Ticker

7/recent/ticker-posts

KISWAHILI KINATOSHA KUWA 'VAZI LA TAIFA'

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akiwa katika vazi la asili.

Na. Jimmy Kiango

Kwa miaka mingi sasa kumekuwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wana hamu na kiu ya nchi kuwa na vazi la Taifa, sijawahi kujua dhamira yao ya kulisaka hili wanaloliita vazi la Taifa ni nini! Kama dhamira ni utambulisho wa Utanzania wetu sina hakika kama vazi litatosha kututambulisha.

Nasisitiza kiu hiyo ya kulitaka hilo vazi ni ya baadhi ya wanasiasa si wananchi wa Tanzania iwe bara ama hata Zanzibar, sina hakika kama wananchi wana kiu hiyo, maana mimi na baadhi ya watu niliojaribu kuwauliza hawana kiu hiyo. Hawana na ndio maana wala haiwashangazi wala kuwaumiza hata harakati hizo zinapokwama.

Ni ukweli usiopingika harakati za kusaka vazi la Taifa kwa muda mrefu sasa hazijawahi kufanikiwa pamoja na kuundiwa kamati zilizojaa manguli na wabobevu wa Sanaa, Ubunifu na Mitindo lakini hakuna matokeo chanya yaliyopatikana tangu mwanzo na hata sasa.

Ikumbukwe kuwa mchakato wa kutafuta vazi la Taifa ulianza muda mrefu, lakini ulianza kuchanua zaidi mwaka 2011, hapo ulichukua sura mpya baada ya  aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo (Wakati huo) Dkt. Emmanuel Nchimbi kuunda kamati maalum ya kulisaka vazi hilo.

Hata hivyo kazi hiyo haikukamilika kwani kulitokea mabadiliko katika Baraza la Mawaziri mwaka 2012, ambapo Dkt. Nchimbi alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Fenella Mukangara  alipewa Wizara hiyo na suala hilo halikuwa kipaumbele chake.

Pamoja na Kamati maalum  iliyoteuliwa na  Dkt. Nchimbi kulishughulikia suala hilo na kumkabidhi michoro sita waliyoipata katika michoro 200 waliopelekewa na wasanii mbalimbali, hakuna kilichoendelea.

Uongozi wa Waziri Fennela haukuwa na mpango kabisa na jambo hilo, hadi pale Nape Nnauye alipokabidhiwa wizara hiyo na mwaka 2014 aliufufua tena mchakato huo na kuipa kazi kamati ileile ya Dkt. Nchimbi ili iendeleze pale ilipoishia.

Kamati hiyo iliundwa na wabobezi na manguli wa Sanaa, Burudani,Ubunifu na Habari akiwemo Mkurugenzi wa Kampuni ya Clouds Media, Joseph Kusaga ambaye alikuwa Mwenyekiti, Katibu alikuwa Angela Ngowi huku wajumbe wa kamati hiyo wakiwa ni Habib Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali,Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda, ambaye baadaye alitangaza kujiweka kando.

Kama ilivyokuwa awali, hata katika awamu hiyo ya pili hakuna kilichofanikiwa badala yake kazi yao iliishia kwa mara nyengine kwenye makavazi ya Wizara.

Kutokana na kutojua mzizi wa tatizo na kwa sababu hitaji hilo ni matakwa ya baadhi ya wanasiasa zaidi mwaka 2022 aliyekuwa Waziri wa ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohamed Mchengerwa nae alilifufua upya suala hilo kwa kuunda kamati maalum.

Uamuzi wa Mchengerwa ulisukumwa na agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kutaka mchakato wa kupatikana kwa vazi la Taifa uendelee.

Haraka Waziri Mchengerwa akatekeleza matakwa ya kisiasa kwa kuunda kamati, safari hii ikiwa na uongozi na wajumbe wapya isipokuwa Mustafa Hasanali ambaye alikuwamo kwenye kamati zote za awali.


Aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi 

Kamati ya Mchengerwa iliundwa na Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Profesa Hermas Mwansoko (Mwenyekiti) na Mkurugenzi wa Utamaduni kutoka Wizarani Dkt.Emmanuel Temu (Katibu)

Wajumbe ni Chifu Antonia Sangali (Mwakilishi wa Machifu),Hadija Mwanamboka (Mbunifu wa Mitindo),Mustafa Hasanali (Mbunifu Mitindo),Mrisho Mpoto(Msanii) Fatuma Hassan, maarufu kama DJ Fetty na Masoud Ally maarufu kama Kipanya (Mchoraji na Mtangazaji).

Uteuzi wa kamati hii mpya ulizua minong’ono kidogo, baadhi ya wakereketwa walijawa na hinda kidogo na kudai kuwa kamati hiyo inakwenda kutafuna fedha za serikali bila sababu kwa hoja kuwa tayari kazi ilishafanyika huko nyuma.

Waziri kwa dhamira ya kutaka kikombe cha lawama kimuepuke alitoa utetezi wake kuwa kamati hiyo haitafanya kazi tofauti na ile iliyofanywa awali, badala yake itaanzia pale walipoishia wenzao.

Masikini ya Mungu, Waziri Mchengerwa nae yakamkuta yale yaliyomkuta Dkt. Nchimbi na baadae Nape ya kuhamishwa Wizara.

Yalimkuta hayo kabla hajakamilisha kazi. Februari 14, mwaka huu akaondolewa kwenye Wizara hiyo na kupelekwa wizara ya Maliasili na Utalii na nafasi yake kuchukuliwa na Dkt. Pindi Chana.

