Pamoja na timu ya Simba SC kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kumaliza dakika 90 kwa usawa wa mabao 1-1 katika mechi mbili za robo fainali dhidi ya Wydad, bado timu hiyo imeendelea kusalia kwenye vinywa vya mashabiki na viongozi wa soka Afrika.
Simba ilimaliza safari yake kwenye michuano ya CAF kwenye Uwanja wa Mohammed V jijini Casablanca nchini Morocco.
Katika mchezo huo ambao Simba haikuwa na mabadiliko katika kikosi chake kilichoanza mechi ya Dar es Salaam, ilionesha ubora wa hali ya juu mbele ya mabingwa watetezi wa kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bao la dakika ya 24 lililofungwa na Bouly Sambou kwa kichwa lililosababisha wakati mgumu kwa Simba, ambapo baadhi ya mashabiki wa soka Tanzania na nje ya Tanzania waliamini timu hiyo ingefungwa goli nyingi.
Hata hivyo Simba iliziba njia za Wydad kwa muda mwingi na kuufanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi kwa wenyeji.
Ili kulaimisha mchezo huo Wydad walifanya mabadiliko ya wachezaji wanne ambao waliingia kwa awamu mbili huku Simba wakifanya mabadiliko ya wachezaji wawili Erasto Nyoni aliyechukua nafasi ya Jean Baleke na Kibu Denis nafasi yake alichukua Moses Phiri dakika za nyongeza.
Ubora wa Simba ulionekana katika dakika zote za mchezo na mambo yalikuja kubadilika kwenye matuta.
Erasto Nyoni, Saido Ntibazonkiza na Moses Phiri walionesha uwezo wa kupiga penati tofauti na Shomari Kapombe na Clatous Chama ambao walikosa.
Sasa Wydad atakutana na Mamelodi Sundowns kwenye mchezo wa nusu fainali.
0 Comments