Ticker

7/recent/ticker-posts

MASWALI 10 MUHIMU KWENYE MAKUBALIANO YA TANZANIA NA DUBAI KATIKA UENDESHAJI WA BANDARI

Jana, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, pamoja na viongozi waandamizi wa wizara na taasisi zake, alikutana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuzungumzia suala la mkataba baina ya Tanzania na Dubai kuhusu uendeshaji wa bandari za Tanzania. Ufuatao ni muhtasari wa mambo 10 muhimu yaliyozungumzwa jana.

Dubai inaruhusiwa kuingia mkataba na Tanzania?

Jibu ni ndiyo. Ingawa Dubai ni sehemu ya Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), suala la uwekezaji si sehemu ya masuala ya Muungano. Katiba ya UAE imeeleza kuhusu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano na suala la uwekezaji halimo. 

Mapendekezo ya kuboresha mkataba yanayotolewa sasa yatafanyiwa kazi?

Ndiyo. Makubaliano ya Tanzania na Dubai yametoa fursa ya kufanya marekebisho kwenye mikataba. Lakini hatua hiyo itafuata baada ya mkataba kuridhiwa kwenye mabunge ya nchi hizo na taratibu za mabadilishano ya nyaraka baina ya pande mbili (exchange of instruments) kukamilika. 


Wanaokosoa mkataba wa IGA baina ya Dubai na Tanzania wana hoja?

Nyingi ya hoja zinazotolewa – karibu hoja nane kati ya kila 10, hazihusu IGA bali mikataba mahususi itakayoingiwa wakati wa utekelezaji. Kwa mfano, masuala kama ukomo wa mkataba, kiwango cha uwekezaji, idadi ya ajira na mambo mengi yanayozungumzwa yatafanyiwa kazi kwenye mikataba itakayoingiwa baadaye. 

Kuna maelezo kuwa mkataba unatoa wajibu kwa Tanzania na haki kwa Dubai. Kuna ukweli?

Dhana ya IGA ni mpya. Kuna tofauti kati ya IGA na Mikataba ya Biashara baina ya nchi na nchi (BIT). Mkataba huu unahusu uwekezaji unaofanyika Tanzania na si biashara baina ya Tanzania na Dubai. Katika IGA hili ni la kawaida kwa sababu Tanzania ndiyo mwenyeji na uwekezaji wote utafanyika kwake. Ni muhimu haki za anayeleta mtaji zikazingatiwa.


Mkataba unauza bandari zetu?

Hapana. Kimsingi, mkataba unahusu uendeshaji ambao ni asilimia nane tu ya shughuli zote za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Kwa miaka 22 iliyopita, kampuni ya TICTS ilikuwa ikifanya shughuli kama hizo na bandari yetu haikuwa imeuzwa au kubinafsishwa. 

Watanzania watapoteza ajira baada ya ujio wa DP World?

Hapana. Suala la ajira kwa Watanzania limewekewa kifungu kabisa kwenye IGA. Hakuna mfanyakazi hata mmoja wa Bandari ambaye atapoteza ajira kutokana na shughuli za uendeshaji baada ya DP World kuanza. Inatarajiwa kuwa ufanisi na ubora wa huduma utakaoanza utasababisha kuwapo kwa ajira nyingi zaidi kuliko ilivyo sasa.

DP World itauziwa ardhi ya Tanzania?Hakuna ardhi ambayo DP World itauziwa kwa mujibu wa mkataba uliopo. TICTS haikuuziwa ardhi yoyote ya Tanzania kwa miaka yote iliyokuwa ikiendesha shughuli za makasha kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Uwekezaji utaathiri ulinzi na usalama wa Tanzania?

Hapana. Kama ilivyo viwanja vya ndege, Bandari ya Dar es Salaam pia ni lango la kuingilia Tanzania. Kwa sasa, viwanja vya ndege kuna watoto huduma kama Swissport na wengine na bado vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na majukumu yake kama kawaida. Suala la ulinzi kwenye maeneo nyeti ya nchi yetu litabaki kuwa jukumu la vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.


Kwa nini serikali haiwekezi yenyewe na inaita wageni?

Uzoefu duniani kote unaonyesha sekta binafsi ni mahiri zaidi katika uendeshaji wa shughuli za bandari kuliko serikali. Nchi nyingi duniani, wakiwamo jirani zetu kama Kenya, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Angola, Ghana na kwingine bandari zinaendeshwa na sekta binafsi. Pia, DP World ina meli takribani 400 na maana yake ni kuwa nao kunahakikisha biashara ya uhakika kwa sababu ya mtandao mpana ilionao. 

Kwa nini uwekezaji huu ni muhimu?

Uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya bandari kwenye mapato ya nchi kutoka asilimia 37 za sasa hadi takribani asilimia 70. Jambo hili litaipa serikali uwezo mkubwa zaidi wa kusaidia sekta muhimu kwa jamii kama vile elimu, afya, maji na kuzimua sekta nyingine za uchumi na hivyo kuchochea upatikanaji wa ajira kwa watu wengi zaidi.

Post a Comment

0 Comments