Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimetangaza kushirikiana na Kituo Cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) kuwasaidia wafanyakazi 195 wa kampuni ya Sahara Media kudai kulipwa malimbikizo ya madai ya mishahara yao kiasi cha sh 3.5 bilioni.
Uamuzi huo,umetangazwa jana na Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma na Mjumbe wa bodi ya udhamini wa JOWUTA, Mutta Robert katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa chama cha ushirika Nyanza, baada ya kukutana na pande zote katika mgogoro huo.
Juma amesema baada ya majadiliano baina ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na ofisi ya Idara ya kazi mkoa wa Mwanza na LHRC wameazimia kupeleka mgogoro huo katika Tume ya usuluhishi(CMA)
"Kwa kuwa mwajiri hajakaidi kulipa deni hili na kwa kuwa ameshindwa kulipa licha ya kuahidi kufanya hivyo hali yake ya fedha itakapokuwa nzuri ,tumeona njia bora ni kupeleka shauri hili CMA,”amesema
Amesema JOWUTA kama chama cha wafanyakazi itashirikiana na LHRC na wanasheria wengine ambao tayari wameonesha nia ili kuhakikisha haki za wafanyakazi hao zinapatikana .
Juma amesema uamuzi huo,pia umefikiwa ili kulinda heshma ya Tasnia ya Habari nchini,kwani kwa sasa ni miongoni mwa sekta ambazo zinachangamoto kubwa ya malipo na stahiki za waandishi na watangazaji kwani wengi hawana mikataba licha ya kufanya kazi kwa miaka mingi.
"JOWUTA tunaamini kesi hii ya Mwanza itakuwa ni mfano wa kesi nyingine ambazo zitafata katika kulinda na kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini,kwani hadi sasa kuna waandishi wanalipwa sh 1000 kwa habari moja na wengi hawalipwi kabisa na kubaki kutegemea kulipwa na wanaowapa habari,”amesema
Amesema Wafanyakazi wa vyombo vya habari wanastahiki kupata heshima na hadhi sawa na wafanyakazi wa sekta nyingine kwani licha ya serikali kutunga sheria za kazi na sheria za vyombo vya habari lakini bado wanahabari wanataabika.
"Wanahabari licha ya kufanya kazi kubwa bado asilimia 80 hawana ajira za kudumu wala mikataba, tofauti na taaluma nyingine hali ambayo imekuwa ikiathiri utendaji wao wa kazi,”amesema
Amesema wakati wamiliki wa vyombo vya habari wakililia uhuru wa vyombo vya habari na kulipwa malimbikizo ya madeni ya matangazo wanapaswa kutambua kuwa uhuru huo hautakamilika kama wanahabari wataendelea kuwa na maslahi duni, kufanya kazi bila mikataba na kutolipwa mishahara.
"Tunataka katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu suala la maslahi bora kwa Wanahabari lipewe kipaumbele kwani uhuru wa vyombo vya habari hauna maana kama hakuna maslahi bora kwa Wanahabari , tunaiomba serikali kuchukuwa hatua kwa wamiliki ambao hawazingatii sheria licha ya kupata mapato katika vyombo vyao”amesema
Wakili Hamisi Mayomba wa LHRC.
Tayari taratibu za kufungua shauri hilo zimeanza na ambacho kinasubiriwa ni kukamilishwa kwa nyaraka mbalimbali ambazo zitasaidia katika shauri hilo.
Mjumbe wa bodi wa Wadhamini JOWUTA ,Mutta Robert alisema watatumia sheria za kazi kufungua mashauri katika vyombo vyote vya habari ambavyo havilipi wanahabari.
"Sheria za kazi zipo tutahakikisha tunazitumia kulinda heshima ya taaluma hii kwani kuna wamiliki wa vyombo vya habari wanawatumia wanahabari kama vitega uchumi vyao”amesema
Robert ambaye pia ni Mwanasheria amesema sheria zipo wazi na lazima zifuatwe na wamiliki wa vyombo vya Habari na kesi ya Mwanza itakuwa mfano kwa wamiliki wengine ambao hawazingatii sheria za kazi.
Awali Afisa kazi kiongozi mkoa wa Mwanza, Betty Mtega alisema Ofisi yake imechoshwa na mashauri ya Wanahabari kushindwa kulipwa stahiki zao.
"Tumekuwa na kesi ya Sahara Media na vituo vingine vya radio, hawataki kuwalipa wafanyakazi wao licha ya kukiri kudaiwa”amesema
Hata hivyo amesema serikali pia haijakaa kimya na shauri la Sahara Media kwani hivi karibuni litafikishwa mahakamani na ofisi ya Mwanasheria Mkuu Kanda ya Ziwa.
"Kamishna wa kazi nchini tayari amekamilisha taratibu zote za shauri hili kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kumbukumbu zetu hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2021 wafanyakazi 152 walikuwa wanadai zaidi ya sh 2.5 bilioni na mwajiri amekiri kudaiwa”amesema.
Hata hivyo amesema deni hilo limekuwa kubwa kutokana na wanahabari kutojua sheria za kazi kwani walipaswa kufungua mashauri mara tu wanaposhindwa kulipwa kwa miezi miwili.
Mwenyekiti wa chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza,Edwin Soko amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanaajiri na kutoa mikataba bora.
"Mwanahabari bora ni yule ambaye pia uchumi wake upo vizuri hivyo wamiliki wakiwalipa vizuri wafanyakazi wao wataweza kufanya kazi kwa weledi mkubwa”amesema
Hata hivyo Soko amewataka wanahabari nchini kujiunga na JOWUTA kwani kisheria ndio chama pekee cha wafanyakazi ambacho kinadhamana ya kutetea maslahi yao.
0 Comments