Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA NA KENYA KUBORESHA HUDUMA YA UMEME KANDA YA KASKAZINI

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba(kulia) akipata maelezo ya mifumo kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi katika Mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Lemugur, wakati wa ziara ya kukagua maenedeleo ya ujenzi wa Kituo hicho, Juni 12, 2023 mkoani Arusha.

Na Zuena Msuya, Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa, mradi wa kimkakati  wa umeme utakaounganisha Tanzania na Kenya kupitia kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Lemugur  kilichopo mkoani Arusha utaboresha huduma ya umeme katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Mramba alisema hayo, Juni 12, 2023 mkoani Arusha, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha Lemugur mkoani humo, ambacho kitakuwa na uwezo wa kupokea na kusambaza umeme wa msongo mkubwa wa Kilovolti 400, kutoka Singida, Namanga hadi nchini Kenya.

“Mradi huu ni Mkubwa kwa nchi yetu, ni mradi wa kimkakati katika kuboresha huduma ya umeme nchini, pia kituo hiki cha Lemugur, kitaiunganisha Tanzania na Kenya kwenye umeme, na kitaboresha upatikanaji wa huduma ya umeme unaoikabili Mikoa ya Kanda ya Kaskazini”, alisema Mhandisi Mramba.

Amesema, kituo cha Lemugur ni muhimu kwa Serikali kwa kuwa, kinaunganisha njia ya umeme kutoka Tanzania kwenda Kenya kama ilivyo katika mpango wa Serikali wa kutaka kuunganisha Tanzania na nchi nyingine kwa njia ya Msongo mkubwa wa Kilovolti 400.

Pia, kituo hicho kitakuwa na uwezo kupeleka na kuboresha huduma ya umeme katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

“Kwa miezi kadhaa sasa, Mkoa wa Tanga umekuwa na changamoto za upatikanaji wa huduma ya umeme kwa kuwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi mkoani humo imezidiwa uwezo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kutokana na uwepo wa viwanda vingi. Hivyo kituo hiki cha Lemugur kitafanya mkoa wa Tanga kupata umeme kutoka vituo viwili ambapo kituo kingine ni Chalinze.”amesema Mhandisi Mramba. 

Aidha, amesema kituo hicho pia kitakuwa na uwezo wa kusambaza umeme wa Msongo wa Kilovolti 33 katika mkoa wa Arusha wenye shughuli nyingi za kiuchumi na Utalii.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba(katikati) akimueleza jambo Mkandari anayetekeza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Lemugur, Clive Sihwa kutoka Kampuni ya GOPA (pili kushoto), wakati wa ziara ya kukagua maenedeleo ya ujenzi wa Kituo hicho, Juni 12, 2023 mkoani Arusha.
Mhandisi Mramba aliongeza kuwa, Serikali pia ina mpango wa kujenga njia nyingine ya kusafirisha umeme kwa kuunganisha nchi ya Zambia  na Tanzania na kisha Uganda na Tanzania.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Mramba alitoa maagizo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuwa kazi ya ujenzi katika kituo hicho ifanyike kwa ubora na viwango vinavyotakiwa na hadi kufikia Julai 31, 2023, ujenzi wa kituo hicho uwe umekamilika. 

Aidha, ameagiza kuwa, mwezi Septemba mwaka huu, njia za kusafirisha umeme kutoka Arusha kwenda Tanga ziwe zimekamilika ili mkoa huo uwe na uwezo wa kupata umeme kutoka Mkoa wa Arusha.

 Kwa upande wake, Mkandarasi anayetekeza mradi huo, Clive Sihwa kutoka Kampuni ya GOPA alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati uliopangwa kwa kuwa sehemu kubwa ya ujenzi katika mradi huo imekamilika.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Mramba na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo walikagua njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa Kilovolti 400 katika eneo itakapojengwa Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na Watu, mkoani Arusha.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba(katikati) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakati wa ziara ya kukagua maenedeleo ya ujenzi wa kituo cha Lemugur, Juni 12, 2023 mkoani Arusha.

 

 

Post a Comment

0 Comments