Na Sidi Mgumia, Dar es Salaam
Ili kuwa na uhifadhi bioanuai
endelevu wadau wa mazingira nchini wamekutana kujadili hali halisi iliyopo sasa
na namna bora yakukabiliana na changamoto zilizopo.
Kupitia mradi wake wa Tuhifadhi
Maliasili, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa
(USAID) limewakutanisha wataalamu wa mazingira,
misitu pamoja na waandishi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira
Tanzania (JET) ili kujadili na kusaidia juhudi za uhifadhi wa bioanuai na mazingira kwa ujumla.
Hilo linajiri wakati ambapo inaelezwa kuwa mazingira haswa misitu hapa nchini inakabiliwa na changamoto za kupanuka kwa miji na kukua kwa shughuli za binadamu; misitu kuchomwa moto, uvunaji haramu na matumizi ya mazao ya misitu yasiyo na tija.
Noronha amesema maeneo mengi yaliyohifadhiwa yana
misitu, majani ambayo yanaichukua hewa ya ukaa kwa asilimia kubwa, kulingana na
takwimu za dunia hayo maeneeo yanachukua takriban asilimia 37 ya hewa chafu
inayozalishwa duniani ambapo huichukua hewa hiyo na kuipeleka ndani chini ya
ardhi.
“Kwa Tanzania ukiangalia maeneo ya uhifadhi
tuliyonayo, ardhi asilimia karibia 30 na zaidi imehifadhiwa kwahiyo unaweza
ukaona mchango mkubwa uliopo katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya
tabia nchi,” aliongeza Noronha
Aliongeza kuwa maeneo hayo ikija kwenye suala la
mabadiliko ya tabia nchi, yanasaidia uhifadhi wa udongo pia yanachangia uwepo
wa maji kwa kuhifadhi vyanzo vya maji, hivyo ni muhimu kuvitunza.
“Kingine cha muhimu sana ni kwamba haya maeneo ya
uhifadhi ni maabara za utafiti na data kwa ajili yakusaidia kupima viwango vya
madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na namna gani binadamu wanaishi na
mabadiliko haya. Na baada ya utafiti kunapatikana namna nzuri ya kufanya
maamuzi sahihi ya maendeleo nchini.
Akiongelea kuhusu shughuli za maendeleo na utunzaji
wa bioanuai, Dk Kalumanga amesema kuwa ni ngmu kuzuia shughuli za binadamu lakini
nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania kupitia taasisi husika za mazingira
kama vile NEMC waliamua kuweka miongozo na mipango ya namna ya kuhifadhi
mazingira ndani ya eneo liliondelezwa ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Utangazaji Utalii Ikolojia kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Anna Lauwo alisema mabadiliko ya tabia nchi bado ni changamoto kubwa ulimwenguni, mataifa bado yanaendelea kukuna vichwa kutafuta namna za kupambana na changamoto hiyo.
“Mabadiliko ya tabia nchi yalianza miaka mingi iliyopita ulimwenguni na kwa Tanzania athari za mabadiliko hayo zilianza kuonekana mwaka 2009, kukaanzishwa miradi mbalimbali ya kuhifadhi ardhi, mradi wa kwanza ulikuwa Babati mkoani Manyara ambao ulikuwa wakuhifadhi miti na kuweka matuta yanayoitwa makinga maji ili mvua ikinyesha maji yaingie chini na kuhifadhiwa. Miradi yote hiyo katika maeneo mbalimbali nchini ilikuwa na lengo la kukabiliana na mabadiliko hayo,” alisema Lauwo
Lauwo alisisitiza kuwa pamoja na hilo Serikali ilianzisha mikakati ya kurekebisha sera, sheria, miongozo zinazoendana na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili yakuonyesha ni jinsi gani watakabiliana na hayo maabadiliko.
Ikiwa kama changamoto ya dunia, Lauwo alisema mwaka 2011kulifanyika kikao mjini Born, Ujerumani maamuzi yakawa ni kurejesha uoto wa asili (misitu) hekta milioni 350 ili kuokoa mazingira duniani, wakakubalina kila bara lirejeshe kiasi kadhaa ambapo Afrika ilikubali kurejesha hekta milioni 100. Mwaka 2013 Afrika ilikutana nchini Afrika Kusini kujadili namna yakutekeleza makubaliano hayo ambapo Tanzania ilisema inachangia hekta bilioni 5.2 kulingana na uchafuzi wa mazingira uliopo.
“Mataifa yaliona njia rahisi isiyo na gharama yakukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni kurudisha uoto wa asili kwa maana ya kupanda miti, hii ni kwasababu chakula cha miti ili iweze kuishi ni caborndiyoxide na yenyewe inatoa oxygen inayosafisha anga na ndio maana tunasema kwa mfano msitu wa Pugu ni mapafu ya Dar Es Salaam kwakua kazi ya mapafu ni kusafisha damu na ndivyo ilivyo kwa miti kusafisha anga,” alisisitiza Lauwo
Akifafanua zaidi juu ya mjadala huo
kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Mazingira Tanzania (JET), Dk. Ellen Otaru alisema lengo kuu la mjadala ni
kuibua masuala ya msingi yanayohusu utunzaji wa bioanuai na mazingira kwa
ujumla, kujua namna bora yakukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia
nchi lakini pia kuwafikishia ujumbe wananchi, watunga sera na wadau wengine wa
mazingira kupitia habari zilizoandikwa kwa kina zenye uwazi na uelewa mkubwa.
“JET tuna nafasi kubwa sana yakuwaelimisha na
kuwabadilisha uelewa wananchi, watunga sera, watekelezaji na wawekezaji juu ya masuala
ya uhifadhi wa bioanuai kwa maana ya umuhimu wake, faida zake lakini pia
madhara yatokanayo na uharibifu wa bioanuai hizo na namna Serikali na ulimwengu
zinavyopambana na changamoto hizo,” alisema Dk. Otaru
Nchini Tanzania, ongezeko la idadi ya watu,
usimamizi mbovu wa mazingira, shughuli za kilimo na mabadiliko ya tabia nchi
vinatishia hali ya maisha kote mijini na vijijini pamoja na masuala muhimu
katika kusaidia juhudi za uhifadhi wa bioanuai.
0 Comments