Wafanyabiashara wakubali kusitisha Mgomo wa kufunga maduka.
Wawakilishi wa Wafanyabiashara Kariakoo kukutana na Waziri mkuu May 18 Saa 5 asubuh Magogoni DSM.
RC Makalla Aelekeza TRA kusitisha Operesheni ya Kamatakamata.
Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt, Samia itaendelea Kutatua kero za wafanyabiashara.
Kufuatia wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kupanga kufanya mgomo wa kufunga maduka kushinikiza Serikali kutatua kero zao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam CPA. Amos Makalla mapema leo amekutana na wafanyabiashara hao na kufanikiwa kumaliza mgomo huo.
Akitoa tamko la Serikali CPA. Makalla amesema Serikali imewaelekeza TRA kusitisha Operesheni ya kamatakamata mpaka pale ufumbuzi wa pamoja utakapopatikana.
Aidha CPA. Makalla amesema ifikapo Alhamis ya Mei 18 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atafanya kikao na Kamati ya Wafanyabiashara wa Kariakoo Saa 5 asubuh ofisi ya Waziri mkuu Magogoni Dar es Salaam ili kupata Suluhu ya pamoja ya kumaliza tatizo hilo ambapo kwenye kikao hicho kitajumuisha pia mawaziri wa kisekta.
Pamoja na hayo CPA, Makalla ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuendelea kufanya biashara kwa amani na utulivu wakati Serikali ikiendelea kufanyia kazi madai yao huku akihimiza kulipa kodi kwa mujibu wa Sheria.
Baada kukamilika kwa kikao hicho Cha maridhiano, wafanyabiashara wote walielekea kwenye maduka yao na kuyafungua ambapo baadhi ya Wafanyabiashara wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza na kutatua kero yao kwa wakati na wameahidi kushirikiana na Serikali.
0 Comments