IDADI ya wagonjwa wa Figo wanaopewa huduma za kuchuja damu katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila imeongezeka kutoka wagonjwa 91 kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022 na kufikia wagonjwa 157 kwa kipindi kama hicho mwaka huu 2023 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 72.
Hatua hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa katika sekta ya afya na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza vifaa tiba na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH-Mloganzila Dkt. Immaculate Goima amesema uelewa wa dalili za magonjwa yasiyo ya kuambukiza miongoni mwa jamii umeongezeka jambo ambalo limepelekea wagonjwa kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na kuanza matibabu mapema.
Dkt. Goima ameongeza kuwa Mloganzila imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na pale wanapohisi kuwa na dalili za magonjwa hayo wanashauriwa kufika hospitalini mapema kwa ajili ya ushauri na matibabu badala ya mgonjwa kusubiri hatua za mwisho ndio anakwenda hospitalini.
“Mloganzila tuna wataalamu wenye ujuzi na weledi katika matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya figo, tunatoa huduma kwa saa 24 siku kila siku, watoa huduma wetu wana ari, morali na wanajali wagonjwa pia wanatoa huduma muda wote” amefafanua Dkt. Goima.
Akizungumzia kuhusu huduma za kupandikiza figo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH-Mloganzila Gyunda Anthony ameeleza kuwa, Mloganzila ilifanya upandikizaji kwa wagonjwa watatu ambapo kumekuwa na mafanikio makubwa kwani wagonjwa hao na ndugu waliowachangia figo wanaendelea vizuri na kufanya shughuli zao kama kawaida.
0 Comments