Sina hakika kama Dkt. Chana ana mzuka na uhitaji wa suala hilo la vazi la Taifa, kama hana hii nia maana yake  mchakato na zoezi zima ndio umekwama na kama anao basi huenda nae akaja na kamati yake.

Imani niliyo nayo, yapo mambo mengi muhimu ndani ya Wizara hiyo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi zaidi ya hili la vazi la Taifa.

Ukweli ni kwamba zoezi hilo ni gumu na halitakuja lifanikiwe milele na ikitokea limefanikiwa basi utakuwa ni utashi wa kisiasa tu na si matakwa ya wananchi.


Aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Fennela Mukangara akiwa na baadhibi ya wajumbe wa iliyokuwa Kamati ya Vazi la Taifa.

KWANINI  GUMU

Zoezi hilo ni gumu na ugumu wake unakolezwa na idadi ya makabila yaliyopo Tanzania ambayo ni zao la Tanganyika yenye makabila zaidi ya 100 na kila kabila lina tamaduni, mila na desturi zake na hali iko hivyo pia Zanzibar.

Uwapo wa idadi kubwa ya makabila kunaharamisha kabisa kiu ya kutafuta vazi la Taifa, uharamu unaletwa na hilo vazi litakalopatikana ni wazi litakuwa ni mfano ama mfanano wa kabila moja au makabila machache ndani ya Tanzania.

Hatua hii ya kuchagua vazi la Taifa kutoka kwenye kabila moja au makabila machache kuwa vazi la Taifa inaweza isituache salama, inaweza kuzua chuki zisizo na msingi, tukubali kila kabila linatamani vazi lake liwe vazi la Taifa.

Lakini hebu tujiulize ukiacha matumizi ya Migolole, Kaniki, Ngozi, Mashuka, Baibui na Kanzu ni vazi lipi jengine litaweza kuutambulisha zaidi utanzania wetu?

Ukiondoa Baibui na Kanzu, je, hawa wanaolisaka vazi la taifa wako tayari kuvaa kaniki na kwenda nazo mbele ya macho ya wakubwa wa dunia! Ni nani kati yao yuko tayari kuiacha suti yake ya bei ghali na kuvaa vibwende vilivyoungwa ungwa na fundi Saidi wa pale Bwembwela, Muheza!

Tukubali kuwa hatuwezi kuwa na vazi moja la taifa na hilo lisiwe tatizo kama ambavyo si tatizo kwa sasa. Kama tumeweza kupata Bendera ya Taifa, wimbo wa Taifa, Nembo ya Taifa na Lugha ya Taifa vitutoshe na turidhike, haya mengine tunayoyasaka yanaweza yasiimarishe umoja wetu na badala yake yakatubagua.

Tunataka vazi la Taifa ili kumfurahisha nani au kumuonesha nani kuwa sasa tunalo vazi la Taifa, je, kuna mahali popote Viongozi wetu,Wanamichezo wetu ama Wananchi wamewahi kubaguliwa kutokana na kukosa vazi la Taifa!?


Aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Fennela Mukangara akiwa na baadhibi ya wajumbe wa iliyokuwa Kamati ya Vazi la Taifa

Tunayo zaidi ya miaka 60 sasa tangu tupate Uhuru, sidhani kama tuliwahi kuwa dhalili kwa kukosa vazi la Taifa, Tanzania hatutakuwa wa kwanza kutokuwa na vazi la Taifa na kulikosa vazi hilo hakutuondolei utambulisho wetu mbele ya macho ya wakubwa.

Hakuna shaka yeyote Lugha ya Kiswahili ni yetu na ndiyo iliyotuweka pamoja tangu kale hadi sasa, Kiswahili kimeubeba uswahili wetu, kimeubeba utambulisho wetu, kimetubeba Watanzania wa Bara na Visiwani, hakuna kingine kitakachotutambulisha popote pale zaidi ya Kiswahili na Uswahili wetu.

Hatuna sababu tena ya kuhangaika na kitu mbadala cha kutuunganisha kama Taifa, tukubali wenzetu wenye vazi la taifa hawana Lugha rasmi ya Taifa, zaidi ni wakabila, sisi Mungu ametujalia hilo,hatuna ukabila badala yake tuna Utaifa, tusichokonoe mengine, hatutayaweza. Tushukuru hiki tulicho nacho.

Vazi la Taifa tuwaachie wenye nalo, sisi tuendelee na Kanzu zetu, Mabaibui, Migolole, Kaniki, Ngozi na Shuka zetu na hata wanaopenda kuvaa Suti waendelee tu, midhali haitudhuru kuna ubaya gani!


Muhimu tukithamini Kiswahili kwa dhati ya mioyo yetu, tukipe thamani stahiki ili kiwe mali yetu kikweli kweli.

Tukipambe, tukirembe, tukivike vazi la hariri na tusiogope kukisema popote pale, tujivunie Kiswahili, tukifanye kuwa sisi na sisi tuwe Kiswahili.

Moja ya mambo muhimu yaliyotuunganisha wananchi tangu tukiwa Tanganyika na Zanzibar hadi sasa tukiwa Tanzania, ni Kiswahili na pongezi ziende kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake waandamizi kwa kukisimamia Kiswahili Mijini na Vijijini.

Uzungumzaji na uandishi mzuri wa Lugha ya Kiswahili unatosha kuwa utambulisho wetu, hatujachelewa kama tunataka kuwa na kitu bora zaidi cha kututambulisha haraka basi vazi la Taifa letu kiwe Kiswahili, tukipe thamani halisi Kiswahili chetu ili yeyote atakaemuona Mswahili aseme huyu ni Mtanzania.

Post a Comment

0 Comments