Uwekezaji mkubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa maslahi ya taifa kwa sasa.
Mwendelezo wa malumbano na misuguano inayofanywa na baadhi ya wanasiasa na wasomi juu ya kuupinga uamuzi wa Serikali kuingia makubaliana na Dubai katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam unatoa mwanya kwa washindani wetu kwenye biashara ya Bandari kutuvuruga zaidi.
Kauli hizo zimetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa leo alipokutana na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini. Katika mazungumzo yake pamoja na mambo mengine, Prof. Mbarawa pamoja na wataalamu wa Wizara yake wamefafanua Kwa kina kuhusu mkataba huo wa uendeshaji wa bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.
Profesa Mbarawa na wataalamu wake wamefafanua kipengele Kwa kipengele vilivyomo kwenye mkataba huo ambavyo baadhi yake vimeibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.
Ikumbukwe kuwa Juni 10, 2023, Bunge lilipitisha azimio la kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari Tanzania.
Profesa Mbarawa amewasisitiza wahariri kuwa lengo la mkataba huo wa makubaliano ni kuweka msingi wa majadiliano kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Amesema mkataba huo umeweka msisitizo kwenye mambo muhimu kama vile ajira kwa Watanzania, ukomo wa mkataba wenyewe pamoja na ulinzi wa Taifa.
Amesisitiza kwamba wakati wa utekelezaji wa mkataba huo, utazingatia masuala mbalimbali kama vile kuweka bayana ukomo wa mkataba, muda wa marejeo ya utekelezaji na mikataba ya kikazi itasainiwa kwa mujibu wa maslahi ya nchi. Alisema mifumo ya kiuendeshaji ya kampuni ya DP World itasomana na mifumo ya Serikali.
"Wahariri, nyie ni watu muhimu, tumeiona haja ya kuzungumza nanyi baada ya kufanikiwa kuzungumza na viongozi wa dini na wafanyakazi wa Bandari.
" Nia yeti ni kutoa ufafanuzi wa makubaliano hayo ili muweze kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi wetu," amesema Waziri Mbarawa.
Pamoja na Serikali kuchukua hatua mbalimbali, Profesa Mbarawa amesema bado ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam haujafikia viwango vinavyotakiwa kimataifa. Amesema hali ya sasa ya utendaji wa bandari imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ukilinganisha na bandari shindani kikanda.
Ametoa mfano mmoja kwamba wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es Salaam ni siku tano ikilinganishwa na siku moja na saa sita kwa Bandari ya Mombasa. Pia, amesema Bandari ya Durban huko Afrika Kusini, meli inakaa kwenye nanga kwa siku moja na saa 13.
Ufanisi mdogo wa Bandari ya Dar es Salaam unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa mifumo ya kisasa na kutokuwepo kwa maeneo ya kutosha ndani na nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhia shehena pamoja na eneo la maegesho ya meli," amesema.
Kutokana na changamoto hizo, Serikali ilitafuta mwekezaji kwa ajili kuongeza ufanisi wa bandari hiyo, ndipo akapatikana Kampuni ya DP World, ambayo tayari imeingia makubaliano yatakayowaongoza kwenye mikataba ya kiutendaji.
Aidha Mwenyekiti wa majadiliano baina ya pande mbili za mkataba huo, Hamza Johari amesema mkataba huo unakwenda kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa bora na ya kisasa na itaondokana na utaratibu wa kupakua na kupakia mizigo tu.
"Bandari ya kisasa maana yake ni kuufuata mzigo kwa mzalishaji hukohuko na kuuleta hadi bandarini, kisha unaupeleka hadi kwa mwagizaji, hii tunaita end to end port. Tunataka kwenda huko," amesema.
Johari ametumia nafasi hiyo kufafanua mkataba huo kifungu kwa kifungu na kuwaeleza Wahariri namna mkataba huo utakavyokuwa na manufaa kwa Tanzania na kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa na nafasi kubwa ya kukusanya kiasi kikubwa cha mapato.
"Huu si mkataba wa utekelezaji, ni makubaliano yanayoweka msingi wa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World."
Johari ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA), amesema mkataba huo hauna matundu,hauna dosari na ni mkataba mzuri na wenye tija kwa nchi.
Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deudatus Balile amesema kuna haja ya kulitolea ufafanuzi wa kina suala hilo ili lieleweke kwa kina na watu sahihi wa kulijibia ni wataalam.
0 Comments