Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka jamii ishirikiane na akinamama katika malezi ili kujenga jamii yenye maadili ya kitanzania.
Ametoa wito huo jana
usiku (Jumapili, Mei 14, 2023) wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya
Mtoko na Mama kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ikiwa ni
maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani. Hafla hiyo iliandaliwa na taasisi ya Binti
Lindi Initiative.
“Akinababa washirikiane na
akinamama katika malezi ya watoto kwani kidole kimoja hakivunji chawa. Sote
tumelelewa na akinamama zaidi, lakini akinababa tunapaswa vilevile kujipa muda
na kufuatilia mwenendo wa tabia ya mtoto kuanzia asubuhi mpaka usiku,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu
ametoa wito kwa jamii kuheshimu na kuthamini mchango wa mama katika malezi. “Kama
wahenga walivyosema, kuzaa siyo kazi ila kazi ni kulea mwana, tushirikiane na
akinamama wote katika malezi ili kwa pamoja tuweze kujenga jamii yenye maadili
ya Kitanzania,” amesema.
“Ninatambua kuwa mama zetu katika karne hii mnafanya shughuli nyingi za
kiuchumi kwa ajili ya ustawi wa familia na Taifa kwa ujumla. Niwasihi sana
muendelee kuwa vinara katika suala la malezi ya watoto,” amesisitiza.
Amewataka wazazi na
walezi wajitambue kuwa wao ni taasisi muhimu tena ya kwanza katika malezi ya
mtoto. “Timizeni wajibu wenu, shirikianeni na taasisi za kiserikali ili kukuza
na kuimarisha maadili kwa watoto wenu pamoja na kutenga muda wa kuwafuatilia
ili kujua changamoto zao na kuwelea ipasavyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi wa taasisi ya Binti Lindi Initiative Kijakazi Yunus
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Mwanaidi Ali Khamisi alisema Siku ya Mama Duniani huadhimishwa kila Jumapili ya pili ya mwezi Mei kila mwaka.
Alisema kumekuwa na
matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto na wizara yake iliamua kuunda madawati
ya watoto kwenye shule zote za msingi na sekondari ili wapate mahali pa
kujieleza pindi wakiona dalili ama wakifanyiwa ukatili.
“Hadi kufikia Machi 2023, madawati 1,488 yameundwa ambapo 1,070 yako
kwenye shule za msingi na 418 yako kwenye shule za sekondari. Lengo letu ni
kuzifikia shule 25,000 hapa nchini,” alisema.
Kwa nyakati tofauti,
walisisitiza kuwa suala la lishe bora kwa watoto katika ngazi zote za makuzi
kuwa ni la muhimu. “Lishe isipokuwa kamili kwa mtoto, inaweza
kuleta ulemavu hata kama alizaliwa akiwa mzima (bila ulemavu),” alisema
Bi Sophia Mbeyele ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Makumbusho ambaye
amekuwa akifanya harakati kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Naye Mkurugenzi wa
taasisi ya Binti Lindi Initiative, Bi. Kija Yunus Mohammed alisema: “Niwasihi
vijana tuwaheshimu wazazi wetu na kamwe tusiwaone kuwa wamepitwa na wakati
kwani sikio halizidi kichwa. Tuepuke vishawishi vya fedha vinavyoweza kuwa
chanzo cha kuleta tatizo la kimaadili miongoni mwetu,” alisema.
Akisisitiza kuhusu
malezi, Sheikh Alhad alisema: “Mtoto anapaswa anyonyeshwe maziwa ya mama yake
kwa miaka miwili ili kumjengea hatma nzuri na kuimarisha uhusiano na mama yake
na muumba wake. Mtoto asiyenyonya kwa miaka miwili hukosa mahusiano na Mungu,”
alisisitiza.
Naye, Askofu Sylvester
Gamanywa wa Kanisa la BCIC la jijini Dar es Salaam aliomba viongozi wa dini washirikishwe
kwenye suala la maadili ili kujenga hofu ya Mungu. “Bila hofu ya Mungu, sheria
haifanyi kazi. Na hofu hii ya Mungu inatoka kwenye misahafu yetu, Niwasihi
viongozi wa dini tusiishie kusalisha tu, bali tujenge hofu ya Mungu ndani ya
jamii,” alisisitiza.
Halfa hiyo ilihudhuriwa
na viongozi mbalimbali, mabalozi na wanawake na mabinti kutoka sehemu
mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.
0 Comments