NA JIMMY KIANGO
Uwekezaji ni nyenzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi nchini kwa maendeleo ya sasa na ya vizazi vijavyo na umuhimu wa uwekezaji nchini ni kutengeneza ajira, kuongeza wigo wa kodi na kupata teknolojia kutoka mataifa mengine.
Umuhimu mwengine ni kupanua na kukuza miundombinu nchini, kuvutia mitaji na kupunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje ambazo hugharimu fedha nyingi za kigeni (import substitution)
Kutokana na umuhimu wa uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilianzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 26 ya mwaka 1997, lengo ni kuratibu, kuhamasisha, kuvutia na kuwezesha uwekezaji nchini na kuishauri serikali mambo yote yanayohusu uwekezaji.
Katika kuhakikisha sekta binafsi inapata nguvu ya kiuchumi, kituo kinalo jukumu la msingi la kuiwezesha sekta binafsi kufanya kazi zake kupitia uwekezaji kwa kuratibu, kuhamasisha na kutoa huduma kwa wawekezaji.
Katika kulitambua hilo Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, leo Julai 17,2023 amekutana na wahariri na waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini ili kuwaeleza umuhimu na majukumu ya kituo hicho.
Pamoja na mambo mengine Teri amesema kuwa kwasasa kituo kinafanya kazi zake kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Namba 10, ya Mwaka 2022 na kwamba wao ni Wakala wa Serikali kwa ajili ya kuratibu mambo yote yanayohusu uwekezaji nchini.
Aliyataja majukumu ya kituo hicho kuwa ni kuhimiza uwekezaji, kuwafikia na kutoa chachu ya uwekezaji kwa wawekezaji wazawa na wageni, kuhamasisha, kuvutia uwekezaji kwenye fursa za uwekezaji nchini,kuwezesha uwekezaji na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji
Aidha Kituo kina jukumu la kuishauri serikali mambo yote yahusuyo uwekezaji nchini na kwamba kituo kinashirikiana na taasisi mbalimbali katika kufanikisha na kutimiza majukumu yake.
Katika kipindi cha mwaka 2021-2023 kituo kimeweza kufanikisha masuala ya Usajili wa Miradi, Miradi ya Kimkakati, Huduma kwa wawekezaji (Aftercare Services), Kutungwa kwa Sheria Mpya ya Uwekezaji, Ujenzi wa mifumo na utumiaji, Utoaji wa taarifa kwa Umma na Uhamasishaji Uwekezaji.
Katika Kipindi cha Januari 2021 hadi Juni 2023, Kituo Kimesajili jumla ya miradi 778, ambapo mwaka 2021 kilisajili miradi 256 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3,786.75 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 52,846.
Mwaka 2022 kituo kilisajili miradi 293 yenye thamani ya dola za Marekani 4,,537.70 inayotarajiwa kuzalisha ajira 40,889 na mwaka huu wa 2023 kuanzia Januari hadi Juni, kituo kimeshasajili miradi 229 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 2,208.14 na inatarajiwa kuzalisha ajira 31,647.
Usajili huo wa Miradi kuanzia Jan 2021 - Juni 2023 umekuwa na manufaa kwa taifa kupunguza tatizo la ajira kwa kutengeneza ajira mpya 125,382, thamani ya miradi hiyo ni dola za kimarekani Milioni 10,532 ambapo mitaji kutoka nje na ndani imewekezwa
Kwa miradi hiyo kusajiliwa, serikali imeongeza wigo wa mapato, Miradi kutoka nje ya nchi imeleta teknolojia mpya kutoka mataifa mengine (transfer of technology)
Aidha kumekuwa na Miradi ya Kimkakati (Strategic Investment Projects) ambayo imeibua mikataba yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 2.91, katika kipindi cha Januari 2021 - Juni 2023, Kituo kimesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya Kimkakati ipatayo 16 (Strategic Investors projects) na Miradi hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira mpya za moja kwa moja zipatazo 45,065,ambapo katika Kipindi cha Januari hadi Juni 2023, miradi ya Kimkakati 10 imesaini mikataba ya utekelezaji na Kituo.
“Hii ni rekodi kwa Kituo Kusainisha mikataba 10 kwa mara moja tangu kuanzishwa kwake, Mikataba hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1,805.12 na Miradi hiyo ya kimkakati inatarajia kuzalisha ajira mpya za moja kwa moja zipatazo 16,355 na itasaidia kukuza maendeleo ya teknolojia.
Katika kuhakikisha kituo kinahudumia wateja wake kwa ufanisi Teri amesema wameanzisha utaratibu wa kukutana na wawekezaji wa Kisekta ambapo
Katika kipindi cha Machi- Juni 2023 Kituo kimekutana na Sekta ya usafirishaji, Sekta ndogo ya sukari, Sekta ya taasisi za kifedha, Matumizi ya Derivative Rights na Sekta ndogo ya mbolea.
Aidha kituo kinao Mkakati wa siku 1000 (Miaka Mitatu) utakaosaidia Kutimiza malengo hayo, ambao ni kuweka Msisitizo kwenye utekelezaji wa Land bank Manual ili Kituo kuweza kuwa ardhi ya kutosha yenye miundombinu kama barabara, umeme na maji
Kuendelea kuboresha rasilimali watu kwa kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi, wa kati na mrefu.
Kuendelea kuboresha matumizi ya mifumo ya ndani na ya nje
“Kwa kutambua jukumu kubwa ambalo kituo inalo kwa taifa, Kituo kinaendelea kujikita katika maboresho ya kiutendaji ili kuleta mageuzi kwenye uwekezaji, kuwafikia wawekezaji wazawa wengi zaidi ili wanufaike na huduma za Kituo na kuboresha mahusiano na wadau wa uwekezaji ndani na nje ya nchi.”
Pamoja na mambo mengine Teri amesema TIC inapambana ili kuhakikisha nchi inakuwa na wawekezaji wengi zaidi na kwamba ana uhakika zipo baadhi ya bidhaa zitaondoka kabisa kwenye tatizo la kupatikana kwake.
Alizitaja bidhaa hizo kuwa ni sukari na mafuta na kwamba hadi kufikia Desemba 2024 Tanzania haitakuwa na tatizo la sukari, kwani kuna ongezeko la ujenzi wa viwanda vya sukari nchini.
Amesema kwa sasa sheria ya uwekezaji inamlinda na kumjali zaidi mzawa na kwamba Mtanzania yeyote anaweza kuwekeza kwenye miradi mbalimbali.
0 Comments