayokamatwa mengi ni yale yaliyotokana na mauaji ya tembo ya miaka ya nyuma na wahusika kuyachimbia chini.
Kanon amesema kwa kiasi kikubwa biashara ya meno ya tembo ukuaji wake unawategemea zaidi wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi ambao hushirikiana na majangili, ambapo hulipwa kulingana na kazi wanazozifanya.
“Kuna mgao huwa unatembea, wapo wanaopewa shilingi 5000, wengine 10,000 na wengine hupata zaidi.
"Kuna yule anayehudimia vijana wa kazi, yeye ndio hupata zaidi ingawa kuna wale wakubwa zaidi ambao nao hufaidika sana pia."
Ofisa wanyamapori wa daraja la kwanza TAWA, Tryphon Kanon akifafanua jambo |
"Tulibaini kilo moja ya jino la tembo huuzwa kwa kati ya Sh. 50,000 hadi 70,000 ambapo anayempiga risasi tembo analipwa 10,000, anayewaongoza na kuwaonyesha njia wauaji 5,000, anayeng’oa (dakika sita) 10,000 na wabebaji 5,000.” amesema
Aidha TAWA kwa kushirikiana na wadau wanaamini elimu sahihi ikitolewa kwa jamii vitendo hivyo vitaondoka kwani wao ndio watakuwa mstari wa mbele kuwafichua majangili na wanaoshirikiana nao.
Kwa upande wake Meneja Ufuatiliaji Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, John Noronha, amesema changamoto kubwa ni kutotekelezwa kwa sheria na kanuni zinazoongoza uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori.
“Migogoro tunayoiona kwenye hifadhi, mapori ya akiba ni baadhi ya viongozi kutosimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria na kanuni zinazoongoza rasilimali, kutotenga na kupanga matumizi ya ardhi."
Akizungumza kwenye semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amesema ulinzi wa wanyama na uhifadhi wa maliasili unategemea zaidi uelimishaji jamii na ndiyo ajenda iliyobebwa na JET kwa kutoa elimu kwa wanahabari wote ili iwe rahisi kuisambaza.
“Wahariri wakielewa na kuandika, kutangaza na kusambaza habari sahihi ni wazi jamii kubwa itaelewa na kuwa walinzi wakubwa wa wanyama wetu nchini."
Kwa upande wake Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema wataendelea kuwajengea uwezo Wahariri na waandishi wa habari kuhusu uhifadhi, ulinzi na utunzaji wa maliasili ili kuifikisha jamii katika malengo yaliyokusudiwa.
Mwenyekiti wa JET, Ellen Otaru akiongea na wahariri wakati wa semina |
"Niwaombe Wahariri mkawe mabalozi wa masuala ya uhifadhi wa wanyamapori, ninyi mnao uwezo wa taarifa zenu kuwafikia watu wengi zaidi, tushirikiane kwenye hilo."
0 Comments